Zinazobamba

"CHAPOMBE" KITWANGA AFUNGUKA BAADAYA KUTOKA ISLAELI,SOMA HAPO KUJUA


ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema yupo imara na amerejea nchini akiwa na matumaini mapya.

Pamoja na hali hiyo, amesema kuwa hivi sasa anajipanga kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha anaisaidia nchi pamoja na wapigakura wake na kuwa na maendeleo ya kweli na Jumatano ya Julai 29, ataripoti bungeni.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana baada ya kurejea akitokea nchini Israel ambako alikwenda kwa shughuli zake binafsi.

Alisema licha ya mtihani uliomkuta, kwa sasa yupo imara kwa ajili ya kuwatumikia wapigakura wake kwa kuwawakilisha vema ndani ya Bunge.

“Niko imara kabisa na nina nguvu na matumaini mapya, nimeingia nchini jana (juzi) nikitokea nchini Israel ambako nilikuwa na shughuli zangu binafsi. Unajua mimi ni mtaalamu (wa mawasiliano) na wewe unajua kabla sijaingia kwenye siasa nilikuwa nafanya nini.

“Kifupi ninasema nilikwenda Israel kwa shughuli zangu binafsi kabisa ambazo kwa kipindi cha wiki tatu nilizokuwa huko nimefanya. Hata wanaosema nilikwenda kulia kwa Bwana nao ni mawazo yao, maana unajua ile ni nchi takatifu kutokana na historia yake,” alisema Kitwanga.

Alipoulizwa amepokeaje hatua ya kufutwa kwake kazi na Rais John Magufuli kwa kile kilichoelezwa ni ulevi, alisema kwa sasa hawezi kusemea jambo hilo kwani aliyemteua ndiye mwenye mamlaka ya kumwajibisha.

“Rais ni mtu mkubwa anaweza kufanya jambo lolote ili mradi havunji sheria, hata kilichotokea kwangu ni mamlaka yake halali, ingawa Mungu ndiye muweza wa kila jambo. Mimi ni Mkristo safi, nasi tumefundishwa kusamehe saba mara sabini na kusahau yaliyopita,” alisema.

Akieleza mikakati yake, Kitwanga alisema kuwa baada ya kuripoti bungeni wiki ijayo, atakuwa na ziara ya wiki tano ndani ya jimbo lake ambako atazungumza na wapigakura wake na kueleza yaliyomsibu hatua kwa hatua.

“Sitaki kuingia ndani sana ila mengine nitayasema nikiwa jimboni, lakini si kwa lengo la kubishana na mtu, na uzuri kila hatua ambayo nimepitia hata wapigakura wangu walikuwepo kwa uwakilishi wa madiwani wa Misungwi ambao walikuwa mjini Dodoma,” alisema.

Mei 21, mwaka huu, Rais Magufuli alimng’oa Kitwanga kuhudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na madai ya ulevi, huku taarifa zaidi za ndani zikieleza kuwa alianza kushughulikiwa bila yeye mwenyewe kujua.

Hakuna maoni