TRA YAFIKIA MALENGO YAKE KATIKA UKUSANYAJI KODI KWA MWEZI WA OCTOBA,SOMA HAPO KUJUA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikia
kukusanya shilingi trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba ikiwa ni kukamilisha malengo
waliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa kodi Bw. Richard Kayombo wakati wa mkutano na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam kuhusu hali ya makusanyo na zoezi la uhakiki wa
namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN)linaloendelea hivi sasa.
“Tumefanikiwa kukusanya shilingi
Trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa ni kufanikisha malengo ya
ukusanyaji kodi nchini ili kukuza uchumi wa nchi pamoja kusaidia Serikali
kuendeleza huduma za jamii nchini” amesema Bw. Kayombo.
Aidha Bw. Kayombo amesema kuwa mapato hayo
yametokana na mikakati thabiti iliyowekwa na mamlaka hiyo katika ukusanyaji
kodi hapa nchini ili kuweza kusaidia ongezeko la pato la Taifa .
Katika hatua nyingine TRA imefanikiwa kushinda kesi
9 kati ya 10 zilizokuwa zikiendelea katika mahakama mbalimbali nchini dhidi ya
walipa kodi wake na kufanikiwa kupata kiasi cha takribani Bilioni 16.9 .
“Tumefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10
ambazo zilifikishwa mahakamani dhidi ya walipa kodi na kupata kiasi cha
shilingi bilioni 16.9 hivyo kufanya juhudi zetu za kukusanya mapato mengi
zaidi” aliongeza Bw. Kayombo.
Mbali na hayo Bw. Kayombo amesema kuwa zoezi la
uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi ambalo limeanza hivi karibuni
linaendelea na litafikia tamati Novemba 30 mwaka huu kwa mkoa Dar es salaam
hivyo wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya uhakiki huo.
Aidha Bw. Kayombo ameongeza kuwa kila mwenye
namba ya utambulisho wa mlipa kodi anatakiwa akahakiki kwa ajili ya kupata
taarifa sahihi za mlipa kodi ili kuepuka kufutwa kwa namba yake ya
utambulisho baada ya zoezi hilo kumalizika kwa mkoa husika.