PROFESA LIPUMBA APUUZWA KILA KONA,SASA AONEKANA KICHEKESHO KWENYE JAMII,SOMA HAPO KUJUA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba ameendelea kupingwa ndani ya chama hicho, na safari hii
jumuiya ya wanawake wa chama hicho ikiibuka na kumtaka ajiweke kando ili
kuepusha mpasuko zaidi.
Aidha, wamewataka wanawake wafuasi wa chama hicho
kote nchini, kuunga mkono uongozi wa muda uliowekwa na Baraza Kuu la Uongozi wa
CUF hivi karibuni, ambao ulimtangaza Julius Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Muda ya Uongozi ndani ya chama hicho kilichowahi kuwa kikuu cha upinzani
Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini
Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF, Savelina
Mwijage ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema kauli yao imelenga kuunga
mkono hatua iliyochukuliwa na Baraza la Uongozi dhidi ya wanaotajwa kukiuka
Katiba.
Baraza hilo lilikutana Agosti 28, mwaka huu mjini
Zanzibar ikiwa ni hatua ya kukabiliana na hali ya hewa iliyochafuka baada ya
kundi la wanachama kuvamia Mkutano Mkuu Maalumu wa uchaguzi Agosti 21, mwaka
huu jijini Dar es Salaam.
Mwijage aliyefuatana na wabunge wengine wanne wa
viti maalumu, amesema wanawake ndani ya CUF wamefedheheshwa na wafuasi wa
Profesa Lipumba kwa kufanya vurugu, kudhalilisha wanawake wakati wa mkutano wa
Dar es Salaam na pia kukisababishia chama hasara ya Sh milioni 600 zilitozumika
kugharamia mkutano huo.
“Tunalaani kwa nguvu zote vitendo vya
baadhi ya watu wanaotaka kukivuruga chama, lakini pia kuiingiza nchi katika
migogoro ya udini, ukabili, ubara na Uzanzibari. Mbinu hiyo imepitwa na wakati,
tunawaomba Watanzania wote wapuuze siasa hizo za uchochezi,”alisema.
Akizungumza hatua ya kusimamishwa kwa baadhi ya
viongozi 11 wa juu wa chama hicho, wanaodaiwa kushiriki kukivuruga chama,
alisema ni hatua sahihi na kwamba hata Profesa Lipumba hapaswi kuwa nyuma ya
vurugu hizo, kwani aliachia madaraka kwa hiyari yake wakati chama kikielekea
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kauli ya wanawake hao wa CUF ilikuja saa chache
baada ya Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya ambaye ni mbunge pekee wa kike
mwenye jimbo kutoka chama hicho, kuliambia Bunge kuwa hajatikiswa na uamuzi wa
kumsimamisha uanachama na kwamba anaendelea kutimiza majukumu yake ndani ya
chama, ambacho kabla ya mpasuko wa hivi karibuni, ndiye aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu Tanzania Bara.
Mbali ya Lipumba na Sakaya, wengine waliositishiwa
uanachama ni Abdul Kambaya ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
chama hicho, Ashura Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha,
Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.
Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na aliwahi kuwa Naibu
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa
wabunge kipindi cha 2010-2015; Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo
Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.
Kutokana na kusimamishwa kwa viongozi hao, Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alimtangaza Mtatiro aliyewahi
kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara kuwa kiongozi wa kamati ya uongozi wa muda,
inayowajumuisha pia Ahmed Katani na Mwijage ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa.
Katani ni Mbunge wa Tandahimba, Mtwara wakati
Severina alikuwa mjumbe wa kamati kama hiyo ilipoteuliwa Agosti mwaka jana
baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu uenyekiti kwa barua ya Agosti 5, mwaka jana.
Baraza hilo lilimteua pia Joram Bashange kukaimu
nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbaraka Maharagande kuwa Kaimu Naibu
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi hapo nafasi hizo
zitakapojazwa rasmi kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Chama hicho