RAIS MAGUFULI APINGWA KILA KONA,CHAMA CHA CUF CHAMVAA KUHUSU KAULI YAKE,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetoa tamko la kumshangaa
Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa kutaka Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa
tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), atunukiwe tuzo kwa utendaji uliotukuka, anaandika
Pendo Omary.
Chama hicho kimesema kwamba mshangao
uliopo unahusu kitendo cha rais Magufuli kumsifia Jecha ambaye anajulikana
dunia nzima kuwa amevuruga uchaguzi mkuu wa Zanzibar.
“Ni jambo la kushangaza Rais anamsifia hadharani
Jecha kuwa amefanya kazi nzuri asilimia 100 wakati waangalizi wa ndani na nje
wa uchaguzi walijiridhisha kuwa uchaguzi ulikuwa huru, wa haki na uliofanyika
kwa amani,” amesema Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF.
Mtatiro ametoa taarifa hiyo kwenye mkutano wake na
waandishi wa habari uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni,
jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ni majibu ya chama hicho kwa kauli alizotoa
Rais Magufuli katika hotuba zake mbili alipokuwa katika ziara ya kushukuru
wananchi wa Zanzibar. Alifanya mikutano Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba
Ijumaa na Kibandamaiti, mjini Zanzibar jana.
Katika mikutano yake alimsifia Jecha kuwa alifanya kazi
kwa ufanisi na jana alipokuwa uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti, alipendekeza
apewe tuzo na Rais wa Zanzibar.
Mtatiro katika kauli yake amesema kwamba Jecha
alipofuta uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015 alijifanyia tu bila ya kuwa na
mamlaka yoyote ya kisheria ya kufanya hivyo.
Kwa kufuta uchaguzi, katika siku aliyotarajiwa
kutangaza matokeo ya mwisho ya kura za urais, Jecha alivunja sheria na
kusababisha tafrani hivyo kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
kilichoitwa “uchaguzi wa marudio” uliofanyika 20 Machi 2016.
Ni katika uchaguzi huo wa marudio, Jecha alimtangaza
Dk. Ali Mohamed Shein kuwa mshindi, utangazaji uliofanyika siku hiyohiyo ya
uchaguzi. Tofauti na ilivyokuwa Oktoba 2015 ambako kwa siku nne Jecha
alishindwa kutangaza ushindi wa CUF kilichomsimamisha katibu mkuu wake, Maalim
Seif Shariff Hamad.
“Ni jambo lisilokubalika hata kidogo kujisifia
ushindi wa kupora katika uchaguzi kutokana na kupendelewa na Tume ya Uchaguzi
ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema Mtatiro katika tamko
lake.
Mapema kabala ya mkutano wa Mtatiro na waandishi wa
habari kulitokea tafrani kati ya walinzi wa CUF na walioaminika wafuasi wa
Mwenyekiti aliyejiuzulu na baadae kusimamishwa uanachama Prof. Ibrahim Lipumba
waliotaka kulazimisha kuingia ndani ya makao makuu Buguluni.
Soma taarifa kamili…..
.
RIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Imetolewa leo Tarehe 4/9/2016
MWENYEKITI WA CCM, RAIS JOHN MAGUFULI
AACHE KUTUMIA MAMLAKA YAKE VIBAYA AHESHIMU MISINGI YA HAKI,
DEMOKRASIA, KATIBA NA SHERIA ZA NCHI
YETU
Waheshimiwa wanahabari,
Awali napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa
kuitikia wito wetu, nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya
kutupasha habari mbalimbali zinazohusiana na hali ya kisiasa, kiuchumi na
kijamii ndani ya nchi yetu na nje ya mipaka yake. Lakini pia kuwapa pole
kutokana na namna mnavyotekeleza majukumu yenu katika mazingira magumu ya hofu
na vitisho vinavyofanywa na watendaji wa serikali ya awamu ya tano.
Nitumie fursa hii pia kwa kuwa ni mara yangu ya
kwanza rasmi kuzungumza na vyombo vya habari toka BARAZA KUU LA UONGOZI CUF
TAIFA liniamini na kunipa dhamana kubwa ya utendaji na usimamizi wa chama chetu
kwa kuniteua kuwa MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI WA CHAMA CHETU CHA WANANCHI
CUF TAIFA, tukisimamia majukumu yaliyopaswa kufanywa na Mwenyekiti wa Chama
Taifa na Makamu Mwenyekiti Taifa.
Naahidi nitatekeleza wajibu wangu kwa uaminifu
mkubwa na weledi wa hali ya juu kwa madhumuni ya kuwaletea watanzania
mabadiliko sahihi ya maendeleo ya kisiasa na kiuchumi wanayoyataka katika Taifa
letu.
Waheshimiwa wanahabari,
Tumewaiteni na kuomba kuzungumza nanyi kwa lengo la
kujibu kauli zilizotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alizozitoa
juzi na jana (tarehe 2-3/9/2016) katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika
kisiwa cha Pemba, uwanja wa Gombani na Unguja katika uwanja demokrasia
(Kibandamaiti) na kupitia nyinyi tufikishe ujumbe wetu kwa Mwenyekiti wa CCM,
Rais JOHN MAGUFULI na watanzania kwa ujumla.
Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amezungumza
mambo mengi na pia amejikita katika kutoa kauli za dhihaka na mipasho dhidi ya
Chama cha Wananchi CUF na katibu mkuu wetu Maalim Seif Sharif Hamad jambo
ambalo tunaamini kwa hadhi na heshima ya nafasi yake na hadhi ya taasisi ya
urais hakupaswa kufanya hivyo kama kiongozi wa nchi.
Pamoja na masuala mengine Mwenyekiti wa CCM, Rais
JOHN MAGUFULI amesema amekwenda kuwashukuru wananchi wa Unguja na Pemba kwa
kumchagua yeye pamoja na Dokta Ali Mohamed Shein, amewahahakishia Wazanzibari
kuwa atailinda amani ya nchi kwa nguvu zake zote na yeyote atakayejaribu
kuivuruga amani atamshughulikia kwa nguvu zake zote bila huruma, ataulinda
Muungano kwa nguvu zake zote na lazima uendelee kudumu katika kipindi chote cha
utawala wake.
Tatu, amezungumzia maendeleo – Maji, viwanda,
miundombinu, uvuvi na kadhalika lakini pia amezungumzia kuitunza amani akitolea
mifano ya nchi zisizokuwa na amani ikiwemo Libya, Iraq, Syria, Somalia na
mauaji ya kimbali yaliyotokea Rwanda mwaka 1994. Magufuli amepongeza aliyooiita
“kazi nzuri ya majeshi” nadhani kwa kuisaidia kupata ushindi na kuwathibiti
wanaotaka mabadiliko na amempongeza Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC, kwa
kufuta uchaguzi wa tarehe 25/10/2016 uliompa ushindi Maalim Seif Sharif Hamad,
na kumuombea apewe tuzo kwa kazi nzuri aliyoifanya.
Anashangaa kwanini Dokta Shein ameunda serikali kwa
kuvishirikisha vyama vingine wakati alishinda (Shein) kwa asilimia 99 huku
akijigamba kuwa yeye kamwe hawezi kuingiza na hataingiza mtu hata mmoja kutoka
upinzani katika serikali yake pamoja na kupata ushindi wa asilimia 58 anasahau
kuwa hivi karibuni amemteua Mwenyekiti wa TLP Mhe. Agustino Lyatonga Mrema,
kuwa Mwenyekiti wa bodi ya PAROLE.
MSIMAMO WA CUF JUU YA KAULI ALIZOZITOA
RAIS MAGUFULI:
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF CHAMA CHA WANANCHI)
kimesikitishwa na kauli zisizofaa kwa heshima na hadhi ya taasisi ya urais na
nafasi yake kama kiongozi wa nchi kutoka kauli za uchochezi, kupandikiza chuki
na uhasama, kuwagawa wananchi na kutaka kujenga chama chake kwa njia ya vitisho
na kutumia vyombo vya dola. Tunamtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli atambue
kuwa hatoweza kujenga umoja wa watanzania kwa kutoa kauli za kuimarisha chuki,
uhasama na kutosimamia haki, na kuunga mkono vitendo vya uvunjaji wa demokrasia
na sheria za nchi. Rais Magufuli hawezi kuwa mfano wa kuigwa kwa vizazi
vijavyo katika mikakati ya mataifa masikini ya kulinda sheria, haki za kiraia,
utawala bora na kuleta maendeleo shirikishi (Inclusive Develeopment).
Kauli nyingi za kuchochea chuki na uhasama
alizozitoa Rais Magufuli si za kwanza wala si ngeni kwa Wazanzibari. Kisiasa
wazanzibar na hasa wafuasi wa CUF (ambao ni wengi) wamekuwa waathirika wakubwa
wa matumizi makubwa ya ukandamizaji na unyanyasaji iunaofanywa kikatili sana kupitia
MAJESHI, MAZOMBI, JANJAWIDI nakadhalika. Mauaji yaliyofanywa na Serikali
ya CCM chini ya utawala wa serikali ya awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamini
William Mkapa Januari 26-27, 2001
yalisababisha watu 46 kuuliwa na vyombo vya Ulinzi, watu 38 wameuwawa kwa kificho mpaka leo hawajaonekana. Watanzania 658 waliojeruhiwa, na 135 waliopata vilema vya kudumu katika maisha yao. Aidha zaidi ya wazanzibar 4000 waliishi kama wakimbizi Shimoni, Mombasa nchini Kenya, orodha yao tumeiambatanisha na taarifa hii. Kama kweli Rais Magufuli anataka kulinda amani ya Tanzania haiwezekani kuwa raia wamekuwa wakipigwa na kuteswa na kukatwa viungo vyao na kuporwa mali zao na vikosi vya majeshi, Mazombi na akiwa kimya na kutoa kauli za kubariki vitendo hivyo. Kwa mtizamo wa Magufuli, ukatili na uhuni unaotendwa na MAZOMBI ukiungwa mkono na vikosi vya majeshi ya SMZ na vile vya Muungano eti ndiyo ulinzi wa amani. Lakini, Kauli mfano wa hizi zimewahi kutolewa na watangulizi wake na viongozi wa Zanzibar waliopita. Hata hivyo mwisho wa yote hawakuweza kufanikiwa kuwahadaa wazanzibari kudai haki yao na mwaka hadi mwaka wazanzibar wanaotaka mabadiliko wawekuwa wakiongezeka na kuidhihirishia dunia kuwa hawawezi kuvunjwa moyo na vitisho, hujuma na ukandamizaji.
yalisababisha watu 46 kuuliwa na vyombo vya Ulinzi, watu 38 wameuwawa kwa kificho mpaka leo hawajaonekana. Watanzania 658 waliojeruhiwa, na 135 waliopata vilema vya kudumu katika maisha yao. Aidha zaidi ya wazanzibar 4000 waliishi kama wakimbizi Shimoni, Mombasa nchini Kenya, orodha yao tumeiambatanisha na taarifa hii. Kama kweli Rais Magufuli anataka kulinda amani ya Tanzania haiwezekani kuwa raia wamekuwa wakipigwa na kuteswa na kukatwa viungo vyao na kuporwa mali zao na vikosi vya majeshi, Mazombi na akiwa kimya na kutoa kauli za kubariki vitendo hivyo. Kwa mtizamo wa Magufuli, ukatili na uhuni unaotendwa na MAZOMBI ukiungwa mkono na vikosi vya majeshi ya SMZ na vile vya Muungano eti ndiyo ulinzi wa amani. Lakini, Kauli mfano wa hizi zimewahi kutolewa na watangulizi wake na viongozi wa Zanzibar waliopita. Hata hivyo mwisho wa yote hawakuweza kufanikiwa kuwahadaa wazanzibari kudai haki yao na mwaka hadi mwaka wazanzibar wanaotaka mabadiliko wawekuwa wakiongezeka na kuidhihirishia dunia kuwa hawawezi kuvunjwa moyo na vitisho, hujuma na ukandamizaji.
Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amemsifia
Dokta Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wazanzibar kwa kura nyingi.
Jambo hili linachekesha na kustaajabisha dunia, kwani Hata mtoto mdogo
anayeishi Zanzibar au Tanganyika anatambua kuwa Dr. Shein si rais halali wa Zanzibar.
Ni rais aliyeingizwa madarakani kwa kile kinachoweza kuitwa “tyranny
of the highest order of the African Power Mongers who are ready to shed blood
for power” yaani “udhalimu wa kiwango cha juu kabisa
kinachofanywa na viongozi waroho wa madaraka ambao wako tayari kumwaga damu ili
watawale”. Katika uchaguzi halali wa tarehe 25/10/2016. Wazanzibar
walimchagua kwa kura nyingi kabisa, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wao.
Wazanzibari wanajua hivyo, Watanzania wanajua hivyo, Waafrika wanajua hivyo na
dunia inaimba wimbo huo. Kujidanganya kuwa Dokta Shein ni rais halali wa
Zanzibar ni uotaji wa ndoto ya mchana kuwa Tanzania ina viwanda kila kata na
kila kijiji, ndoto ambayo kwa aina ya uongozi wa John Magufuli haiwezi kutimia.
TAKWIMU ZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA TAREHE
25/10/2015:
Wapiga kura wote wa NEC Zanzibar ni 417,882. Kura
alizopata LOWASSA 211,033 = 50.05% kura alizopata MAGUFULI ni 194,317=
46.50% Ushindi wa kura za lowassa dhidi ya Makufuli ni 16,721.
ZEC wapiga kura wote ni 402,354. Kura alipigiwa Maalim
Seif ni 207,847 =53.32%. kura alizopata Dokta Ali Mohamed Sheni ni
182,011 =46.68%. Ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad dhidi ya Dk Sheni ni
kura 25,836.
Kwa matokea haya ni wazi kuwa Wanzanzibar wameikataa
CCM. Wazanzibar hawakuwachagua wagombea wa CCM John Magufuli na DK Shein wake.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF CHAMA CHA WANANCHI)
kinaendelea na msimamo wake uliotolewa na kikao cha Baraza KUU la uongozi Taifa
kilichofanyika tarehe 2-3 April, 2016 wa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi huo
haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais
wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui
waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar
waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali,
Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao. CUF itaendeleza
msimamo wake wa kutoshirikiana na Serikali haramu iliyoundwa na dokta Shein
kutokana na uchaguzi batili uliofanyika kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume
na Sheria ya Uchaguzi. Kwa vyovyote vile, Serikali ya dokta Shein haitakidhi
matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa
Katiba ya nchi.
Chama Cha Wananchi CUF, kinaendelea na msimamo wake
wa kuutambua uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru, wa haki na uliofanyika katika
hali ya amani na utulivu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia linayatambua matokeo
yake ambayo yanaonyesha wazi kwamba chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif
Sharif Hamad Kitendo cha zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari kususia uchaguzi
haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 kimezidi kuyapa nguvu maamuzi yao ya
tarehe 25 Oktoba, 2015 mbele ya macho ya Watanzania na kwa Jumuiya ya
Kimataifa. Chama cha CUF na Viongozi wake hawawezi kuyumbishwa na watu
wenye weledi mdogo sana na siasa za Zanzibar, kama alivyoonesha Rais John Pombe
Magufuli. Vitisho vyote vilivyotolewa na Magufuli dhidi ya wanaosimamia HAKI
SAWA KWA WOTE na misingi ya kidemokrasia, havitarudisha nyuma juhudi za
kuijenga Zanzibari na Tanzania mpya.
Tunamtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli afahamu
kuwa stahiki zote anazopewa Maalim Seif zipo kisheria kwa mujibu wa katiba ya
Zanzibar na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama wanavyopewa viongozi
wastaafu wengine hapa nchini. Stahiki hizo si hisani inayotoka mfukoni mwa
kiongozi yeyote Yule. Wala si fedha za CCM, ni fedha za watanzania zinazotokana
na makusanyo ya kodi zinazolipwa na wananchi. Sheria ya Mafao ya Viongozi
wastaafu wa Kisiasa ya Zanzibar (The Political Leaders Retirement
Benefits Act) namba 6 ya mwaka 1999 iliyopitishwa na Dr. Salmin
Amour tarehe 15 Mei 2000) imeeleza wazi kuwa viongozi wote wa kisiasa
waliohudumu katika serikali ya Zanzibar kuanzia mwaka 1995 kwenda mbele
watakuwa na haki isiyoondolewa kwa namna yoyote, ya kupokea stahiki zote muhimu
kama viongozi wastaafu. Rais Magufuli amekuwa rais wa kwanza Tanzania
mwenye kutoa kauli zenye ukakasi kwa jamii, zenye kugongana na tabia ya kufanya
maamuzi bila kuangalia katiba na sheria za nchi. kwake yeye urais siyo taasisi,
ni mtu, kwa Magufuli urais ni ubabe, dhuluma, vitisho, kukandamiza na kutojali
katiba na sheria za nchi. Huenda Taifa letu limepata janga kubwa la
kitaifa katika awamu hii ya uongozi wa nchi. Ni jambo la aibu sana
kuona rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavunja sheria za nchi yake na
anamhamasisha rais wa Zanzibar afanye kama anavyofanya yeye.
Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli anazungumzia
kulinda amani bila kuzungumzia kulinda haki. Na wakati huo huo anachochea
matumizi makubwa ya kijeshi yasiyozingatia sheria kwa wananchi. Mifano
aliyoitoa ya nchi zilizoingia katika uvunjifu wa amani haina uhusiano kabisa na
masuala yanayoendelea katika nchi yetu. Rais Magufuli anasahau kuwa nchi hizo
anazozitolea mifano, ziliharibiwa kwa sababu ya kuwa na viongozi walioamini
katika nguvu za kijeshi (kama yeye) kuliko uongozi wa kidemokrasia na wa
kufuata sheria. Raia wa nchi hizo anazozitaja Magufuli walinyimwa haki za
msingi za muda mrefu na watawala ndipo wananchi walipoanzisha harakati za
kujikomboa, majeshi yaliyoziunga mkono hayakuweza kuzima nguvu ya mabadiliko.
Ni jambo lisilokubalika hata kidogo kuwa na rais ambaye kila kukicha mahubiri
yake ni namna gani “majeshi yake yatawashughulikia raia wa nchi yake”. Hizi ni
hotuba zinazowafanya wananchi wajiandae kisaikolojia kupambana na majeshi yao.
Watanzania hawakumchagua Magufuli ili ayaandae majeshi kwa ajili hiyo,
alikabidhiwa nchi hii ikiwa na amani na CUF haitakuwa tayari kumuona anaiingiza
katika migawanyiko, vitisho na visasi ambavyo vinaweza kuzaa machafuko.
Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
–ZEC (Jecha SALIM Jecha) kuhudhuria na kushiriki katika mkutano wa CCM
uliofanyika Unguja ni ushahidi tosha kuwa tume ya uchaguzi ya ZEC si chombo
kilicho huru na kwamba tume hiyo ipo hapo kuhakikisha kuwa Serikali ya CCM
haiondolewi madarakani na wananchi wanaotaka mabadiliko ya uongozi wa kisiasa
nchini na kwamba ZEC ni tawi la CCM linalotekeleza matakwa yao. Kwa msingi huo
huo, CUF na vyama vingine ambavyo vinapigania mabadiliko hapa Tanzania
vitaendeleza mipango imara ya kupigania kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi
Zanzibar na Tanzania Bara (NEC na ZEC). Ni jambo lisilokubalika hata kidogo
kujisifia ushindi wa kupora katika uchaguzi kutokana na kupendelewa na Tume ya
Uchaguzi ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Tunamtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli atambue
kuwa; CUF ni taasisi kubwa ya kisiasa nchini iliyo na wawakilishi wa kuchaguliwa
na wananchi kutoka kila kona ya nchi yetu, CUF ina wabunge 18 kutoka Pemba,
inawabunge wanne (4) kutoka unguja, inawabunge 10 kutoka Tanzania bara. CUF ni
chama cha kitaifa kweli, na tangu mwaka 1995 mpaka sasa CCM haijawahi kupata
kiti hata kimoja cha uwakilishi toka Pemba. Magufuli asaidiwe na chama chake,
kwamba matamanio yake ya kuifanya Tanzania iwe nchi ya mapambano ya kijeshi na
raia hayatafikiwa. Akumbushwe kuwa kauli zake zimejaa uchochezi wa kila namna
anajaribu kuwaghadhibisha wananchi (Provoke), ghilba za kisiasa za waziwazi na
nia ovu iliyojaa visasi. Kauli za namna hii akiendelea kuzitoa katika kipindi
cha miaka yake mitano, ataimaliza huku kila mtanzania akijiridhisha kuwa nchi
ilipata rais ambaye hakujua nini maana ya urais, na kwa vyovyote vile
hakuwatendea haki waliomchagua.
Mwisho:
Sote tunatambua kuwa Serikali ya CCM kwa kumtumia
Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli imeshindwa katika ulingo wa kisiasa kwa
kushindana kwa hoja, imekosa uvumilivu wa kisiasa na badala yake inaendesha
nchi kwa mfumo wa mabavu bila kuzingatia sheria, haki na wajibu, taratibu na
kanuni. Hebu tujiulize, ni nchi gani duniani ambayo ilishinda NGUVU YA UMMA
INAYOTAKA MABADILIKO?
Madhumuni ya harakati za kupigania uhuru wa nchi
yetu miaka ya 1953-1961 yalikuwa na lengo la kutuondoa watanganyika kutoka
katika utumwa, unyonyaji, unyanyasaji, ukandamizaji, ubepari na ubeberu wa
rasilimali za Taifa letu na watu wake.
Jeshi la mkoloni lilikuwa likitumika kuwadhalilisha
wazee wetu. Leo hii baada ya miaka 55 ya kujitawala, tukiwa ndani ya mfumo
halali wa kisheria wa demokrasia ya vyama vingi nchini, serikali ya CCM kwa
kumtumia Rais John Magufuli inaturudisha nyuma na kufanya vitendo vibaya zaidi
kwa raia wake kuliko ilivyokuwa ikifanywa na wakoloni! Cha kusikitisha takwimu
hazionyeshi jeshi la polisi lilipotumia nguvu kubwa kupambana na raia kisha
raia wakafungua mashtaka mahakamani, Serikali (Jeshi la polisi) ni lini
lilishinda kesi hizo.
Mauaji ya mwandishi David Mwangosi ni ushahidi wa
hili na kesi nyingine nyingi orodha ni ndefu ambazo zikifikishwa mahakamani
haki inaangukia kwa walioshtakiwa? Tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa kamwe
hatoweza kuzuia nguvu kubwa ya watanzania iliyo tayari kuleta HAKI SAWA KWA
WOTE na mabadiliko sahihi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, na kuboresha hali za
maisha na kipato cha mtanzania kwa kutumia vyema rasilimali za nchi yetu.
Tuna kila sababu ya kuunganisha nguvu zetu kama
watanzania kumzuia Rais kwa njia ya amani asiendelee kuikanyaga katiba ya nchi
aliyoapa kuilinda. Tunahitaji Taifa letu liwe salama na hatuhitaji kwa namna
yeyote ile uvunjwaji wa sheria na matumizi ya nguvu kubwa za vyombo vya dola
yanayoandaliwa na rais mwenyewe ili yafanywe dhidi ya wananchi wadai
demokrasia.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)
Kinawataka watanzania wote bila ya kujali itikadi za vyama vyetu kusimama imara
kutetea misingi ya uongozi wa Taifa letu kwa kuilinda na kuihifadhi katiba na
sheria za nchi yetu na kuhakikisha zinaheshimiwa, zinafuatwa na kuhifadhiwa na
kila mmoja wetu.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha
Wananchi) tunawahakikishia watanzania wote kuwa daima tutaendelea kusimama
imara na kuwaunganisha watanzania wote ili kuimarisha umoja na mashirikiano
baina yetu ya KUDAI HAKI SAWA KWA WOTE NA DEMOKRASIA YA KWELI kwa maslahi
mapana ya Taifa letu.
HAKI SAWA KWA WOTE
____________________________________
JULIUS MTATIRO
MWENYEKITI KAMATI YA UONGOZI CUF -TAIFA