ZANZIBAR YAANZA TARATIBU,MSIKITI WAVAMIWA NA KUBOMOLEWA,SOMA HAPO KUJUA
Watu wasiojulikana wamevamia katika makazi ya watu eneo la Msumbiji mjini Unguja na kuvunja mabanda na msikiti.
Watu hao maarufu kama mazombi, walifanya uhalifu huo usiku wa kuamkia jana, ambapo walivamia eneo hilo wakiwa wamejifunika nyuso zao na soksi maalumu, huku wakiwa na silaha za jadi.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, amesema kuwa watu hao walivamia eneo hilo saa 10 alfajiri.
Alisema watu hao baada ya kufika katika eneo hilo ambalo linadaiwa kukusanya mashabiki wa vyama vya upinzani, walianza kuvunja mabanda ya mafundi seremala.
“Lilikuwa kundi la watu, tena wote ni mazombi, wakiwa na silaha za moto pamoja na zile za kijadi kama mapanga, marungu, mikuki na mashoka.
“Wamefanya uharibifu mkubwa wa mali zetu yakiwamo mabanda ya mbao, msikiti wa mabati wa hapa Msumbiji ambao tumekuwa tukiutumia kama msikiti wa muda wakati huu wa kisasa ukiendelea kujengwa.
“Vurugu hizi wamefanya zimekuwa kubwa sana na uharibifu, huu kwa kweli ni uonevu wa hali ya juu, wameharibu mabanda karibu yote kama unavyoona na mengine ya biashara yaliyopo kando ya barabara hadi kufikia eneo la mabati,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi lipo katika uchunguzi.
“Tumepata taarifa za tukio la kuvunja vibanda katika eneo la Msumbiji na Jeshi la Polisi tumeanza msako wa kuwabaini watu waliohusika na tukio hili, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kamanda Mukadam.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni