JPM ATONESHA KIDONDA CHA FREEMAN MBOWE NA MKURUGENZI WA NHC,SOMA HAPO KUJUA
RAIS John Magufuli amepongeza hatua ya Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) kumwondoa Freeman Mbowe, katika jengo ambalo amekuwa
akipanga kwa muda mrefu, anaandika Pendo Omary.
Siku tano zilizopita, Mbowe
ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pia Mbunge
wa Jimbo la Hai aliondolewa kwenye jengo hilo na mawakala wa NCH, Fosters
Auctioneers kwa madai ya kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. 1.3 Bilioni huku
mvutano wa kuwepo kwa uhalali wa deni hilo ukiendelea.
Jengo hilo lipo katika makutano ya Mitaa ya Mkwepu
na Indira Gandhi (Makunganya) jijini Dar es Salaam ambapo mawakala hao
walichukua vifaa vya kampuni hiyo katika upande wa uzalishaji Gazeti Tanzania
Daima chini ya Kampuni ya Free Media.
Rais Magufuli alilisifu shirika hilo leo asubuhi
wakati akizungumza na baadhi ya waliokuwa wapangaji katika nyumba za NHC
zilizokuwepo Magomeni Kota ambazo zilibomolewa mwaka 2012.
Kwenye mkutano huo Rais Magufuli amelitaka shirika
hilo ndani ya siku saba kuwaondoa wapangaji wote wanaodaiwa na serikali kwenye
nyumba zake.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amesema, ndani
ya miezi miwili kuanzia leo serikali itaanza kujenga nyumba za waliokuwa wakazi
wa eneo hilo.
Waliokuwa wapangaji katika nyumba za Magomeni Kota
zilizomilikiwa na serikali waliondolewa kwa mkataba na Manispaa ya Kinondoni
katika makazi hayo mwaka 2012 kupisha ujenzi wa makazi mapya kwa muda wa mwaka
mmoja.
Katika mkataba huo makubaliano yalikuwa; manispaa
hiyo kuwalipa wapangaji hao kodi ya nyumba ya muda wa mwaka mmojo na mara baaya
ya ujenzi kupangishwa katika nyumba hizo na baadaye kuuziwa, hata hivyo mpaka
sasa hakuna kilichotekelezwa.
Rais Magufuli amesema, “kwa sasa eneo hili la heka
33 lipo mikononi mwangu. Ndani ya miezi miwili, tutaanza kujenga nyumba na
majengo ya mwanzo ni ya wakazi 644. Tutaanza kutoa fedha mwezi huu.
“Yatakapo malizika kujengwa, orodha ya majina yote
ninayo wawe wapo hai au watoto wao ndio watakaoingia kwenye nyumba hizo.
Nikishamaliza kujenga hizo nyumba hao wakazi 644 watauziwa nyumba.”
Rais Magufuli amesema, ujenzi wa nyumba hizo
utakapokamilika ndani ya muda wa mwaka mmoja kuanzia sasa, kabala ya wakazi hao
kuuziwa nyumba hizo, serikali itawaruhusu kuishi kwa muda wa miaka mitano bila
kulipa kodi ambapo baada ya muda huo kupita ndipo watauziwa. Hatua hiyo
inalenga kufidia ghalama walizotumia tangu waondolewe katika nyumba hizo.