Zinazobamba

UGONJWA WA SICKLE CELL WAIVURUGA SERIKALI,SOMA HAPO KUJUA

Pichani ni Yasmini Razak, mzazi wa Ronald Massamba ambaye anasumbuliwa na selimundu leo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)



BAADA ya kusitishwa utolewaji huduma ya bure kwa wagonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kumetokea mvutano baina ya wazazi wa wagonjwa na uongozi wa hospitali hiyo, anaandika Regina Mkonde.

Mvutano huo umechipuka baada ya Shirika la Trust Fund la nchini Uingereza kumaliza mkataba wake wa mradi wa utafiti kwa watu wenye ugonjwa wa selimundu nchini mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu na kwamba, mradi huo ulisaidia

wagonjwa hao kupata matibabu bure kwa kipindi cha miaka 10.
Wakizungumza kwa wakati tofauti leo, viongozi wa MNH na wazazi wa wagonjwa wametoa kauli za mvutano ambapo wazazi wanataka huduma hiyo iendelee kutolewa bure huku uongozi wa MNH ukisema kuwa, muda wa utolewaji huduma hiyo bure umeisha hivyo huduma hiyo ni ya malipo.

Akizungumza na waandishi wa habari Yasmini Razak, mzazi wa Ronald Massamba ambaye anasumbuliwa na selimundu leo jijini Dar es Salaam amesema, baada ya kusitishwa utolewaji huduma bure kwa wagonjwa, alifanya jitihada za kuomba msaada kwa baadhi ya viongozi wa serikali ili huduma hiyo itolewe bure bila ya kufanikiwa.

“Nilipokwenda Muhimbili kwa lengo la kumpeleka mwanangu kliniki, nikakuta huduma inayotolewa ni ya malipo huku baadhi ya wazazi wenye wagonjwa wakilalamika juu ya gharama wanazotozwa. Wengi wao hawakuwa na uwezo wa kulipia gharama hizo,” amesema.
Anaeleza, aliamua kumtafuta Lawrence Museru, Mkurugenzi wa MNH baada ya kukosa ushirikiano wake akamtafuta Grace Magembe, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kukosa msaada ndipo alipoamua kumtafuta Hamisi
Kigwangalla, Naibu Waziri wa Afya ambaye pia alimuahidi kumsaidia ambapo mpaka sasa hajapata msaada huo.
Razak amesema, serikali haina budi kuchukua hatua mapema kusaidia wagonjwa wa selimundu ili kunusuru maisha yao kutokana na kwamba, Tanzania inashika nafasi ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wenye selimundu.
Baada ya wazazi hao kuongea na waandishi wa habari leo, MNH na Wizara ya Afya imetoa ufafanuzi juu ya usitishwaji huduma hiyo ambapo imewataka wagonjwa kufuata utaratibu wa uhamisho ili wakapate huduma katika hospitali zilizopo karibu yao.
MNH kupitia Museru imesema kuwa, wagonjwa waliokuwa wanatibiwa hospitalini hapo kurudi kwenye hospitali za mikoa na kwa wale ambao wako katika hatari wanaruhusiwa kutubiwa Muhimbili baada ya kupata barua za rufaa.
“Muhimbili huduma bado ipo, haijasitishwa kama inavyosemwa na baadhi ya watu, iliyositishwa ni huduma ya bure,  wagonjwa watakaopata rufaa ya kutibiwa hapa watachangia huduma kama ilivyo kwa wagonjwa wengine,” amesema.
Magembe amesema, wagonjwa walidhani kuwa huduma hiyo inatolewa na Muhimbili pekee na kuwa, hospitali zilizokaribu nao kuna kliniki za wagonjwa waselimundu.
Dorothy Gwajima, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Tiba Wizara ya Afya amesema, tangu awali huduma za wagonjwa wa waselimundu zilikuwa zinalipiwa na kuongeza kuwa, kama kutakuwa na mgonjwa asiyekuwa na uwezo anaruhusiwa kuomba msaada kupitia dawati la utawi wa jamii.



Hakuna maoni