MASIKINI MENEJA WA MSANII DIAMOND,SASA ANASAKWA KWA UDI NA UVUMBA NA MAHAKAMA,SOMA HAPO KUJUA
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa hati ya
kukamatwa kwa Hamis Tale ‘Babu Tale,’ ambaye ni meneja wa mwanamuziki wa bongo
fleva, Diamond Platnumz, anaandika Faki Sosi.
Mahakama imetoa hati hiyo
kutokana na Babu Tale kutotii amri ya mahakama iliyomtaka amlipe Shekhe Hamis
Mbonde Sh. 250 milioni.
Babu
Tale anatakiwa alipe fedha hizo kutokana na kuvunja mkataba kati yake na Shekhe
Mbonde, kwa kuuza na kusambaza nakala za mawaidha (DVDs) bila ridhaa
ya shekhe huyo, jambo ambalo ni kinyume na haki miliki.
Kutokana
na Babu Tale na mwenzake Iddi Tale kushindwa kulipa fedha hizo kama
ilivyoamriwa tarehe 18, Februari mwaka huu, mahakama ilitoa hati ya
kukamatwa kwa wadaiwa hao tarehe 8 Julai mwaka huu.
Katika
hati hiyo, mahakama ilimuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda ya Ilala kuwa, hadi
leo tarehe 19 Julai mwaka huu awe amewakamata wadaiwa hao ili wafike mahakamani
kueleza kwanini wasipewe adhabu kwa kukiuka amri ya mahakama.
Shauri
hilo limetajwa tena leo mbele ya Juma Hassan, Kaimu Msajili wa Wilaya wa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo ametoa hati nyingine kumuelekeza
Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni kuwakamata wadaiwa hao.
Msajili
Juma ametoa hati hiyo baada ya Mwesigwa Muhingo, Wakili wa Shekhe Mbonde,
kuomba hati hiyo ipekwe Kinondoni kwa kuwa Babu Tale anaishi huko na si Wilaya
ya Ilala kama hali ya kwanza ilivyoeleza.
Tarehe
18 Februari mwaka huu, Jaji Augustine Shangwa, aliwaamuru wadaiwa kulipa Sh.
200 milioni kama fidia ya kuvunja haki miliki ya Shekhe Mbonde na Sh. 50
milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunja makubaliano.
Katika
uamuzi wake Jaji Shangwa amesema, Juni 16, 2013, Mbonde aliingia makubaliano na
wadaiwa hao na wenzake ya kufanya biashara ya kurekodi mawaidha na kutengeneza
nakala DVDs kwa ajili ya kuziuza nchini.
Wadaiwa
hao waliahidi kumjengea nyumba, kumnunulia gari na kuitangaza kazi yake pia
walimpa Sh milioni mbili na kumnunulia kanzu na kofia (baraghashia) na kurekodi
DVDs zenye ujumbe Uzito wa Kifo, Fitina Juu ya Wanawake, Umuhimu wa Swala,
Mwanadamu Yumo Ndani ya Hasara na Maadui wa Uislam.
Amesema,
makubaliano ya awali yalikuwa kurekodi halafu baadaye wakubaliane kuhusu bei na
jinsi ya kuziuza, badala yake waliziuza na kuzisambaza nakala hizo na kujipatia
faida bila kumshirikisha Mbonde ambaye alitumia ujuzi wake.
Mbonde
kupitia wakili wake Muhingo, Gwamaka Mwaikugile na Clement Kihoko,
alifungua kesi ya madai namba 185/2013 akiiomba mahakama iamuru wadaiwa
wamlipe Sh. 700 milioni kama fidia ya kuvunja makubaliano na Sh. 50
milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunjwa kwa makubaliano.