JWTZ LALIA NA GAZETI LA TANZANIA DAIMA,SOMA HAPO KUJUA
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
limesikitishwa na taarifa iliyotolewa na gazeti la Tanzania Daima toleo Nambari
4290 la tarehe 01 Septemba 2016, ikihusisha shughuli za Jeshi hilo
zinazoendelea katika maadhimisho ya miaka 52 ya kuzaliwa kwake na shughuli za
kisiasa.
Tunapenda kuwataarifu wananchi kwamba kazi ya
Jeshi ni kulinda na kutetea maslahi ya Taifa na mipaka ya nchi, aidha, Jeshi
letu linafanya kazi kwa kufuata mila, desturi, nidhamu, kanuni na sheria za
Kijeshi kwa weledi wa hali ya juu, hivyo lisihusishwe na propaganda zozote za
kisiasa kwani Jeshi letu ni lenye maadili ya kitaasisi ya hali ya juu.
Jeshi ni taasisi ya dola wala si taasisi ya
kiitikadi, kwa maana uhusiano wake na wanasiasa ni wakati linapotetea na
kulinda maslahi ya wananchi. Inaombwa kuwa makini katika utoaji wa
maelezo au malalamiko, iachwe mara moja vyama vya siasa kuingilia ratiba za
Kijeshi.
Ikumbukwe kwamba tarehe 25 Julai kila mwaka ni siku
ya kuwakumbuka Mashujaa wetu waliolitumikia Taifa hili kwa umakini na nguvu
zote kwa kuleta mafanikio tunayoyaona, na hii ilipitishwa mwaka 1979 wakati
Majeshi yetu yanarudi kutoka Uganda baada ya ushindi wa vita vya Kagera.
Sherehe ya mapokezi hayo yalifanyika mji wa Bunazi
Wilaya ya Misenye wakati huo Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera ilipoanzishwa kuwa
tarehe hiyo iwe siku ya Mashujaa na kupitishwa Kisheria, ikabaki siku ya
tarehe 01 Septemba kuwa ni siku ya kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania, hivyo jana tulikuwa tunasherekea siku ya kuzaliwa JWTZ. Ieleweke
hivyo na iachwe mara moja kuchanganya shughuli za Kijeshi na mambo ya Kisiasa,
viongozi wa kisiasa wekeni kumbukumbu zenu vizuri.
Jeshi linasisitiza wanasiasa ni vizuri wakasoma vema
historia ya nchi wanayotaka kuiongoza na wanayoongoza ili kuepusha upotoshaji,
lugha na maneno yanayotolewa na viongozi wa kisiasa wenye matakwa binafsi
kuhusisha shughuli za Jeshi na siasa zao yanatia ukakasi na kiungulia, awe
makini kuongea vitu ambavyo haelewi na kutokuwa makini zaidi aelewe madhara
yanayoweza kutokea kutokana na upotoshaji.
Jeshi letu linafanya shughuli zake ki
weredi.
Imetolewa na Kurugenzi ya
Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Dar es Salaam,
Tanzania.
Kwa Mawasiliano zaidi: 0784-477638