MAMA RWAKATARE AZIDISHA UPENDO KWA WAFUNGWA,SOMA HAPO KUJUA
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of
God (Mlima wa Moto), Getrude Rwakatare amesema ataendelea na mpango wake wa
kuwanusuru wafungwa wanaotumikia adhabu magerezani kwa kuwalipia faini ili
warejee uraiani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es
Salaam, alisema katika awamu ya pili ameamua kuwalipia wafungwa 43 waliopo
katika magereza ya Mkoa wa Dodoma.
“Kampeni hii ya kuwalipia faini kati ya
Sh 50,000 hadi 200,000 wafungwa waliopo magerezani imetupa moyo na Watanzania
wengi wameguswa na hata kutupongeza. Kutokana na hali hii kanisa letu sasa
limefanya hivyo tena na safari hii tunaelekea mkoani Dodoma,”
alisema.
Mchungaji Rwakatare alisema kesho watawatoa wafungwa
hao mkoani Dodoma ambapo vigezo walivyoangalia ni wanawake wanaonyonyesha,
wagonjwa na wazee.
“Nasi tunatimiza maandiko ya Mungu
katika kufanya hivi na kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa Parole, Augustino
Mrema,” alisema Mchungaji Rwakatare.
Alisema kutokana na makosa mbalimbali ya faini
waliohukumiwa nayo wafungwa hayo, kanisa lao limetoa Sh milioni 6.8 kwa ajili
ya kulipia faini hizo.
Awali Rwakatare kupitia kanisa lake, aliwalipia
wafungwa 78 katika magereza matatu ya Keko, Segerea na Ukonga ya jijini
Dar es Salaam na kuachiwa huru baada ya kulipa faini ya Sh milioni 25
zilizochangwa na waumini wa kanisa hilo.