VIONGOZI WADINI WAENDELEA KUMNGOJEA RAIS MAGUFULI NI KUHUSU OPARESHENI UKUTA,SOMA HAPO KUJUA
Viongozi wa dini nchini waliopanga kumwona Rais John
Magufuli kwa mazungumzo kuhusu hali ya siasa nchini wanaendelea kusubiri maombi
yao kujibiwa licha ya kupita zaidi ya siku 90 sasa.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Askofu Frederick Shoo jana alisema: “Siwezi kusema Rais
amekataa kuonana nasi, hapana. Labda ni kwa lile tulilokuwa tuende kumuona nalo
(Ukuta) lakini kwa mazungumzo mengine milango ya Rais iko wazi,”
alisema.
Wazo la viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu
kutaka kuonana na Rais lilibuniwa Agosti ili kuzuia maafa ambayo yangejitokeza
baada ya Chadema kutangaza kufanya maandamano waliyoyapa jina la Ukuta,
Septemba Mosi.
Hata hivyo, Dk Shoo alielekeza atafutwe Katibu wa
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Dk Leonard Mtaita kwa maelezo
zaidi akisema ni mmoja wa wanaoratibu suala hilo.
Dk Mtaita alipotafutwa kwa mara ya kwanza Septemba
azungumzie kama barua waliyopeleka kwa Rais imejibiwa alisema tetemeko la ardhi
lililotokea mkoani Kagera na kusababisha maafa makubwa litachelewesha mpango
wao wa kukutana na Rais.
Hata hivyo alipotafutwa tena jana, Dk Mtaita aliomba
atafutwe mwenyekiti mwenza wa kikao kilichoibuka na wazo hilo ambaye ni Sheikh
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim.
“Tumewaachia wenzetu walioko Dar es
Salaam, Sheikh Salim ndiye mwenyekiti mwenza na yeye yuko Dar na ndiye
alijitolea kufanya mawasiliano na Mheshimiwa Rais,”
alisema Dk Mtaita.
Sheikh Salim alipotafutwa ili aeleze alipofikia
kufanikisha kuonana na Rais alijibu kwa kifupi tu: “Sisi tuko katika
kusubiri. Barua tulishatuma kwa Mheshimiwa Rais. Tunasubiri tu”.
Msemaji wa Serikali, Hassan Abass alipoulizwa
alitaka atafutwe Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kwa
kuwa ndiye msemaji wa Rais.
“Mtafute Msigwa maana yeye yupo karibu
na Mheshimiwa (Rais Magufuli) na anajua ratiba zote,” alieleza.
Alipotafutwa, Msigwa aliwataka viongozi hao
kuendelea kusubiri kwa kuwa kila kitu kina utaratibu wake na pia inategemea
ratiba ya Rais.
“Kama wameandika, wasubiri watajibiwa,”
alisema Msigwa.
Viongozi wa Chadema wanaposoma Katiba na Sheria ya
Vyama vya Siasa wanaona wana haki ya kufanya mikutano ya ndani na hadhara na
maandamano mradi tu Jeshi la Polisi litaarifiwe siku na mahali pa shughuli
hiyo.
Rais Magufuli alipiga marufuku siasa za ushindani
hadi mwaka 2020 jambo ambalo Chadema waliamua kujitokeza kupinga kwa
maandamano.
Mbali ya Rais Magufuli, Jeshi la Polisi lilitangaza
kuwa ni marufuku kufanya mikutano na maandamano.
Hali hiyo iliyotishia kuwepo makabiliano yenye maafa
ndiyo iliyowaibua viongozi wa dini ambao walichukua hatua kwanza kuwasihi
viongozi wa Chadema na pili kuwataka wasubiri mrejesho.