CHADEMA YAKUTANA 'CHOBINGO',SOMA HAPO KUJUA
KAMATI Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), inaanza kikao chake leo, ambacho pamoja na mambo mengine kitajadili
hali ya kiuchumi na kisiasa ya nchi, anaandika Charles William.
Tumaini Makene, Mkuu wa Idara
ya Habari na Mawasiliano wa Chadema amesema kuwa kikao hicho kinakaa kwa siku
mbili jijini Dar es Salaam siku ya leo na kesho (Oktoba 22 na 23).
“Pamoja na mambo mengineyo lakini pia Kamati Kuu
itapokea na kujadili kwa kina hali ya kisiasa hapa nchini na kupitisha mazimio
kadhaa,” amesema.
Katika kikao hicho cha siku mbili huenda Chadema
ikaibuka na mipango mipya ya kujiimarisha katika kipindi hiki ambacho mikutano
ya hadhara ya viongozi wa vyama vya siasa imepigwa marufuku na Rais John
Magufuli.
Itakumbukwa kuwa kikao cha dharura cha CC ya Chadema
kilichokaa mwezi Julai mwaka huu kiliibuka na azimio la kufanya mikutano ya
maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima chini ya mwamvuli wa Umoja wa
Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
Hata hivyo chama hicho kiliahirisha mpango wake huo
uliopangwa kufanyika tarehe 1 Septemba, kwa madai kuwa kiliombwa na viongozi wa
dini kabla ya kutangaza kuachana na mpango huo rasmi mnamo Septemba 30 mwaka
huu na kuahidi kuibuka na mbinu mpya.