TUNDU LISSU ATANGAZA VITA MPYA NA JESHI LA POLISI,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kitaliburuza Mahakama Kuu, Jeshi la Polisi kwa kuwatesa na kuwashikilia watu 12
kinyume na utaratibu wa kikatiba na kisheria, anaandika Pendo Omary.
Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu
wa Chadema leo amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, hadi
kufikia Jumanne wiki ijayo, iwapo Jeshi la Polisi halitawapeleka mahakamani
mahabusu wanaoshikiliwa katika vituo vya polisi kwa sababu za kisiasa litapeleka
mashitaka Mahakama Kuu.
“Nimefanya mahojiano na watu 10 wanaoshikiliwa na
kituo cha polisi cha Oysterbay na Kituo Kikuu cha Polisi cha
kati. Mahabusu wa Oysterbay wamezungumza mbele ya mkuu wa kituo hicho
kwamba wameteswa sana. Wakiwa chini ya ulinzi wa polisi wamepigwa sana.
“Huwa wanachukuliwa kutoka mahabusu usiku na
kupelekwa mikocheni kwenye kituo cha mateso. Wanavuliwa nguo na wanapigwa hadi
kuvuja damu. Wanawekwa katika vituo vya polisi zaidi ya wiki mbili bila
kupelekwa mahakamani kwa sababu tu ya tuhuma,” amesema Lissu.
Lissu amewataja watu wanaoshikiliwa katika kituo cha
polisi Oysterbay kuwa ni; Anstotle Mgasi na Hosia Mbuba waliokamatawa Vwawa,
Juma Salum na Suleiman Said waliokamatwa Pemba, Dk. David Nikas aliyekamatwa
Tunduma, Mdude Nyangali aliekamatwa Songea.
Wengine ni Shakira Makame na Ignas Mzenga. Baadhi ya
mahabusu hao walikamatwa mikoani na kusafirishwa mpaka Dar, huku Ben Nzogu na
Musa Sikabwe wakiwa wamehifadhiwa kituo cha kati (Central).
“Kwa kuwa Jeshi la Polisi, linakiuka katiba na
sheria, ikifika Jumanne wiki ijayo halijawapeleka mahakamani watu hawa.
Tutaenda Mahakama Kuu kwa kutumia utaratibu wa ‘Habeas Corpus’ ili jeshi hilo
litaitwa na mahakama kueleza kwa nini linawashikilia watu hao kinyume na
sheria,” amesema Lissu.
Amesema Chama hicho kina taarifa zisizo rasmi kwamba
mpaka sasa nchi nzima wanashikiliwa jumla ya watu 73 kwa kile kilichoitwa,
“kukosoa utawala wa Rais John Magufuli” ikiwemo kusambaza video inayomwenyesha
Lissu akisema Rais Magufuli ni ‘dikteta uchwara’
“Mahakama lazima iwahoji polisi, kwa nini
wanawashikilia na kuwatesa watu bila kuwapeleka mahakamani? Tusipowazungumzia
hawa wasio viongozi basi watanzania wengi wataumizwa,” amesema Lissu.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, Jeshi la Polisi
linatakiwa kumshikilia mtu kama mahabusu kwa muda usiozidi masaa 24 na baada ya
hapo linatakiwa kumfikisha mahakamani.
Kifungu cha 360 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai, kinaruhusu Mahakama Kuu, kutoa amri mtu yeyote ambaye anashikiliwa
kinyume cha sheria kupelekwa mahakamani au kuachiliwa huru.