RAIS MAGUFULI AANZA KUGONGA "MWAMBA",AHADI YA MIKOPO KWA WANAFUNZI YAANZA KUFIFIA,SOMA HAPO KUJUA
RAIS John Magufuli amekiri ‘kugonga mwamba’ kwa
ahadi ya serikali yake kwamba, hakuna mwanafunzi wa Chuo Kikuu
atakayecheleweshewa mkopo na kama ikitokea hivyo, mtumishi wa serikali
aliyehusika na suala hilo atapoteza kazi, anaandika Pendo Omary.
Magufuli alikuwa akizungumza
katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alipoenda kwa ajili ya
kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa majengo 20 ya mabweni ambayo yatakuwa na
uwezo wa kubeba wanafunzi 3,846.
Rais Magufuli, Oktoba mwaka jana alipokuwa
akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Jimbo la Tabora Mjini
mkoani Tabora alisema; “Huwezi kumtoa mwanafunzi Kaliua (Tabora), kwenda
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, awe amefaulu kwa daraja la kwanza au la pili
halafu afike pale chuoni fedha zake hujamuingizia wakati bodi imeshamteua
kwenda masomoni.
Kama umemteua kwenda Chuo Kikuu, hukujua kuwa
anatakiwa kupata mkopo? Serikali ya Magufuli, ukimcheleweshea mkopo mwanafunzi
ujue kazi huna,” alisema na kushangiliwa.
Rais Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa leo UDSM
ameishia kulalamika kuwa mawasiliano mabovu kati ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU),
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu (HESLB) na Wizara ya Elimu ndiyo yamesababisha
wanafunzi kutopewa fedha za mikopo mpaka sasa.
“Hakukuwa na Coordination (uratibu), tangu mwanzo
ilitakiwa vyuo vikuu vyote ya Elimu ya juu viwe na tarehe moja ya kufungua.
Unafungua chuo haraka halafu unataka wanafunzi wafanye usajili wakati bodi ya
mikopo haijalipa,” amesema Magufuli.
Kinyume na ahadi yake kwamba ucheleweshaji wa mikopo
ukitokea, atawafukuza kazi watumishi waliohusika, leo Rais Magufuli ‘amegwaya’
kutangaza kumchukulia hatua mtumishi yoyote aliyehusika na uzembe huo wala
kueleza hatua zozote atakazochukua kutokana na ucheleweshaji huo wa mikopo.
Itakumbukwa kuwa, mpaka sasa ni wiki mbili tangu
wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa UDSM, waanze kuripoti chuoni hapo lakini
serikali imeshindwa kuidhinisha malipo ya fedha zao za kujikimu huku wanafunzi
hao pia wakigomea kusaini fedha ya kujikimu iliyo pungufu, tofauti na
utaratibu.
Pia ni siku sita sasa tangu wanafunzi wa mwaka wa
Pili, Tatu na mwaka wa Nne waanze kuripoti chuoni hapo lakini serikali
imeshindwa kuwapatia fedha zao za kujikimu, jambo linalowapa wakati mgumu
kujikimu kwa chakula na malazi.
Rais Magufuli amesema tayari Wizara ya Fedha imetoa
Sh. 80 bilioni za awali kwa ajili ya kulipia mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu
huku akisema serikali haitatoa fedha kwa wasiostahili kupata mikopo