WANAOKIHUJUMU CHAMA CHA CUF HAWA HAPA,MAALIM SEIF AWATAJA,SOMA HAPO KUJUA
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad,
ameibuka na kutaja utatu unaojumuisha mwenyekiti wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Jeshi la
Polisi akieleza ndio unaoshirikiana kukihujumu chama hicho, huku akibainisha
mambo tisa anayoeleza kuwa ‘ushahidi wa ushirikiano’ na hujuma hizo.
Akizungumza katika mkutano na wahariri na waandishi
wa habari jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuibuka
kwa mgogoro ndani ya chama hicho baada ya Jaji Mutungi kumtambua profesa
Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif alitumia dakika 95 kueleza
hujuma hizo na kudai zinalenga kukifanya chama hicho kutodai haki ya
kunyang’anywa ushindi wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar.
Akiwa sambamba na viongozi mbalimbali wa chama
hicho, alisema hana ugomvi na Profesa Lipumba na yupo tayari kukaa naye meza
moja kueleza uongo wa mtaalamu huyo wa uchumi, ikiwa ni pamoja na ukweli
anaouficha kuhusu kujiuzulu kwake uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana na uamuzi
wake wa kutaka kurejea katika chama hicho.
Mbali na kukiri CUF kupitia katika wakati mgumu kwa
sasa, Maalim Seif alisema hujuma hizo zilizotokana na ‘wakubwa’ kuchukizwa na
kitendo cha chama hicho kuwasilisha vielelezo Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa
(ICC) vinavyowatuhumu viongozi wa Serikali kutumia mamlaka yao vibaya katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, zimesababisha chama hicho kutopata ruzuku ya
Sh milioni 117 kila mwezi, tangu Agosti mwaka huu.
“Mtiririko wa matukio haya (tisa)
yanaonesha wazi hujuma hizi…, ni mambo yanayoratibiwa kwa
suhirikiano wa makusudi kati ya msajili, polisi na Lipumba,
“ alisema Maalim Seif.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuvamiwa kwa Mkutano
Mkuu wa CUF iliofanyika Agosti 21, utekaji wa wanachama na viongozi wa chama
hicho, kuvamiwa kwa ofisi kuu iliyopo Buguruni, kuvunjwa kwa ofisi za wilaya ya
Bagamoyo na Mkuranga, wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la chama
hicho kuzuiwa kufanya kikao cha ndani.
Mengine ni kuzuiwa kufanyika kwa mkutano mkuu
maalumu wilaya ya Tanga, utekaji wa mlinzi wa chama hicho uliofanyika Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuzuiwa kwa kikao cha ndani mkoani Mtwara pamoja na
walinzi wa Profesa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa CUF kuingia chumba cha
mahakama kuu hiyo.
Agosti 8 mwaka jana Profesa Lipumba alitangaza
kuachana na uongozi wa chama hicho, baada ya CUF kukubaliana na Ukawa
kumsimamisha Edward Lowassa kuwania urais.
Hata hivyo, Juni mwaka huu Profesa huyo aliomba kwa
barua kurejea kwenye wadhifa wake, ambao kwa sasa unashikiliwa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro aliyechaguliwa katika mkutano wa
Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho.
Uamuzi wake huo ulizua sintofahamu ndani ya
CUF huku mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho uliofanyika Agosti 21
mwaka huu kumchagua mwenyekiti mpya ukivunjika baada ya kundi la wafuasi wa
chama hicho kuvamia na kufanikiwa kuzima mchakato wa kupiga kura kumchagua
mwenyekiti mpya, wakishinikiza Profesa Lipumba aruhusiwe kurejea katika wadhifa
huo.
Baada ya sakata hilo Baraza Kuu la Uongozi la chama
hicho lilimvua uanachama Profesa Lipumba na kuwasimamisha uanachama makada
kadhaa wa CUF, jambo ambalo liliingiliwa kati na Msajili wa Vyama vya Siasa
aliyetoa waraka wa kumtambua Lipumba kuwa mwenyekiti.
Kitendo cha Lipumba kutambuliwa na kurejea katika
chama hicho kilisababisha Baraza la Wadhamini la CUF kufungua kesi Mahakama Kuu
na kumshtaki profesa huyo Jaji Mutungi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju.
Katika ufafanuzi wake, Maalim Seif alisema Lipumba
alivamia Mkutano Mkuu wa chama hicho akiongozwa na polisi na kusababisha vurugu
kubwa sambamba na uharibifu wa mali lakini polisi haikuchukua hatua yoyote.
“Kumekuwa na matukio kadha aya utekaji
wa viongozi na wanachama wa CUF…, mkurugenzi wetu wa fedha Joram Bashange
alitekwa akiwa anatoka nyumbani kwake na walinzi wa Lipumba, licha ya kukamatwa
na kufikishwa polisi waliachiwa na gari walilotumia nalo halipo kituo cha
polisi buguruni,” alisema.
Alisema Septemba 24 mwaka huu, Lipumba na wafuasi
wake walivamia ofisi kuu ya CUF iliyopo Buguruni na kufanya uharibifu huku
akipewa ulinzi mkali wa polisi.
“Polisi kazi yao ni ulinzi wa raia na
mali zao pamoja na kupambana na wahalifu lakini hivi sasa wao ndio wanatetea
wahalifu. Tunamuomba Mwigulu (Nchemba-Waziri wa Mambo ya Ndani) kuingilia kati
na kutizama watendaji walio chini ya wizara yake,”
alisema Maalim Seif.
Alisema tukio la nne ambalo polisi imeshindwa
kukamata wahusika licha ya kuwajua ni uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Lipumba
wa kuvunja ofisi za chama hicho wilayani Bagamoyo na Mkuranga.
“Wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la
uongozi la chama walizuiwa kufanya kikao cha ndani Newala na kukamatwa
walipokuwa Nachingwea,” alisema na kubainisha kuwa wakati
viongozi hao wakikamatwa, Lipumba anafanya vikao kama hivyo bila kukamatwa.
“Polisi walizuia kufanyika kwa mkutano
mkuu maalum wa wilaya ya Tanga kwa madai kuna pande mbili zinavutana. Pia
Novemba 10 mwaka huu mlinzi wa chama, Mohamed Said alitekwa akiwa mahakama kuu
na kupigwa sana na kunyang’anywa fedha na kupelekwa kuhojiwa na Lipumba. Tukio
hilo lilitokea mbele ya polisi,” alisema.
Alisema jeshi hilo pia lilizuia kufanyika kwa kikao
cha ndani mkoani Mtwara pamoja na walinzi wa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa
CUF kuingia ndani ya chumba cha mahakama kufuatilia shauri lao, huku akimtaja
mmoja wa walinzi hao kuwa ni Hassan Kingwele.
Akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Lipumba,
Maalim alisema msomi huyo anatumiwa na dola na kubainisha kuwa anaficha
ukweli juu ya uamuzi wake wa kujiondoa CUF.
“Lipumba bado hajasema sababu za kweli
juu ya kujiuzulu kwake, yeye ndio alikuwa mwanzilishi wa Ukawa katika Bunge
Maalum la Katiba na ndio aliyemtafuta Lowassa na kumshawishi awanie urais
kupitia Ukawa,” alisema.
“Lowassa ilikuwa ajiunge na NCCR kwa
sababu ni chama kidogo ili CUF na Chadema tumuunge mkono kwa mantiki hiyo iweje
Lipumba aseme mimi sikumshirikisha ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa?”
Alisema yeye hana ugomvi na Lipumba bali mtaalam
huyo wa uchumi ana ugomvi na CUF, huku akidai kuwa hivi sasa anatumia udini,
ukabila na uzanzibari kukigawa chama hicho.
“Hizi ni jitihada za dola kunifanya
nisidai haki kwa yaliyotokea Zanzibar…, hilo halitawezekana nitaidai tu mpaka
mwisho,” alisema.