SERIKALI MBIONI KURUHUSU POMBE YA GONGO,SOMA HAPO KUJUA
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage amezishauri kampuni zinazotengeneza vilevi kutengeneza pombe yenye
ladha ya gongo, kwa kuwa baadhi ya wateja wanavutiwa na ladha hiyo wana
wanakipenda kinywaji hicho.
Mwijage ameyasema hayo leo bungeni mjini Dodoma
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Gimbi Masaba (Chadema)
aliyehoji mpango wa serikali wa kuanzisha na kuhalalisha viwanda vya
kutengeneza pombe aina ya gongo ili kuchochea uchumi wa nchi na kubainisha
kuwa, gongo ikitengenezwa kiwandani itafuata ubora unaotakiwa kisheria.
“Moja ya kigezo muhimu cha kuanzisha
kiwanda ni uwepo wa soko, kutokana na wananchi kupenda kinywaji hiki(gongo)
nawashauri wadau wa sekta hii kuwasiliana na ofisi za Sido ambazo zinapatikana
mikoa yote ili kupata muongozo juu ya uanzishaji wa viwanda bora na salama vya
aina hii,” alisema Mwijage.
Amesema haiwezekani Serikali kuhalalisha gongo, ila
inaishauri sekta binafsi kuanzisha viwanda vitakavyotumia malighafi
zinazotengeneza kinywaji hicho kwa lengo la kuzalisha kinywaji kinachokidhi
viwango vya usalama na ubora wa chakula.
Katika swali la nyongeza, Masaba amehoji kama
serikali ipo tayari kufanya utafiti kujua faida zilizo kwenye gongo.
Mwijage amesema faida zinafahamika, lakini
atawaelekeza wataalamu wake waendele maeneo yenye gongo na pombe nyingine za
kienyeji ili kuzifanyia utafiti na zitengenezwe kwa kufuata ubora na viwango.