FAMILIYA YA ALIYEUWAWA KWENYE KESI YA ZOMBE AMUANGUKIA RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kinondoni, SP Christopher Bageni akisindikizwa kupanda gari la askari baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa |
Baada ya Mahakama ya Rufani kutoa hukumu dhidi ya
vigogo wa polisi katika mauaji wafanyabiashara wa madini, familia ya mmoja wa
marehemu amemuomba Rais John Magufuli kuwasaidia yatima walioachwa.
Akizungumza jana, Martha Martine ambaye alikuwa mke
wa marehemu Mathias Lunkombe alisema kwa kuwa mahakama imeshatoa hukumu hiyo,
hawezi kupingana nayo, badala yake akaeleza namna kifo cha mumewe
kilivyoiathiri familia, hususan watoto wawili alioachiwa.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa juzi, aliyekuwa mkuu
wa upelelezi wa makosa ya jinai Wilaya ya Kinondoni, Christopher Bageni
alihukumiwa kunyongwa hadi kufa huku Abdallah Zombe na wenzake wawili
wakiachiwa huru.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya rufani ya Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) ambaye hakuridhishwa na hukumu ya Mahakama Kuu ambayo
iliwaachia huru washtakiwa hao.
Bageni alikuwa ni miongoni mwa washtakiwa kwenye
kesi hiyo iliyokuwa inawakabili askari polisi tisa akiwamo Zombe ambaye alikuwa
Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam.
Wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, ndugu yake Eprahim
Chigumbi na Mathias Lunkombe na dereva teksi, Juma Ndugu waliuawa Januari 14,
2006 kwenye Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Kutokana na hukumu hiyo, Martha alisema kwa sasa
anaishi maisha magumu kwa kuwa anatumia fedha nyingi kuwasomesha watoto wake
Grace anayesoma kidato cha nne na Fulmes anayesoma kidato cha pili.
Alisema Serikali ilimuahidi kumsaidia kutunza watoto
lakini hakuna msaada wowote alioupata kutoka serikalini wala kwa kiongozi
yeyote.
Kutokana na hali hiyo, Martha alimwomba Rais
Magufuli kuwasaidia watoto hao kupata elimu na mahitaji mengine muhimu ili
waweze kuja kujitegemea kimaisha.
Mdogo wa marehemu Protas, Mathias Lunkombe alisema
tangu kaka yake alipofariki amekuwa akihudumia familia mbili, ya kwake na ya
marehemu kaka yake.
Kuhusu hukumu iliyotolewa, alisema haki imetendeka
kwa kumhukumu Bageni kunyongwa hadi kufa japokuwa hakuna hukumu ambayo ingeweza
kupoza au kuondoa machungu waliyonayo kwa ndugu yao aliyeuawa.
“Pamoja na kumuua kaka yangu lakini kifo
chake ni cha kumdhalilisha kwa sababu walimsingizia kuwa ni jambazi ilhali ni
mfanyabiashara wa madini. "
Mke wa Bageni asita
Wakati familia ya Lunkombe ikisema hayo, mke wa Bageni amekataa kuzungumzia hukumu kifo iliyotolewa kwa mumewe.
Mke wa Bageni asita
Wakati familia ya Lunkombe ikisema hayo, mke wa Bageni amekataa kuzungumzia hukumu kifo iliyotolewa kwa mumewe.
“Mimi ni askari, nipo chini ya Kamishina
(wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon) Sirro, siwezi kuongea na waandishi
wa habari siruhusiwi kuongea chochote,” alisema mke wa
Bageni, Stella Saria na kuongeza:
“Kijeshi sisi tuna miiko ya kazi, kama
mume wangu amepata matatizo hayo ni mambo ya kawaida, mimi nina viongozi wangu
wa kazi, nilivyofundishwa kama ni kitu cha familia yangu, Christopher alikuwa
ofisa wa polisi watajibu viongozi wake wapo.
“Mimi nina amani ya kutosha, ni Mkristo
nimempokea Yesu, tatizo haliwezi kunitokea nikadharau miiko ya kazi. Mimi ni
kiongozi askari, naelewa miiko ya kazi lazima niiheshimu, samahani sana.”