MAJAMBAZI YA MBAGALA YAULIWA,SOMA HAPO KUJUA
Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia
Silaha cha Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kilifanikiwa kukamata
watuhumiwa wanne wa ujambazi waliohusika katika mauaji ya askari polisi 4
katika benki ya CRDB iliyopo maeneo ya Mbande, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro wakati
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema watuhumiwa
hao walikamatwa wakati wa majibizano ya risasi yaliyotokea Oktoba 11, 2016
katika pori la Dondwe lililopo Chanika.
“Kikosi kilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa
mmoja, baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa ni jambazi na ndiye
aliyehusika katika mauaji ya askari polisi huko Mbande,” amesema.
Kamanda Sirro ameongeza kuwa “Baada ya kumkamata
mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo akiwa na wenzie saba, alitupeleka
mahala walipo wenzake, ila alikimbia, wenzie walipojua polisi wapo maeneo hayo,
walianza kurusha risasi ndipo polisi nao wakaanza kurusha risasi.”
Kamanda Sirro amesema kuwa, watuhumiwa hao
walizidiwa na mashambulizi ya risasi ambapo walijeruhiwa vibaya na kwamba
walifariki dunia wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Amesema askari polisi walifanikiwa kuipata bunduki
ya kijeshi aina ya SMG iliyofutwa usajili ambayo watuhumiwa hao waliipora
kutoka mikononi mwa polisi waliowaua mbande ikiwa na risasi 22 ndani ya
magazine.
Katika tukio lingine, Kamanda Sirro amesema mnamo Oktoba
11, 2016 maeneo ya magomeni polisi wakiwa doria walifanikiwa kukamata bastola
moja aina ya bereta baada ya kutelekezwa na kundi la vijana.
Pia amesema Jeshi la Polisi limekamata watuhumiwa
watatu wakiwa na bomu moja la kienyeji, mapanga manne, visu viwili, na bisibisi
moja.
Vilevile Jeshi la Polisi Dar es Salaam Oktoba 12,
2016 walikamata panya road zaidi ya 10 maeneo ya Mbagala.