CHADEMA NI KIBOKO,YAJA NA MPANGO WA KUACHANA NA RUZUKU ZA SERIKALI,SOMA HAPO KUJUA
Chadema imetangaza kuwa Januari itaanza kutumia kadi
mpya za uanachama za kielektroniki, zitakazoiwezesha kukusanya Sh13.9 bilioni
kwa mwaka na kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali.
Mkakati huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa chama
hicho Freeman Mbowe wakati wa mkutano wa ndani uliofanyika mkoani Morogoro.
Tofauti na Mbowe, viongozi wengine wa chama hicho walioko mikaoni ni Edward
Lowassa aliyeko Dodoma na Frederick Sumaye ambaye yupo Singida.
Mbowe alisema mfumo huo utasaidia pia kudhibiti
baadhi ya viongozi wasio waaminifu, wanaotumia mwanya wa kuuza kadi na
kushindwa kuwasilisha fedha kwenye hazina ya chama.
Alisema kwa mfumo huo mpya, kama Chadema itakuwa na
wastani wa wanachama 100,000 katika wilaya moja na kila mmoja kulipa ada ya
Sh1,000 kwa mwaka, maana yake itaingiza Sh100 milioni.
Kwa hoja hiyo ya Mbowe, ikiwa chama hicho kitakuwa
na wastani wa wanachama 100,000 katika kila wilaya za Tanzania Bara ambazo ni
139, Chadema itakuwa na uwezo wa kukusanya Sh13.9 bilioni kila mwaka.
Vyama vya siasa vinapata ruzuku kwa mujibu wa sheria
na ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
ilibainisha kuwa jumla ya Sh67.7 bilioni zililipwa na Serikali kwa vyama vya
siasa katika mwaka kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka wa fedha 2009/2010
mpaka 2012/2013. Fedha ambazo kwa mujibu wa CAG zilikuwa hazijakaguliwa
kisheria.
Ikilinganishwa na mkakati mpya wa Chadema, fedha
hizo ni ndogo katika kuhudumia shughuli za chama nchi nzima.
Mbowe alisema Chadema imeamua kuhakiki wanachama
wake ili ifikapo Januari iwe tayari imemaliza kazi hiyo na kuingia rasmi katika
mfumo mpya, utakaokisaidia kuondokana na dhana ya utegemezi wa ruzuku kutoka
serikalini.
Alisema ili chama kipige hatua na kuondokana na
utegemezi wa ruzuku serikalini, wamekusudia kuingia katika mfumo wa kupata
mapato kutoka ndani ya wanachama kupitia ulipaji wa ada.
Mbowe alizungumza na wanachama hao kutoka ngazi za
vitongoji, vijiji, kata na wilaya waliohudhuria mkutano mkuu maalumu wenye
lengo la kuwakumbusha mambo mbalimbali ya kuimarisha chama hicho baada ya
Serikali ya Rais Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara.
“Katika kipindi cha miaka miwili ijayo,
Chadema itakuwa tayari imefanya utambuzi wa wanachama wake kwa kuwatambua
katika kila mtaa, kitongoji, kijiji, kata na jimbo kupitia mfumo mpya wa kadi
za eleketroniki ifikapo Januari 2017,” alisema Mbowe.
Alisema katika baadhi ya maeneo ya mikoa hapa
nchini, kadi za uanachama za Chadema ni lulu na zimekuwa zikiuzwa hadi Sh5,000
badala ya 500.
Alieleza kuwa mapato ya chama lazima yatokane na ada
za wanachama na siyo ruzuku ya Serikali, kwa kuwa utegemezi wa ruzuku ni hatari
kwa uhai wake.
“Hii ruzuku inayotolewa na Serikali
inatolewa kwa sababu ya CCM na CCM bila ruzuku hakiwezi kujiendesha,” alidai.
Mbowe alisema kila jimbo linapata fedha za ruzuku
kulingana na idadi ya kura ilizopata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka
jana, akitolea mfano Jimbo la Mlimba kuwa Mbunge Suzan Kiwanga alishinda kwa
kura 40,000 wakati urais Chadema ilipata kura 38,000 huku katika udiwani
wakipata kata tisa kati 16.
“Kutokana na ruzuku, Mlimba itapata
Sh163,688 kila mwezi. Unaweza kuona fedha za ruzuku kutoka ndani ya chama ni
ndogo sana ambapo Mkoa wa Morogoro unapokea kiasi cha Sh2.2 milioni kila mwezi.
“Kufikia mwaka 2017 kupitia programu ya
Chadema msingi, tumekusudia kukijikita zaidi kusaka wanachama kutoka ngazi ya
mitaa, vitongoji na balozi na tutaanza uchaguzi ndani ya chama.
“Tumebaini kuwa baadhi ya maeneo Chadema
tumeshindwa kupata wenyeviti wa Serikali ya vitongoji na vijiji, kukosa
madiwani na wabunge kutokana na kukosa misingi imara wa wanachama,” alisema
Mbowe