MUFTI WA TANZANIA ALAZWA
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MUFTI wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir Bin Ali, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Awali MTANZANIA lilipata taarifa kuwa Mufti angefikishwa hospitalini
hapo saa 10 jioni na kulazwa katika jengo la Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI).
Mwandishi wa habari hii alifika hospitalini hapo na kwenda moja kwa
moja katika jengo hilo ambako mmoja wa madaktari wa zamu ambaye hakutaka
jina lake liandikwe gazetini alithibitisha taarifa za kulazwa kwa
Sheikh Mkuu.
“Tumepokea taarifa hiyo ya kuja kulazwa Mufti kwa ajili ya matibabu
na tayari tumeandaa mahali pa kumlaza lakini bado hatujampokea.
“Ili aje kwetu lazima apitie kwanza kwa wenzetu wa emergence (kitengo
cha wagonjwa wa dharura) halafu daktari wetu ataenda kumuona ndipo
atahamishiwa huku JKCI,” alisema.
Kutokana na majibu hayo, mwandishi alikwenda kupiga kambi katika
eneo la wagonjwa wa dharura ambako baadaye alimshuhudia Mufti Zuberi
akiwa ameongozana na baadhi ya ndugu na waumini wa dini ya Kiislamu.
Alipotafutwa, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Neema
Mwangomo hakupatikana katika simu zake wala ofisini kwa kuwa alikuwa
katika mapumziko ya mwisho wa wiki.
Mtanzania
Hakuna maoni
Chapisha Maoni