RC MAKONDA AZOMEWA KILA KONA,KAULI ZAKE ZAWASHANGAZA WENGI,SOMA HAPO KUJUA
KAULI mbalimbali zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda wakati wa ziara zake zimezua taharuki jijini humo.
Kwa nyakati mbalimbali wakati wa ziara zake,
Makonda anadaiwa kutoa kauli za vitisho hasa kwa watumishi wa umma.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha ACT-Wazalendo
kimemshtaki mkuu huyo wa mkoa katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na
Utawala Bora ili imuwajibishe.
Katika taarifa yake iliyotumwa jana kwa vyombo vya
habari jijini Dar es Salaam na Katibu wa Ngome ya Wanawake wa chama hicho,
Esther Kyamba alisema kauli alizozitoa Makonda zimewadhalilisha watumishi hao.
“Tumesikitishwa na kuhuzunishwa na kauli
zisizo za kiuongozi na zisizozingatia kanuni za maadili ya utumishi wa umma
zinazoendelea kutolewa na RC Makonda.
“Jana (juzi), katika mkutano anaouita wa
kutatua kero kwa wakazi wa Dar es Salaam aliendelea kushindwa kutatua kero na
badala yake kuongeza kero ya kudhihaki, kudhalilisha kukejeli na kutukana
hadharani wananchi anaowaongoza na watumishi anaowasimamia kitendo ambacho ni
kinyume na maadili ya Watanzania,” alisema.
Kyamba alisema kitendo cha Makonda kumtolea lugha ya
udhalilishaji Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni, Rehema Mwinuka akiwa
Mabwepande kwa kumtamkia kwamba “Hawa ndio vichaa tunaohangaika nao, toka
hapa”. Hakikubaliki.
“Kauli hiyo imetushtua sana,tunalaani
kwa nguvu zetu zote, kauli kama hii si tu haikupaswa kutolewa na kiongozi
mkubwa katika ngazi ya mkoa lakini pia ni kauli mbaya ambayo ililenga
kumdhalilisha Rehema na kumvunjia heshima yake mbele ya umma,”
alisisitiza.
Alisema kutokana na udhalilishaji huo uliofanywa na
Makonda, wameshawasilisha mashtaka yao dhidi yake mbele ya Tume, wakiitaka
imwajibishe kwa kitendo chake hicho cha utovu wa nidhamu na maadili ya utumishi
wa umma.
“Ngome inamtaka mkuu huyo wa mkoa
kutambua kuwa kwa kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na
Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma, kanuni ya 65(1) inamtaka mtumishi wa
umma, “kuepuka kufanya vitendo viovu au kutamka maneno yanayolenga kuwaaibisha
watumishi wa ngazi moja, za chini yao au wa vyeo vya juu,”
alisema.
Alisema kitendo alichofanya, kumwaibisha na kumtolea
lugha ya udhalilishaji, Mwinuka ni kinyume cha Sheria na Kanuni za Utendaji
katika Utumishi wa Umma.
“Tunaitaka Tume ifanye uchunguzi na
kuchukua hatua dhidi ya matamshi mbalimbali yaliyotolewa na Makonda ambayo
yalikiuka sheria ya Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.
“Tunayataka mashirika na asasi
mbalimbali zinazosimamia haki za binadamu, haki za jinsia na utawala bora
kupaza sauti dhidi ya kauli isiyo ya kiuongozi ya Makonda, Ngome na Chama
kwa ujumla tutaendelea kuwasemea wanyonge wote popote walipo kwa kadri ya uwezo
wetu,” alisema