GAVANA WA BENKI KUU APINGWA VIBAYA,ZITTO KABWE AMJIA JUU,NI KUHUSU UCHUMI KUKUA,SOMA KUJUA
Na TOBIAS NSUNGWE-DAR ES SALAAM
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe
amehoji taarifa ya Benki Kuu (BoT) kuhusu kile ilichodai kuongezeka kwa kasi ya
ulipaji wa deni la taifa pasipo kueleza kasi ya ukopaji wake.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana Zitto ambaye
ni mchumi kitaaluma na Mbunge wa Kigoma Mjini alidai hakuna haja ya kushangilia
kuhusu kasi ya ulipaji wa deni hilo kwani taarifa zinaonesha hadi Juni mwaka
huu deni la ndani lilikuwa limeongezeka kwa asilimia 35 ndani ya mwaka mmoja
hadi kufikia Sh. trilioni 10.7.
Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu, juzi alitoa Ripoti
juu ya hali ya uchumi katika kipindi cha nusu mwaka ambapo pamoja na mambo
mengine alieleza kuongezeka kwa kasi ya ulipaji wa deni la taifa lakini
hakueleza kiasi ambacho serikali imekopa kwa kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Zitto inawezekana Gavana alikua
akificha kitu.
“Taarifa ya BoT (Monthly Economic Review) ya mwezi
Julai ndiyo iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu hadi sasa inaonyesha kuwa deni
la taifa linaongezeka hadi kufikia USD 16 bilioni mwezi Juni, (mwisho wa ripoti
ya pili ya mwaka 2016) kati ya mwezi Mei na Juni deni liliongezeka kwa USD 74
milioni, Nyongeza ya mwaka mzima ya 2015 hadi Juni mwaka huu ni USD 890 (2
trilioni ) sasa Gavana anaposema kuwa serikali imelipa halafu hasemi deni
lililoongezeka ndani ya mwaka mmoja ana maana gani?” alihoji Zitto
Zitto anasema kulipa zaidi kwa kukopa zaidi sio
jambo la kujivunia.
“Deni la ndani liliongezeka kwa asilimia 35 ndani ya
mwaka mmoja hadi 10.7 trilioni mwisho wa Juni mwaka huu sasa hii ya kulipa madeni
kwa kukopa zaidi ndio jambo la kusheherekea? Kwanini madeni yaongezeke wakati
mapato ya TRA yameongezeka? Huoni changa la macho hapo?” alihoji.
Katika ripoti iliyotolewa juzi na Ndulu, imeeleza
kuwa Rais John Magufuli amelipa Sh. bilioni 99 za deni la ndani na pia amelipa
dola za Marekani milioni 90 za deni la nje katika muda wa siku 90.
Rekodi hiyo mpya ya ulipaji madeni inadaiwa
haijawahi kufikiwa na Serikali ya awamu ya nne katika kipindi chote cha miaka
10.
Msomi na mtaalamu wa mambo ya kodi kutoka Wizara ya
Nishati na Madini, Profesa Hadley Mafwenga, alisema nidhamu katika ulipaji wa
deni ni muhimu ili kuipa thamani miradi inayoendeshwa na fedha za mikopo ambayo
Serikali ilichukua huko nyuma.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Profesa
Mafwenga alisema ulipaji wa deni la taifa ni muhimu kama nchi inataka kuweka
mazingira ya kuweza kukopesheka siku zijazo na kupunguza athari (risk)
zinazotokana na kuchelewa kulipa madeni hayo.
Kwa mujibu wa Profesa huyo kadiri nchi
inavyochelewesha deni, riba inaongezeka hivyo ni busara kulilipa mapema.
Kwa mujibu wa BoT hadi sasa deni la taifa linafikia
Sh trilioni 51.
Pamoja na hayo, Profesa Mafwega alisema wale
wanaofananisha ulipaji wa deni la taifa kati ya Magufuli na Serikali ya Kikwete
wana mtazamo wa kisiasa zaidi kwani deni liko ‘linked’ na nchi si rais aliyeko
madarakani.
Profesa Mafwenga katika maelezo yake alisisitiza
kwamba hakuwa ameisoma kwa kina ripoti ya profesa Ndulu na kuahidi kuchambua
zaidi pindi atakapoisoma.
Profesa huyo alizungungumzia pia hali ya kukua kwa
uchumi nchini akisema inatokana na kukua kwa wigo wa uzalishaji.
Alieleza kwamba, pia hali ya mfumuko wa bei
inaendelea kushuka na kuzidi kuifanya shilingi yetu kuimarika.
Gavana Ndulu alisema mwenendo wa ukuaji uchumi kwa
nusu mwaka kuanzia Januari hadi Juni 2016, umeongezeka hadi kufikia asilimia
6.7 ikilinganishwa na asilimia 5.7 katika kipindi hicho hicho mwaka 2015.
Profesa Ndulu alizitaja sekta zinazochangia ukuaji
wa uchumi kuwa ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo, uchimbaji madini na gesi,
mawasiliano na sekta ya fedha.
Wachumi wengi wamekuwa wakiitaka Serikali iongeze
kasi ya ulipaji wa deni la taifa ili kuwapunguzia wananchi mzigo na kuiwezesha
nchi kukopesheka tena.