POLISI YAJITETEA KUHUSU KUWAKAMATA WATU WANAOLALA GESTI WAKATI WA MCHANA,SOMA HAPO KUJUA
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar Es Salaam anatoa
rai kwa wakazi wa Jiji la Dar Es salaam na wageni wanaoingia jijini wakitokea
mikoani kupuuza taarifa za sauti zinazozagaa katika mitandao
ya kijamii kuwa Polisi wanawakamata ovyo watu wanaolala kwenye nyumba za kulala
wageni.
Taarifa hizo za uvumi zinazoendelea
kuzagaa kwenye mitandao ya Kijamii kama WHATSAPP, TELEGRAM na pia
zimechapishwa kwenye baadhi ya magazeti kwamba Askari Polisi wanawakamata
watu ovyo mchana wakiwa kwenye nyumba za kulala wageni kwa madai ya
kukamata kwa makosa ya uzembe na uzururaji na pia kutimiza kauli ya Raisi wa
Jamhuri ya muungano wa Tanzania ‘HAPA NI KAZI TU’.
Kimsingi niwatoe hofu raia wema kuwa tunaendelea na
oparesheni za kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwemo wanaofanya
biashara ya nyumba za kulala wageni kinyume cha sheria (guest bubu), majambazi
na wahalifu wengine wa makosa mbalimbali.
Aidha taarifa za kuaminika zimebaini kuwa baadhi ya
nyumba za kulala wageni zimekuwa zikitumika kuhifadhi magenge ya wahalifu, dada
poa na kaka poa, hivyo Jeshi la Polisi tunawajibika kufuatilia na kuwakamata
wahalifu.
Niwajibu wa Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
kwenye nyumba za kulala wageni, Hoteli, migahawa, Vilabu vya vileo, kumbi
za starehe zinazokesha na zisizokesha na watakaobainika kuvunja sheria, hatua
kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.
Sheria ya Mwenendo ya makosa ya jinai kifungu cha
60(1) (sura ya 77 iliyofanyiwa marekebisho 2002) kinampa nguvu askari kufanya
ukaguzi wa maeneo yote yaliyotajwa hapo juu na kumkamata mtu yeyote anayetiliwa
shaka akienda kinyume na utaratibu wa biashara hizo.
Sambamba na hayo nawatahadharisha wafanyabiashara
wote wa nyumba za kulala wageni wafuate taratibu za kupokea wageni kwa kuandika
kwenye vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanayotoka, na
pale watakapomtilia mashaka mteja yeyote watoe taarifa kituo chochote cha
polisi.
Pia wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wa
nyumba kumi wanawajibika kuwatambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na
kuwachukulia hatua stahiki ili kuimarisha usalama katika jiji letu la Dar
Es salaam.
DAR ES SALAAM BILA UHALIFU INAWEZEKANA, TUSHIRIKIANE
KUISAFISHA JIJI LETU
S.N.SIRRO - CP
KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM