WANAHARAKATI WA LHRC WATOA NENO KUHUSU SIKU YA WANAWAKE DUNIANI,SOMA HAPO KUJUA
Leo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana
na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, siku ambayo
ilipitishwa na Umoja wa mataifa mnamo Oktoba 11, 2011. Kauli
mbiu ya kitaifa kwa mwaka huu ni ‘‘Mimba na ndoa za Utotoni zinaepukika, Chukua
hatua kumlinda mtoto wa kike’’.
Hivyo basi katika kuadhimisha siku hii Kituo
kimeangazia mtoto wa kike hapa Tanzania na changamoto anazokumbana nazo. Kwa
mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto wa
kike kati ya umri wa miaka 0-17 hapa Tanzania ni 11,263,891 idadi ambayo
ni sawa na asilimia 48.8 ya watoto wote chini ya miaka 17, ambapo Tanzania
bara kuna watoto wa kike elfu 10,943,846 na Tanzania visiwani
idadi yake ni laki 320,045.
Hivyo basi nusu ya idadi hii ni wanawake na
watoto ikilinganishwa na idadi ya watanzania wote ambao ni milioni
44,928,923 ambapo kati yao wanawake ni milioni 23,058,933.
Inasikitisha kuona kuwa mtoto wa kike hapa nchini
bado amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi na cha kusikitisha zaidi mtoto
huyu anaanza kubaguliwa kuanzia katika ngazi ya familia.
Katika familia nyingi za kitanzania mtoto wa kike
amekuwa akikosa fursa ya kupata Elimu ukilinganisha na mtoto wa kiume na katika
mazingira mengine wazazi wamediriki hata kuwaozesha watoto wao wa kike kwa
ajili ya kupata fedha ya kusomesha watoto wa kiume. Ukiangalia pia katika suala
zima la Elimu ni ukweli usiofichika kuwa idadi ya wasichana wanaoshindwa
kumaliza masomo kwa sababu za kupata mimba imekuwa ikiongezeka.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la watoto
duniani UNICEF kumekuwa na ongezeko la mimba mashuleni kutoka asilimia 23 hadi
26 yaani takribani watoto wa kike 8000 hapa Tanzania kila mwaka hukatisha
masomo kwa ajili ya ujauzito. Vile vile idadi ya watoto wa kike ambao wamekuwa
wakimaliza Elimu ya msingi lakini kutokupewa nafasi ya kujiendeleza kielimu
hata pale wanapokuwa wamefaulu nayo pia imekuwa ikiongezeka na badala yake
mabinti hawa wamekuwa wakilazimika kuingia katika ndoa katika umri mdogo.
Hali hii ya Watoto wakike kutokupata fursa ya elimu
husababisha ongezeko kubwa la watoto wa kike wanaosafirishwa kutoka vijijini na
kuletwa mijini kwa minajili ya kuja kuendelezwa kielimu na matokeo yake mabinti
hawa wamejikuta katika wakati mgumu kwa kufanyishwa kazi za ndani bila malipo
stahiki na wakifanyiwa vitendo vingi vya kikatili na vya kuwadhililisha.
Hali hii imepelekea mabinti wengine kutoroka kutoka
kwa waajiri wao na kuanza kuishi mtaani na hivyo kurubuniwa na kujiingiza
katika biashara za ngono na wengine hata madawa ya kulevya.
Tumeendelea pia kushuhudia kuongezeka kwa vitendo
vya ukatili wa kingono kama ubakaji na ulawiti kwa Watoto wa kike na cha
kusikitisha zaidi vitendo hivi vimekuwa vikifanywa na Ndugu wa karibu sana wa
Watoto hawa wakiwemo wazazi, walezi, majirani na hata walimu huko mashuleni.
matukio haya yamekuwa hayafikishwi Katika vyombo vya Sheria kwani mengi
huzungumzwa kifamilia na kuwaacha watuhumiwa wakiendelea na maisha yao.
Tanzania pia ni nchi moja wapo yenye idadi kubwa ya
ndoa za utotoni kwa takribani ya asilimia 35 watoto wa kike hapa nchini
huozeshwa nchini ya umri wa miaka 18 na hivyo kukatishwa ndoto zao za
kujiendeleza kielemu na hata ustawi mzima wa maisha yao.
Inasikitisha zaidi kuona pia pamoja na juhudi
mbalimbali za utetezi na ushawishi wa wanaharakati katika kupinga vitendo hivi
viovu na mila kandamizi bado Ukeketaji umekuwa ni tatizo kubwa sana hapa
nchini. Kwa mujibu wa takwimu za Viashiria vya Idadi ya watu na afya 2010,
asilimia 14.6% ya wanawake Tanzania wamekeketwa na wengi wao ni watoto wa kike.
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa mbinu mpya
zimekuwa zikibuniwa ikiwemo kukeketa watoto mara wanapozaliwa.
Vilevile, kwa mujibu wa taarifa ya haki za Binadamu
ya mwaka 2015 inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kila mwaka
ongezeko la matukio ya Ukatili kwa watoto ikiwemo watoto wa kike kupewa adhabu
kali ambazo hazilingani na makosa waliyoyafanya, mfano unakuta mtoto anachomwa
mikono moto kwa kosa la kuunguza mboga.
Kwa kifupi watoto wa kike wanapata athari
mbalimbali ikiwemo;
Kuendelea kudidimiza nafasi ya mwanamke katika Jamii
na taifa zima kwa ujumla na kuendeleza mfumo dume kwani ukatili mwingi huanzia
katika ngazi ya familia
Kutokuendelezwa kielimu kwa mtoto wa kike na hii
hupelekea kuendelea kuwa na idadi kubwa ya Wanawake ambao hawana Elimu na hivyo
kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume na pia kushindwa kujikwamua kiuchumi.
Idadi kubwa ya athari za kiafya zinazowapata watoto
wa kike kwa ajili ya kujifungua katika umri mdogo ambayo husababisha wengine
kupoteza maisha, kupatwa na fistula na maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja
na magonjwa mengine ya zinaa.
Malezi duni ya watoto kwa kuwa watoto hawa wanakuwa
bado ni wadogo kuweza kukabiliana na jukumu kubwa la malezi na matunzo ya
familia.
Kuendelea kuongezeka kwa Ukatili na unyanyasaji wa
kijinsia kwani watoto hawa mara nyingi huolewa na watu waliowazidi umri sana na
hivyo kutokuwa na maamuzi yoyote katika nyumba.
Hivyo basi tunapendekeza yafuatayo:
Katika ngazi ya familia wazazi na walezi kuthamini
na kuwajali watoto bila ubaguzi wa jinsi zao. Watoto wote wapewe fursa sawa
kielimu na kujiendeleza kimaisha. Wazazi kuwalinda watoto dhidi ya vitendo
vyote vya Ukatili hasa Ukatili unaoanzia majumbani,sambamba na hilo kutoa
taarifa za matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto na sio kutatua matatizo haya
katika ngazi ya familia ilihali haki ya mtoto inapotezwa.
Wito kwa Jamii kuwajibika katika kuwalinda watoto
dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili. Kuthamini nafasi ya kila mtoto na kuona
mtoto wa mwenzako ni wa kwako; pia kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili katika
maeneo wanayoishi na sio kufumbia macho na kuwaficha waovu.
Serikali kuhakikisha kuwa sheria zilizopo
zinasimamiwa na zinatekelezwa pale zinapovunjwa kwa kuweka mifumo iliyowazi na
rahisi ya kupata na kufuatilia haki
. Vile vile kubadilisha sheria ambazo bado zimekuwa
ni kandamizi kwa mtoto wa kike ikiwemo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoafiki
mtoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 15. Serikali itekeleze agizo
lilitolewa na Mahakama Kuu Julai 8 2016 la kubadili kifungu na 13 cha sheria ya
ndoa 1971 juu ya ndoa za utotoni
Serikali kwa kupitia taasisi zake kama polisi na
mahakama kuhakikisha kuwa Mashauri yanapolekwa Mahakamani yanasikilizwa bila
vikwazo na kutolewa maamuzi kwa wakati stahiki maana ‘justice delayed is
justice denied’ – ‘kuchelewesha haki ni kunyima haki’.
Wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa
ya matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto ili wale wanaofanya vitendo hivi
waaibishwe na waadhibiwe kwa mujibu wa sheria; tunavitaka vyombo vya Habari
visiishie tu kuripoti matukio haya pindi yanapofanyika bali hata kuendelea
kufuatilia mashauri yaliyopo mahakamani ili kusaidia mashauri haya yafanyiwe
kazi kwa wakati.
Pamoja na hilo tunaviomba vyombo vya habari kuwa
makini jinsi wanavyoripotia matukio haya ya Ukatili kwa watoto kwani utoaji wa
taarifa hizi wakati mwingine umekuwa pia ukiendelea kuwavunjia haki watoto hawa
kwa kutozingatia sheria inayotaka utoaji wa taarifa za watoto kutunza majina
halisi ya watoto na hata sura zao.
Na mwisho kabisa tunaomba viongozi wetu katika ngazi
zote za kijamii na hata kitaifa kuibeba ajenda ya haki za watoto na hususani
haki za watoto wa kike kama ajenda ya kitaifa ili kuhakikisha wanalindwa dhidi
ya vitendo viovu na wana mazingira salama ya kukua na kuwa watu wema na
mustakabali mzuri wa maisha yao ya sasa na ya baadae.
Tunawashukuru sana.
Wasalaam, Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu
Dr. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji