RAIS WA COLOMBIA ATWAA TUZO YA NOBEL,SOMA HAPO KUJUA
JUAN Manuel Santos, rais wa Colombia ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel
kwa mwaka 2016 baada ya kufanikiwa kuingia makubaliano ya amani na
waasi wa Farc nchini humo na kusitisha vita vilivyodumu kwa karibu miaka
hamsini, anaandika Charles William.
Wakati Rais Santos akishinda tuzo hiyo kufuatia mkataba wa amani wa kihistoria Colombia, tayari mkataba huo wa kusitisha vita na waasi umeshavunjika.
Rais Santos aliingia mkataba wa amani na kiongozi wa waasi hao
Rodrigo Londono ‘Timochenko’ mjini Cartagena tarehe 27 Septemba, mwaka
huu na alinukuliwa akisema, “Colombia inasherehekea, ulimwengu
unasherehekea, kwa sasa kuna vita vimemalizika duniani.”
Ingawa mkataba huo ulikutana na ukosoaji mkubwa, wakosoaji wadai kuwa
mkataba huo wa amani unawanufaisha waasi wa Farc na kuwapa fursa ya
kukwepa kuwajibishwa na vyombo vya sheria kutokana na makosa ya uhakifu
wa kivita waliyofanya.
Hata hivyo Rais Santos alinukuliwa akisema kuwa hayo ndiyo mapatano bora zaidi yanayoweza kufanywa kwa niaba ya Colombia.
Watu zaidi ya 260,000 waliuawa, kwenye vita hivyo na wengine milioni
sita kuachwa bila makazi kutokana na uharibifu wa miundombinu na makazi.
Siku tano tu tangu kuingiwa kwa makubaliano hayo ya amani katika
taifa hilo na kulifanya kundi la waasi la Farc kuweka silaha chini,
wananchi walipiga kura ya ya maoni na kuyakataa mnamo Oktoba 2.
Baadhi ya wanachama wa Farc, pamoja na maafisa wa kijeshi na polisi
walipangiwa kufikishwa mbele ya mahakama maalumu kujibu mashtaka kwa
makosa ambayo wametekeleza katika vita nchini humo chini ya mkataba huo.
Kundi la Farc, ambalo lilianza kama wanamgambo wa Chama cha
Kikomunisti mwaka 1964, linatarajiwa kuacha vita na kuingia katika siasa
za amani.