UDOM NA UDSM KUTOKEA VURUGU,SAKATA LA MIKOPPO KWA WANAFUNZI LAFIKIA PABAYA,SOMA HAPO KUJUA
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM) ni vyuo ambavyo serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
juu hapa nchini (HESLB) inatarajia kuvinyima baadhi ya fedha za ada za
wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2016/2017, anaandika Charles William.
Uamuzi wa kuvinyima fedha vyuo hivyo
utachukuliwa ili kufidia upotevu wa fedha zinazofikia Sh. 650 milioni kutokana
na uwepo wa wanafunzi hewa katika vyuo hivyo.
Prof. Simon Msanjila, Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya
Elimu, Mafunzo ya Ufundi amewambia wabunge wa Kamati ya Katiba na Sheria leo
kuwa vyuo vilivyokutwa na wanafunzi hewa ambao walikuwa wakilipwa mikopo
vimeitia hasara kubwa serikali na hivyo lazima viadhibiwe.
“Mpaka sasa serikali imekusanya Sh. 1.50 bilioni
pekee kutoka katika vyuo vilivyokutwa na wanafunzi hewa huku UDSM na UDOM
vikikutwa na idadi kubwa ya wanafunzi hewa.
“Tuliwaandikia barua kuwataka walipe au watoe
maelezo juu ya walipo wanafunzi hao ambao tayari walikuwa wameshalipwa jumla ya
Sh. 3.85 bilioni ilihali hawapo vyuoni,” amesema Msanjila.
Uamuzi wa serikali kukata fedha za ada za vyuo vikuu
vilivyoshindwa kurejesha fedha zinazodaiwa kulipwa kwa wanafunzi hewa
utavifanya vyuo hivyo, kukosa mamilioni ya fedha ambazo hutumika kuendesha
shughuli zao za kila siku.
Kuhusu baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo ingawa wana
sifa, Msanjila amesema wanafunzi wengi wamekuwa wakijaza taarifa za uongo
katika fomu zao za maombi na hivyo kufanya bodi ya mikopo iwanyime mikopo hiyo.
“Utakuta mwanafunzi, baba yake ni fundi vyuma lakini
anajaza kwenye fomu kuwa ni mhandisi au mama yake labda ni mpika vitumbua
lakini yeye anajaza kuwa ni mfanyabiashara. Sasa mwanafunzi kama huyo tutampaje
mkopo asilimia mia moja?” amesema Msanjila.
Katika orodha ya wanafunzi hewa wa vyuo vikuu hapa
nchini, iliyotolewa na waziri Joyce Ndalichako tarehe 27 Agosti mwaka huu, UDSM
iliongoza kwa kuwa na wanafunzi hewa 350 ambao waliolipwa Sh. 703.4
milioni huku ikifuatiwa na UDOM iliyokuwa na wanafunzi hewa 364 waliolipwa Sh.
460.9 milioni.
Vyuo hivyo vilitoa maelezo juu ya wanafunzi hao
kukosekana wakati wa uhakiki huku vikipewa fursa ya kuwatafuta ili wahakikiwe
hata hivyo baadhi yao walikosekana kabisa, kwahiyo vyuo vitakatwa fedha za ada
zinazofikia Sh. 650 milioni.
Fedha za ada wanafunzi hulipwa na HESLB kwa vyuo
vikuu ikiwa ni sehemu ya mikataba ya wanafunzi wanaolipiwa na serikali. Fedha
hizo hutumika kusaidia uendeshaji vyuo hivyo.