Zinazobamba

UCHAGUZI MARUDIO NI KUVUNJA KATIBA

Waziri wa nchi, ofisi ya rais -Tawala za mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi) Mh. George B. Simbachawene akizungumza na wanahabari.

KUAHIRISHWA kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kumevikera vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na sasa vinaelekeza tuhuma zao katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Anaandika Faki Sosi.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni miongoni mwa Ukawa kinaeleza kuwa, Tamisemi inatumika kuvuruga uchaguzi huo kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Uchaguzi huo haujapangwa tarehe ya kufanyika baada ya kuahirishwa kwa mara ya pili.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye Makao Makuu ya Chadema, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu amesema uvurugwaji huo pia unamuhusu Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania ambaye Tamisemi ipo kwenye ofisi yake.
Pia Mwalimu amemtuhumu Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene kuwa, yeye na CCM wanalazimisha kuwepo kwa majina ya wajumbe ambao hawana sifa ya kuwa wapiga kura kwenye uchaguzi wa meya.
“Wakurugenzi wa halmashauri ya Ilala na Kinondoni wanatutia mashaka kwa kuongeza wajumbe wasiokuwa halali kupiga kura ya uchaguzi wa meya wa jiji.
“Mwanzo kulikuwa na wajumbe 54 Ilala lakini sasa hivi tumeletewa majina ya wajumbe 57 huku watatu wakiwa wameongezwa kinyume cha taratibu.
“Kinondoni mwanzo kulikuwa na majina 58 lakini sasa hivi yameletwa majina 69 hivyo wameongeza watu 11,” amesema Mwalimu.
Mwalimu anaeleza kwamba kuna kila dalili za kuvuruga uchaguzi huo na kuwa wakurugenzi wa Halmashauri ya Ilala na Kinondoni ndio wanaosimamia uvurugaji huo.
Amewataja baadhi ya wajumbe haramu kwenye uchaguzi huo kuwa Restistuta Mbogo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kwenye Jimbo la Katavi na Monde Tambwe ambaye ni Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tabora na kwamba, wajumbe wengine wanatokea Zanzibar.
Pia amesema Chadema ilipeleka wajumbe wao ambao wanaishi ndani ya Halmashauri ya Kinondoni na Ilala lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wamewakataa wajumbe hao.
“Mmoja anatoka Tanga na tukamuhamishia hapa Dar es Salaam ili kusaidia na wawakilishi wetu hapa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye jiji hili, lakini NEC imetugomea. Hapa haki inatoka wapi?” anahoji.
Habari hii kwahisani ya Mwanahalisi oline

Hakuna maoni