MAALIM SEIF AMJIBU PROFESA LIPUMBA,ADAI KUWA CUF IPO VIZURI,SOMA HAPO KUJUA
Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye
amekuwa kimya kuzungumzia sakata linaloendelea ndani ya chama hicho
likimuhusisha Profesa Ibrahim Lipumba, jana aliondoa ukimya na kueleza kuwa
kinachoendelea ni mpango ulioandaliwa wa kuvuruga jitihada za chama hicho za
kudai haki, lakini hautafanikiwa.
Pamoja na hayo, Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), amesema kuna jitihada alizoziita za mwendokasi za jumuiya ya kimataifa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Maalim Seif alisema hayo jana wakati akitoa salamu
zake fupi kwa mamia ya waumini na wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika
Msikiti wa Kihinani, Wilaya ya Magharibi A.
CUF iko kwenye mvutano wa uongozi kutokana na
Profesa Lipumba kushika ofisi kuu za chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar
es Salaam akisema kuwa ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho baada ya Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini kutoa msimamo na maoni ya ofisi yake kuhusu sakata
hilo.
Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti
mwaka jana, akipinga chama hicho kuendelea kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) baada ya vyama vinne vinavyounda umoja huo kumpitisha Edward
Lowassa kuwa mgombea wao wa urais.
Hata hivyo, Juni mwaka huu Profesa Lipumba
alimuandikia barua katibu mkuu akitaka atengue barua yake ya kujiuzulu, lakini
Mkutano Mkuu wa chama hicho ulijadili suala hilo na kuazimia kukubaliana na
kujiuzulu na baadaye Baraza Kuu kupitisha uamuzi wa kumvua uanachama.
Lakini Maalim Seif, ambaye aligombea urais wa
Zanzibar katika uchaguzi ambao matokeo yake yalifutwa mwaka jana, anauchukulia
mgogoro huo kuwa ni njama za kuwaondoa kwenye mikakati yao ya kudai haki.
“Nasema hiyo ya Profesa Lipumba ni
ajenda iliyolenga kutuparaganya ili tuondoke katika mazingira na hima ya
kutetea haki yetu iliyoporwa. Lakini msijali hiyo haitafanikiwa nasi tumefikia
pazuri sasa,” alisema.
Katika hadhira hiyo, Maalim Seif alilaumu juhudi
alizoziita za baadhi ya watu kutumia vibaya mamlaka kutaka kumzuia asiongee na
wananchi licha ya kuwa umma unayo shauku kubwa ya kuhitaji kumsikiliza kila
anapopita.
“Najua zipo kila mbinu na hila za
kutaka mimi nisiongee nanyi. Wenyewe mmeshuhudia hapa msikitini baada ya
kubainika nakuja, lakini nasema mimi ni binadamu na kiongozi, ninayo haki ya
kuongea na yeyote popote.Nitaongea na nitaongea popote pale,” alisema.
Mkwamo wa kisiasa
Alisema zipo juhudi za ‘mwendo kasi’ kuelekea
ufumbuzi wa mkwamo wa kisiasa Zanzibar kupitia meza ya jumuiya ya kimataifa.
“Wapi lilipofikia suala hili ambalo
naweza kuliita mwendo kasi? Nasema limefikia pazuri mno, tulieni wala msiwe na
shaka, tumefikia hatua ya matumaini makubwa,” alisema Maalim,
mmoja wa wanasiasa wenye nguvu visiwani Zanzibar.
Maalim Seif pia alizungumzia suala la Katiba mpya,
akisema kumekuwapo na juhudi za chini kwa chini za kutaka kupiku ridhaa ya
wananchi kwa kuipitisha Katiba Inayopendekezwa kwa lazima.
Mswada wa mafuta
Akizungumzia muswada wa mafuta na gesi uliopitishwa
hivi karibuni na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Maalim Seif alisema hicho ni
kiini macho kwa kuwa hakuna mabadiliko yoyote hadi sasa juu ya sheria hiyo
ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wabunge wazuiwa Mtwara
Katika hatua nyingine, wafuasi wa CUF wakiongozwa na
mbunge wa Tandahimba, Katani Katani jana walizuiwa na polisi kuendelea na
mkutano wa ndani kwa kile kilichodaiwa ni kuwapo kwa dalili za vurugu.
Wafuasi hao ni wale wanaompinga Profesa Lipumba
ambaye anatambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini.
Tukio hilo lilitokea jana wilayani Newala wakati
wafuasi hao wakiendelea na ziara yao katika wilaya mbalimbali kanda ya kusini.
Katani ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi
lililomvua Lipumba uanachama, alisema amesikitishwa na kitendo cha askari
kuwaruhusu kufanya mkutano na saa moja baadaye kwenda kuwatawanya bila
kuwaambia sababu za msingi.
Alisema kuwa baadhi ya viongozi wa wilaya ya Newala
wanaomuunga mkono Profesa Lipumba walikwenda polisi na kufanya mbinu mkutano
huo usiendelee.
“Newala kuna figisufigisu, tulitoa
taarifa za kikao cha ndani polisi na waliridhia, lakini viongozi wa wilaya
wakaenda polisi kwa kushtukiza kusema kikao kisiendelee kwa hiyo
tukafanya kikao cha ndani, lakini ghafla walituvamia wakiwa na
bunduki na mabomu ya machozi na kututawanya,” alisema Katani.
Mbunge huyo alidai kuwa kutokana na tukio hilo,
wanaamini tamko la kuruhusiwa kufanyika mikutano ya ndani lililenga kumpa
nafasi Profesa Lipumba na wanatarajia kutoa tamko leo kwa kuwa walipotaka
kufanya kikao walikosa ulinzi wa polisi.
“Hii imesababisha kuamini kwamba Profesa
Lipumba anatumika, maana inaonyesha wazi juzi alipokuwa Newala aliruhusiwa
kufanya mkutano akiwa na ulinzi wa polisi, lakini leo (jana) sisi katika ukumbi
ule ule mimi nikiwa kama mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi na mbunge wa
kuchaguliwa na wananchi polisi wameshindwa kutoa ulinzi,”
alisema Katani
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, wa Mtwara, Thobias
Sedoyeka alisema walilazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na kuwapo wa dalili
za vurugu kutoka pande mbili, unaomuunga mkono Maalim Seif na mwingine Profesa
Lipumba.
“Pande mbili zina mgogoro kwa hiyo
kulikuwa na mvutano pande zote mbili za Maalim na Profesa. Mimi nimeona kuna
dalili ya vurugu na vurugu zingekuwapo hata wao wangefanya nini,”
alisema Sedoyeka.
Katani pia alizungumzia taarifa zinazoenea kwenye mitandao za kukamatwa kwa wabunge wa kusini.
Katani pia alizungumzia taarifa zinazoenea kwenye mitandao za kukamatwa kwa wabunge wa kusini.
“Ni kweli tulikuwa Nachingwea tukitokea
Ruangwa wakati tukisubiri kupata chakula tukawa tunapata kahawa na wananchi
waliokuwapo pale tukawa tunabadilishana, mawazo lakini kuna watu walitoa
taarifa polisi kuwa tunafanya mkutano wa hadhara na polisi walipokuja
tulikwenda kituoni na kufanya majadiliano na walijiridhisha kuwa kile
walichoambiwa hakikuwa sahihi,” alisema.
Hivi karibuni, Profesa Lipumba akiongozana na Mbunge
wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma alifanya ziara mkoani Mtwara na kukutana na wafuasi
wake katika Wilaya ya Mtwara na Newala akisema lengo la ziara hiyo ni
kuimarisha chama