PROFESA NDALICHAKO AZIDI KINGIWA KIFUA,WIZARA YAKE YAIBUKA NA KUTOA UFAFANUZI,SOMA HAPO KUJUA
WIZARA
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa ufafanuzi kwamba
haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa kujiunga na vyuo vikuu
badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli kidato cha nne na cha sita
kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti vyenye sifa.
Aidha,
imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni wajibu wa waajiri
wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na kutumia fursa hiyo kufanya
mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.
Naibu
Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana Dar es Salaam
kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni kwamba serikali imepiga
marufuku watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia
ni wenye sifa za kidato cha sita.
Manyanya
alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na sifa za
shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya kufanya mitihani hiyo
waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa
sifa ya kusoma vyuo vikuu.
“Ni
vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu anakaa nafasi
kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki utafanyika kwa vyeti na
wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu Waziri.
Alisema
kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa hazitakiwi kwa
wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia
njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa
taarifa tayari wanayo.
“Kilichoongelewa
siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha sita waliofeli kuingia kwenye
‘foundation course’ na diploma haikutajwa pale kwa kuwa haikuulizwa na hakuna
kauli iliyotajwa pale kukataza watu wa diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya
akirejea kauli ya Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika
mahafali ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.
Profesa
Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
“Nami
ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei mtu sifa. Kama
sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha sita, kama amefeli Baraza
la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa nini anakwepa kule? Kwa nini? Kwa
nini tunataka tuendeleze uchochoro,” alieleza Waziri Ndalichako.
Naibu
Waziri alisema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia ya moja kwa
moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na kinasimamiwa na
mamlaka husika ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wawe na
ufaulu mzuri.
“Tanzania
imejiwekea mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi za kimataifa katika
utoaji wa elimu na hapo awali tulikusudia kuhakikisha elimu inatolewa kwa watu
wengi zaidi na hizo fursa zinawafikia wadau wote katika ngazi mbalimbali kwa
kupanua elimu ya msingi hadi vyuo vikuu,” alieleza Naibu Waziri.
Alisema
walitambua kuna wadau mbalimbali walitamani kusoma vyuo vikuu, lakini hawapati
hiyo fursa na ndiyo wakaanzisha mfumo huo wa Chuo Kikuu Huria na mtu anaweza kusoma
alipo na mfumo umekuwa ukiboreshwa siku hadi siku.
Alisema
iliwekwa mifumo ya vyeti na ngazi zake kulingana na vigezo na hivyo siyo kila
cheti kinachotolewa kinaruhusu mtu kwenda ngazi nyingine na kila mamlaka
imepewa jukumu ili kulinda ubora wa elimu unaotolewa nchini.
Naibu
Waziri alisema kutokana na uanzishwaji wa vyuo mbalimbali kumejitokeza
changamoto na watu kutoka katika mfumo rasmi uliopangwa na kujiwekea mifumo
binafsi ambayo imeingiza hata wanafunzi wa kidato cha nne ambao hawana sifa kuingia
vyuo vikuu.
“Jambo
hilo limesababisha kuwepo kwa msuguano, haiwezekani mtu afeli kidato cha nne
bila kuwa na cheti kingine chochote anaingizwa katika kozi hiyo halafu
anaingizwa chuo kikuu, sisi hatujarasimisha mfumo huo wa ‘foundation course’ na
hatuna vipimo vyake,” alieleza.
Alisema
kwa kawaida mwanafunzi mwenye diploma inayotambulika wamewekewa usawa wa alama
fulani na kidato cha sita hivyo wanakuwa na sifa ya kuingia vyuo, lakini siyo
waliofeli hivyo wanatakiwa kufanya utafiti zaidi katika kozi hiyo.
“Haiwezekani
kila mtu akajianzishia mfumo wake tu, tulifikia eneo ambalo si zuri kama nchi
na sasa tutaimarisha ubora…ukifeli kidato cha nne unatakiwa kwenda kusoma na
kupata cheti kwenye mtaala unaotambulika na ukaenda diploma na unapofaulu
unaweza kwenda chuo kikuu,” aliongeza.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila alisema suala la
‘Foundation course’ limelenga kumuandaa mtu mwenye sifa ambaye amekuwa nje ya
mfumo kwa muda mrefu ili kuingia chuo kikuu, lakini walichokuwa wakikifanya
wengi ni kuwachukua waliofeli kidato cha nne na sita na kuwaingiza katika kozi
hiyo na hatimaye kuwaingiza chuo kikuu.