SUMATRA YACHUKUA UAMUZI MGUMU KWA MADEREVA WALIOGOMA BUKOBA,SOMA HAPO KUJUA
,
JESHI
la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesitisha leseni za
madereva 18 kutokana na mgomo walioufanya kupinga wenzao kupelekwa mahakamani.
Wamiliki
wa mabasi 12 ambayo madereva hao walikuwa wanaendesha kwenda sehemu mbalimbali
nchini, wamepewa siku saba kujieleza ni kwa nini wasifutiwe leseni za kutolea
huduma hizo pamoja na kutakiwa kusitisha ajira kwa madereva hao.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema Julai 23 mwaka huu mkoani Kagera, madereva
wa mabasi hayo walifanya mgomo kupinga kitendo cha madereva wenzao kupelekwa
mahakamani, kukosa dhamana na kulala rumande kutokana na makosa mbalimbali ya
usalama barabarani ikiwamo kuendesha kwa mwendo kasi.
Kamanda
Mpinga alisema dereva yeyote atakayeendesha gari kwa kasi ya zaidi ya kilometa
90 kwa saa atafikishwa mahakamani na sio kutozwa faini kama awali ili kuhakikisha
matukio ya ajali yanapungua nchini.
Alisema
kutokana na hali hiyo madereva wanaoendesha mabasi yanayoanza safari zake
kwenye Manispaa ya Bukoba, walisitisha huduma kwa kushinikiza Mahakama iwaachie
wenzao waliokamatwa kwa makosa ya mwendo kasi.
‘’Serikali haitavumilia kuona madereva wasiofuata sheria za
usalama barabarani na sheria za kazi na ajira. Jeshi la Polisi ndio tunawapa
madereva mafunzo, tunasajili vituo vya mafunzo na kuwapa leseni. Hivyo
tunasitisha leseni zao kwa mujibu wa sheria kwa kukiuka kanuni za leseni,’’ alisema Mpinga
na kuongeza kuwa askari watakaoachia madereva na kampuni za mabasi kutembea kwa
zaidi ya kilometa 90 kwa saa watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mkurugenzi
wa Sumatra, Gilliard Ngewe, aliyataja mabasi pamoja na madereva waliositishiwa
leseni kuwa ni Hussein Tegatega na Miraji Kondo wa Kampuni ya RS Express
wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 425 DDT aina ya Zongtong linalotoka
Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Said
Omary na Amos Danney wa basi la Kimotico lenye namba za usajili T 966 CDY aina
ya Nissan linalotoka Bukoba kwenda Arusha na madereva wanne wa mabasi ya
Princess Muro yenye namba za usajili T 166 DCA na T 923 DCT yanayosafiri kutoka
Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Madereva
hao ni Ally Mshuza, Twalibu Ondossy, Costa Andrew na Witness Lema.
Madereva
wengine ni Musa Tindwa na Gerald Beti wa Kampuni ya Osaka Raha wanaoendesha
basi lenye namba za usajili T 968 CPC linalofanya safari zake Bukoba kwenda Dar
es Salaam na Paul Ngussa wa basi lenye namba za usajili T 810 BDW aina ya
Scania linalotoka Bukoba kwenda Musoma, mali ya Kampuni ya Bunda Express.