WAZIRI MKUU AJITETEA KUHUSU MADAI YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO KUSHINDWA KUONGOZA NCHI,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya
Awamu ya Tano ipo macho, haijalala na haijashindwa kuongoza nchi bali
imejipanga kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.
"Serikali haijashindwa kuongoza
nchi. Nataka niwahakikishie waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwamba
tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa na kazi hiyo imeanza kwa marekebisho
makubwa kwa maeneo ambayo tunadhani yatafanya Taifa hili liweze kupata
mafanikio makubwa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 8, 2016)
Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Bw. Freeman Mbowe, ambaye alitaka kufahamu
Serikali ina mkakati gani wa kunusuru mdororo wa uchumi uliopo nchini.
Bw. Mbowe alidai kwamba hali ya uchumi imeshuka na
kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) uagizaji wa bidhaa kutoka
nje umepungua, uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na sekta ya ujenzi imesimama hali
inayoashiria kudorora kwa uchumi.
Kuhusu suala la kupungua kwa mizigo katika bandari
na vituo vya forodha, Waziri Mkuu amesema usafirishaji wa mizigo kwa njia ya
bahari umeshuka duniani kote kwa sababu ya kushuka kwa hali ya uchumi kutokana
na kuporomoka kwa bei ya mafuta na gesi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema tayari wafanyabiashara
wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wameihakikishia Serikali
kwamba mizigo yao yote itakuwa inapitia Bandari ya Dar es Salaam hasa kwa
mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya standard gauge inayoanzia Dar es
Salaam-Tabora - Isaka.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali
itahakikisha inaendelea kuimarisha amani na ulinzi kwenye maeneo yote nchini na
kwamba vyombo vya dola viko macho. “Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya
uhalifu yakiwemo mauaji watakamatwa popote walipo na kuchukuliwa hatua za
kisheria,; amesema.
Amesema hatua hiyo inatokana na matukio ya mauaji
yaliyotokea hivi karibuni ambapo raia wasiokuwa na hatia na askari waliuawa
katika maeneo ya Vikindu mkoani Pwani, Tanga na Mwanza. Waziri Mkuu ameyasema
hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani
Katika swali lake, Bw. Ngonyani alitaka kujua ya
Serikali kuhusu kukomesha mauaji hayo, yanayotokea kwa watu wasio na
hatia pamoja na askari, ambapo Waziri Mkuu, alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa
wananchi na familia, ambazo ndugu zao walipoteza maisha katika mauaji hayo.
Pia ametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha
wanawafichua watu ambao wanawatilia shaka na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola
ili waweze kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua
Habari na Ofisi ya Waziri Mkuu