PROFESA LIPUMBA AANZA KURUSHA MADONGO KWA WAPINZANI WENZAKE,SOMA HAPO KUJUA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba, amewataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kutoingilia mgogoro uliopo ndani ya chama hicho kwa sababu hauwahusu.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam
alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho katika kikao cha ndani,
kilichofanyika Wilaya ya Kinondoni ambapo alisema Chadema kushindwa kutekeleza
Operesheni Ukuta ni dhahiri chama hicho kimeshindwa kutekeleza kile wanachoahidi
kwa Watanzania.
Alisema mpaka sasa kumekua na vikao mbalimbali
vinavyofanywa na viongozi wa Chadema kwa ajili ya kuivuruga CUF, jambo ambalo
alisema haliwekezani.
“Chadema wanajitahidi kutuvuruga kwa
kutuma waasi wa chama hiki, lakini naomba niwaambie hawawezi, CUF ni ngangari
hata serikali inajua na wanachokifanya ni kupoteza muda bure.
“Unajenga Ukuta wa biskuti, ukiumwagia
juisi unamong’onyoka, Ukuta gani huo, huu muziki wa CUF ni ngangari hawauwezi,”
alisema Lipumba.
Alisema katika kipindi hiki ambacho wana kesi
mahakamani, wanachama wa chama hicho wataendelea na shughuli za kukijenga chama
hicho pamoja na kuwasisitiza kuwa na msimamo wa kutetea chama na katiba
yake, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kufikia malengo waliyokusudia ya kushika
dola kafika Uchaguzi wa mwaka 2020.
Alisema kutokana na hali hiyo, rasilimali za chama
hicho zinasimamiwa kwa umakini chini ya walinzi wa chama hicho, Blue Guard
ambao Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad alisema ni wavamizi
hawatambui.
“Ninamshangaa Maalim Seif sasa hivi
anaibuka na kusema hawatambui walinzi wa chama Blue Guard ambao miaka yote
walikua wanamlinda pamoja na rasilimali za chama, lakini hayo yamekwisha
nitazidi kumwomba aje tujenge chama hata kama kesi inaendelea mahakamani,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano
anayemunga mkono Profesa Lipumba, Abdallah Kambaya alisema kupoteza nafasi ya
umeya na naibu wake katika Manispaa ya Kinondoni ni matokeo ya mgogoro wa CUF
na kutokuwepo ushirikiano ndani ya Ukawa.
“Maalim Seif anaunga mkono Ukawa, mbona
wanachama wa Ukawa wameshindwa kutusaidia ili kupata meya na naibu wake kwenye
uchaguzi wa leo? (jana),” alihoji.