NSSF IMEKUFA KWA UFISADI,BILIONI 270 ZAPOTEA KAMA HAZINA MWENYEWE,SOMA HAPO KUJUA
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekiri
kuwapo ubadhirifu kwenye mkataba wa ubia na Kampuni ya Azimio Housing Estates
iliyotakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi Kigamboni na kuna hatari ya
kupoteza Sh bilioni 270.
NSSF pia imekiri ubadhirifu katika utoaji mikopo
kwenye Saccos mbalimbali nchini ikiwamo ya Bumbuli, inayoonekana kukopeshwa
zaidi ya Sh bilioni mbili, bila kuwa na sifa huku kukiwa pia hakuna kumbukumbu
ya mwaka mzima kama walirudisha mkopo wa awali.
Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe
alieleza jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba Bodi
yake ilipoingia madarakani iligundua ubovu wa mkataba huo na kusitisha kutoa
fedha na sasa inaangalia namna ya kujitoa bila kupoteza fedha zilizowekezwa.
Alisema uwekezaji huo ambao ardhi ya mwekezaji
ilipaswa kuwa ekari 20,000, hatua ya awali ulipaswa kuanza na ekari 300, lakini
uchunguzi uliofanyika hivi karibuni ulionesha kuwa kuna ekari 3,500 pekee hali
inayoonesha udanganyifu uliofanyika tangu awali.
Pia mwekezaji huyo alidanganya uhalisia wa bei ya
ardhi hiyo, kwani alionesha kuwa thamani ya ekari ya moja ni Sh milioni 800
wakati kiuhalisia, ardhi hiyo thamani yake ni Sh milioni 25 peke yake.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema
imekuwa vigumu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
kuthibitisha uwepo wa viwanja hivyo kwa kukosekana hatimiliki, umiliki wa ekari
19,700 za ardhi ambazo ni sehemu ya mtaji wa Azimio Housing Estates kwa
asilimia 20, hivyo fedha za NSSF zinakuwa kwenye hatari ya kupotea.
Alisema NSSF ambayo inamiliki hisa ndogo kuliko
Azimio, imewekeza fedha nyingi, zaidi ya dola milioni 129 za Marekani wakati
mbia huyo aliwekeza dola milioni 5.5.
Akijibu hoja za Mwenyekiti huyo, Profesa Wangwe
alisema mradi huo ulisimama tangu Februari kutokana na mbia kukosa
fedha na kwamba hakopesheki kwani NSSF inamdai.
Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige alisema mradi huo
wa Kigamboni ni mchafu na katika mazingira hayo ambayo Bodi pia imeshituka
kuwa mchafu hivyo ni vema NSSF ingejitoa kuliko kuendelea na
mkataba mbovu.
“Ni vema ukishagundua kuwa unachezea
kitenesi kichafu ambacho kilianza kuchezewa na watu ambao wameshaondolewa,
usiendelee kucheza na mtu yule yule ili asije kukuingiza katika matatizo
makubwa zaidi,” alisema Maige.
Profesa Wangwe alisema ni vigumu kujitoa haraka
kwenye mkataba huo, kutokana na fedha nyingi waliyowekeza ambayo iko hatarini
kupotea na kwamba ardhi yote ni ya mwekezaji huyo hivyo wanatafuta namna ya
kurudisha fedha waliyowekeza hata kama haitakuwa na faida.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh Hilaly alihoji kama
mkataba unaruhusu mwekezaji huyo kukopa ili kuendeleza mradi huo.
Mkurugenzi wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema
mwekezaji huyo alitaka kukopa NSSF ili aendeleze mradi huo ambao umesimama
lakini hakopesheki kwa kuwa anadaiwa.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa
Saccos kukopeshwa mara mbili kwa mwaka, huku zingine zikikosa mikopo na vigezo
vilivyotukia katika kutoa mikopo hiyo.
Kuhusu Saccos ya Bumbuli, Kaboyoka alisema mbunge
wake anafahamika, hivyo inashangaza ipewe fedha hizo kwa mwaka mmoja na kuhoji
sifa zilizotumika kuzitoa wakati Saccoss zingine hazijapata.
Alisema ni vema ufanyike ukaguzi maalumu kwenye
Saccos hiyo kwani fedha hizo ni mafao ya wafanyakazi ingawa pia inatia shaka
katika utoaji, kwani awali Saccos hiyo ilipewa zaidi ya Sh bilioni moja na
kwamba hesabu hazioneshi, kwamba fedha hizo zilirejeshwa, lakini ndani ya mwaka
mmoja ikapewa fedha zingine.
NSSF ilitoa mikopo kwa Saccos tisa kwa kiasi
kinachozidi asilimia 50 ya thamani ya mali za Saccos husika, kinyume na sera ya
Shirika ya kukopesha na ziliomba kiasi ambacho hazikustahili.
Katika ripoti ya CAG mbali na Bumbuli, Saccos
zingine zilizopewa fedha nyingi ni Korongo Amcos, UMMA, SBC, Hekima, Ukombozi,
Uzinza, Harbour na Umoja.
Akijibu hoja hizo, Profesa Wangwe alisema Saccos zilizopewa
fedha zaidi ya mara mbili kwa mwaka ikiwamo ya Bumbuli iliyopewa Sh bilioni
2.473 kwa mwaka 2014/15, wakati anaingia kwenye nafasi hiyo, aliliona hilo kama
tatizo hivyo kuagiza kufanyike ukaguzi maalumu.
Alisema waliokuwa wanasimamia Saccos hizo
walisimamiswa kazi tangu Bodi mpya ilipoingia na kwamba walisitisha kutoa
mikopo ya aina yoyote katika Saccos zote nchini, hadi uongozi wa Shirika
utakapoanzisha utaratibu mpya.
“Watu wote waliohusika na ubadhirifu wameshaondolewa
ofisini, tulishituka kuona namna fedha hizo zilivyotolewa, si zote zilizofika
kwa wahusika, zingine ziliishia kwenye mikono ya watu, tuliona ni vema ufanyike
ukaguzi maalumu,” alisema Profesa Wangwe.