Zinazobamba

WAKULIMA WAMUANGIKIA RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA

Wakulima wakiwa shambani

WAKULIMA na wafugaji kutoka Kijiji cha Wami, Luhindo wilayani Mvomero, Morogoro wamemwomba Rais John Magufuli kuwasaidia wasiporwe ardhi yao, anaandika Christina Haule.
Na kwamba, wameungana kwa pamoja kupinga ardhi yao yenye ukubwa wa hekari 3,500 kupewa mwekezaji bila ya uongozi wa Serikali ya Kijiji kushirikishwa. 
Wakizungumza na waandishi wa habari leo wamesema, wameingia wasiwasi kutokana na kuonekana kwa watu wanaodhaniwa kuwa wataalamu wa ardhi kutoka Ofisi ya Wilaya ya Mvomero ambao walikuwa wakipima maeneo hayo na kupachika bikoni.
Na kuwa, walipoulizwa na uongozi wa kijiji waliwaeleza kuwa, eneo hilo linaandaliwa kukabidhiwa mwekezaji.
Aidha wananchi hao walihoji sababu ya wataalam hao wa ardhi kupima na kuweka alama katika ardhi hiyo ambayo ilikwishapimwa na kutengewa matumizi kwa ajili ya wananchi hao bila kuwashirikisha wananchi wenyewe na hata viongozi wao wa vijiji?
Wananchi hao wamemwomba Rais Magufuli kusikiliza kilio chao na kwamba, kama wataporwa mashamba hayo, ‘Hapa Kazi Tu’ wataitekelezaje?
Apolinary Kahumba, Mwenyekiti wa Kijiji cha Wami Luhindo ameeleza kushangazwa na hatua ya kuweka bikoni bila kushirikisha uongozi wa kijiji.

Amesema, wameweka bikoni kwenye mashamba mengine ambayo serikali ya kijiji iliyatoa ili watu wajiendeleze.
Amesema, hali hiyo inawapa wakati mgumu viongozi wa kijiji na kubaki wakijiuliza kama kuwepo kwa ardhi hiyo kunatambulika kwa mujibu wa  sheria au waambiwe kama sheria iliyopo haifuatwi au kuna sheria mpya ya mwaka 2016 inayowaruhusu watu kupima tena ardhi iliyokwishapimwa.
Akizungumza kijijini hapo, Anglus Mbilinyi aliyeishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 30 amesema, serikali iliwakabidhi maeneo hayo na kuwapatia nakala ya barua iliyokuwa na kumbukumbu namba C.60/3/80 yenye kichwa cha barua ‘Ugawaji wa maeneo ya kilimo kwa wakazi wa mji wa Morogoro 1999/2000.’
Amesema, kilio chao kikubwa leo hii ni kuwekewa bikoni katika mashamba yao ambapo wananchi wote wanakaa kwa uhakika na uthibitisho wa barua walizopewa na serikali tangu zamani.
Okasa Ndakala ambaye ni mfugaji amesema, wamekaa maeneo hayo kwà miaka mingi na kufanya shughuli zote muhimu wakishirikiana na serikali lakini wanashangazwa kuona eneo hilo hawana mamlaka nalo.