CCM WAFANIKISHA FIGISU ZA UMEYA KINONDONI,SOMA HAPO KUJUA
UCHAGUZI wa Meya katika Manispaa ya Kinondoni, Dar
es Salaam leo umevurugwa licha ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijitangazia
ushindi, anaandika
Faki Sosi.
Pamoja na CCM kujitangazia
ushindi, Ukawa wameeleza kuwa, hawatovumilia tena kile walichokiita upuuzi
unaopangwa na CCM kwa kushirikiana na serikali kuwahujumu.
Kauli hiyo imetolewa baada ya vyama vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutibua mkakati wa CCM kisha kususia
uchaguzi huo.
“Kuanzia leo hatutakuwa chama cha kulalamika tena,
tutafuata taratibu za kupambana na uonevu unaoendelea kufanyika nchini,”
amesema Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema akizungumza mbele ya
waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho.
Hata hivyo, baada ya Ukawa kususa uchaguzi huo,
wajumbe wa CCM walijikusanya na kumchagua mmoja wao kuwa Meya wa Kinondoni,
waliomtunuku nafasi hiyo kinyume na utaratibu ni Benjamin Sitta, Diwani wa Kata
ya Msasani.
CCM kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali katika
Wilaya ya Kinondoni wamekuwa wakipanga namna ya kuiangusha Ukawa kwenye
uchaguzi huo jambo ambalo limekuwa likifuatiliwa kwa jicho la karibu na Ukawa
na hata kubaini baadhi ya mbinu hizo.
Ukawa unaowakilishwa na Chadema na Chama cha
Wananchi (CUF) kwenye Manispaa ya Kinondoni, wamegomea uchaguzi huo kutokana na
CCM kuongeza idadi ya wajumbe baada ya wajumbe wa Ukawa kuwa wengi.
Kabla ya kugawanywa kwa Manispaa ya Kinondoni na
kuwa manispaa mbili (Kinondoni na Ubungo), Meya wa Kinondoni alikuwa Boniface
Jacob kutoka Chadema huku naibu wake akiwa Jumanne Amir Mbunju wa CUF.
Baada ya kugawanywa kwa manispaa hiyo, kumeendelea
kuwepo na hekaheka zinazofanywa na vyama vya siasa katika kuhakikisha vinatwaa
manispaa hiyo.
Kutokana na kuibuka kwa sintofahamu kwenye uchaguzi
huo, Ukawa leo wamesusia uchuguzi wa Meya wa Kinondoni kwa madai ya kuondolewa
wajumbe halali wa Ukawa na kuingizwa wajube feki wa CCM.
Uchaguzi huo umevurugwa baada ya wajumbe wa Ukawa
kutoka nje kwa madai kwamba, uchaguzi huo kuwa kinyume na taratibu. Hata hivyo
CCM waling’ang’ania kuendelea.
Halima Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe lilipo kwenye
Halmashauri ya Kinondoni ambaye pia ni mjumbe katika Baraza la Halmshauri hiyo
amesema kuwa, kilichofanyika katika uchaguzi huo ni ukiukwaji wa sheria.
Mdee amesema kuwa, wajumbe halali wamezuiwa kupiga
kura akiwataja kuwa ni Suzani Limo na Salma Mwasa.
Na kwamba, wajumbe wasio halali akiwemo Prof. Joyce
Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi wamejumuishwa.
Amesema, Prof. Ndalichako sio Mkazi wa Kinondoni
aliyewahi kushiriki uchaguzi wa Meya wa Ilala pia Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika
sio mjumbe halali katika manispaa hiyo.
“Hata hivyo, sheria inaeleza wazi kuwa katika
halmshauri moja ni lazima kuwepo na wateuzi wa rais wasiozidi watatu ambapo
katika manspaa hii wapo wanne,”amesema Mdee.
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa amesema
kuwa, awamu hii ya utawala imetupa mazingatio ya sheria na kwamba,
demokrasia ipo gizani.
Mbowe amelituhumu Jeshi la Polisi kuwa wakala wa
Serikali ya CCM, kutokana na utekelezaji wa majukumu yao kwa upande wa siasa na
kwamba chama hicho kina kila sababu ya kuendeleza operesheni ya Umoja
wa Kupinga Udikitekta (Ukuta).
Hata hivyo, ameeleza jinsi uhuru wa vyombo vya
habari unavyoanza kuminywa kutokana na kutozuiliwa kwa vyombo vya habari vya
wananchi kuripoti tukio hilo.
“Magazeti ya Mwananchi, Mtanzania, Tanzania Daima na
MwanaHALISI hayakuruhusiwa kushuhudia mwenendo wa uchaguzi, inaonesha wazi kuwa
wanajua kuwa watafanya dhuluma,”amesema.
Amesema kuwa, vyombo vya habari vilivyoruhusiwa ni
Telvisheni ya Taifa (TBC1) Daily News, Habari Leo vinayomilikiwa na serikali na
Gazeti la Uhuru linalomilikiwa na CCM.
Hata hivyo Dk. Mashinji amesema kuwa, Jeshi la
Polisi linatumika kusaidia Serikali ya CCM kupora haki na kuwa, idadi ya polisi
leo ilikuwa kubwa kuliko wajumbe wa manispaa hiyo ambao ndio wapiga kura.
Dk. Mashinji amesema kuwa, chama hicho kitaaenda
mahakamani kesho kufungua kesi kupinga uchaguzi huo.
Hali ilivyokuwa
Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye ofisi za
manispaa hiyo mapema asubuhi na kushuhudia Jeshi la Polisi likiendelea
kuimarisha ulinzi.
Upande wa kutokea Kituo cha Mabasi cha Magomeni
Hospitali, kulifurika wananchi waliokuwa wanasuburi matokeo ya uchaguzi
huo huku wakiwekewa uzio.