MAALIM SEIF AMUONYESHA MAGUFULI JEURI YAKE,NI KUHUSU MATIBABU YAKE,SOMA HAPO KUJUA
ANAJIWEZA. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Maalim Seif Shariff
Hamad, kwenda matibabuni nje ya nchi bila kutumia mfuko wa serikali, anaandika Faki Sosi.
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) yupo nchini India kuangalia afya yake. Safari hii haijagharamiwa na mfuko wa serikali kama inavyostahili.
Hatua hiyo inatafsirika kama jibu kwa Rais John Magufuli, Rais wa
Tanzania kutokana na kauli yake aliyoitoa alipokua ziarani visiwani
Unguja siku za hivi karibuni.
Kwenye ziara hiyo bila kumtaja jina Maalim Seif, Rais Magufuli
alimshangaa Dk. Ali Mohammed Shein kusaini fedha za matibabu kwa mtu
ambaye aligoma kumpa mkono na kwamba, kama angekuwa yeye (Rais Magufuli)
asingefanya hivyo.
Aliyegoma kumpa mkono Dk. Shein ni Maalim Seif walipokuwa kwenye msiba wa Alhaj Aboud Jumbe, Rais Mstaafu wa Zanzibar.
Kauli ya Rais Magufuli iliibua mjadala mkubwa ndani ya nchi kutokana
na mazingira halisi ya siasa za uhasama visiwani humo na kuwa,
hakustahili ‘kumwagia petroli’ visiwani humo.
Taarifa visiwani humo zinaeleza kuwa, Maalim Seif amesusa kutumia
fedha za serikali hasa baada ya kauli zinazotajwa kuwa za kejeli kwa
viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika matibabu yake
licha ya matibabu hayo kutambuliwa kisheria.
“Ni kweli hajapata fedha kutoka serikali lakini na mimi pia sijui
fedha kazipata wapi. Ni kweli kwamba yupo nchini India kwa ajili ya
uchunguzi wa kawaida wa afya yake,” amesema Salim Bimani, Mkurugenzi wa
Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF.
Mgogoro na uhasama visiwani Zanzibar unaongezeka kila kukicha
kutokana na baadhi ya viongozi wa serikali kutotilia maanani tofauti
hizo.
Tayari utengano umekuwa ukionekana waziwazi kwa baadhi ya wanachama
na wafuasi wa CUF na wale wa CCM kutoshirikiana katika masuala ya
kibiashara na kijamii.
Mara kadhaa Jeshi la Polisi na CCM visiwani humo limekuwa
likimnyooshea kidole Maalim Seif kwenye kwamba, anachochea uhasama
ambapo tayari amehojiwa kutokana na tuhuma hizo.
Hivi karibuni Maalim Seif alikwenda ughaibuni kueleza namna mazingira
ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar ulivyoghubikwa na uchafuzi kupitia Tume ya
Uchaguzi visiwani humo (ZEC).
Maalim Seif alikwenda Marekani, Ulaya, Canada na Umoja wa Mataifa
kulalamikia uvurugaji wa uchaguzi huo wa 25 Oktoba mwaka jana ambapo
sasa, malalamiko yake yameanza kuzaa matunda.
Tayari taasisi ya kimataifa ya umoja wa wanaliberali – Liberal
International (LI) – imeliandikia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa
Mataifa (UNHRC) kutaka kutolewa kwa vikwazo dhidi ya Serikali ya
Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana kwenye tovuti ya LI, taasisi hiyo
imetaka baraza hilo lenye jukumu la kulinda misingi ya haki za binadamu
kwenye mataifa yote wanachama wa UN, kuchukua hatua kali ili kukomesha
“uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukandamizaji wa haki za kisiasa
na kiraia visiwani Zanzibar.”
Katika tamko walilolitoa na kufikishwa mbele ya Mkutano wa 33 wa
Baraza hilo uliofanyika Septemba mosi mwaka huu, Liberal International
imetaka jumuiya ya kimataifa, kufikiria kuweka vikwazo vya kusafiri na
kuzuia mali za watu wote walioshiriki kuidhinisha vitendo vya utesaji
wanasiasa wa upinzani na wafuasi wao.
Taasisi hiyo ambayo CUF ni mwanachama wa muda mrefu, imetoa wito kwa
wabunge wanaofuata mtizamo wa kiliberali walioko upande wa serikali na
upinzani katika mataifa yote duniani kuchukua msimamo imara kupitia
mabunge ya nchi zao na kutoa matamko ya kupinga walichokiita “uonevu
wanaofanyiwa viongozi wa upinzani Zanzibar na wafuasi wao.”