Zinazobamba

Mwigulu: Polisi ‘washughulikieni’ wanaowakashifu


 Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani
MWIGULU Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani, amevitaka vyombo vya usalama hapa nchini, kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaolikashifu Jeshi la Polisi, ikiwemo kusambaza picha za polisi wanaouawa na majambazi, anaandika Moses Mseti
Kauli ya Mwigulu inakuja ikiwa ni wiki moja tu baada ya Jeshi la Polisi hapa nchini kuwakamata wafuasi wa Chadema zaidi ya kumi katika pande mbalimbali za nchi na kuwasafirisha hadi Dar es Salaam ambapo waliripotiwa kupigwa na kuteswa na jeshi hilo.
Akizungumza na wakuu wa Polisi, zimamoto na idara ya uhamiaji katika magereza ya Butimba, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, waziri huyo amesema watu wamekuwa wakilikashifu na kulidhalilisha Jeshi la Polisi jambo ambalo halivumiliki.

“Polisi msisite kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaowadhalilisha ikiwemo kusambaza picha katika mitandao ya kijamii, polisi wanapouawa na majambazi ili kuwa fundisho kwa watu wengine,” amesema na kusisitiza;
“Mbona hatujawahi kuona wanaweka picha za ndugu zao ama watoto wao wanapokufa kwenye mitandao ya kijamii, iweje waweke picha za polisi?”
Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo wa Iramba Magharibi, Singida amesema polisi hawapaswi kudhalilishwa kwa kutuma picha zao mitandaoni wanapouawa kwani ni wazalendo wanaojitoa muhanga kwa kulala nje ili kulinda maisha ya watanzania.
“Wananchi wamekuwa wakiwahusisha polisi na masuala ya siasa jambo ambalo si la kweli kwani kazi ya polisi ni kutekeleza sheria bila kujihusisha na mambo ya siasa. Wasipochukua hatua kali heshima kati ya polisi na wananchi haitakuwepo.