SIKU 100 ZA MAGUFULI,WASOMI,MASHEIKH NA MAASKOFU WAZISHAMBULIA,UBAKAJI WA DEMOKRASIA ZANZIBAR WATAJWA,SOMA HAPO KUJUA
MKWAMO wa kisiasa visiwani Zanzibar umetia najisi
sifa na mafanikio ya Rais John Magufuli katika siku 100 alizokuwepo madarakani
zinazofikia kesho tangu aapishwe tarehe 5 Novemba mwaka jana,anaandika
Faki Sosi.
Waliotoa maoni yao kwa Chanzo changu wametofautiana
mtazamo kuhusu siku 100 za Rais Magufuli madarakani huku wengine wakisema
ameshindwa kufikia maratajio ya wengi hususani utatuzi wa mgogoro wa kisiasa
visiwani Zanzibar.
Alhad Mussa, Sheikh Mkuu wa MKoa wa Dar es Salaam
amesema kuwa siku 100 za Rais Magufuli ni za baraka na neema kwa Watanzania na
kwamba zimetoa nuru na heshima kubwa kwenye serikali yake.
Amesema, ameokoa kiasi kikubwa cha fedha na kwamba
Watanzania watafurahia keki ya Taifa ambapo ameshauri wananchi kushikamana na
kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu.’
“Kauli mbiu hii imeridhiwa na Mungu kwani Mungu
aliumba mbingu na ardhi kwa kuashiria kuwa kazi ni wajibu,” amesema Sheikh
Alhad.
Kwa upande wake Profesa Abdall Sharrif ambaye ni
Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar (BAKIZA) amesema, katika siku 100 za
Rais Magufuli hakufanya cha ajabu.
Amesema siku hizo 100 za Rais Magufuli ni kama
amekuja kusalimu na kusimamisha watu kazi huku akikwepa nafasi yake ya kutatua
mgogoro wa Zanzibar kwa kudai hana mamlaka wakati vurugu zitakapozuka, atatumia
majeshi yake kwenda kuzizima.
“Majeshi ya Jamhuri ya Muungano ndio yaliyoua
Wazanzibari mwaka 2001 na hayo hayo yanaweza kutumika tena kufanya kile
kilichofanywa mwaka huo,” amesema.
Prof. Sharifu amemsifu Ibrahimu Kaduma ambaye ni
kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa mkweli na kujitokeza mbele ya umma.
Amesema kuwa, hatua ya Kaduma kusema kwamba chama
chake (CCM) kimeshindwa na kiwaachie walioshinda ni ujasiri ambao alipaswa kuwa
nao Rais Magufuli na ingeleta tija kwa taifa.
Sheikh Ponda Issa Ponda ambaye ni Katibu Mkuu wa
Jumuiya na Taasisi za Kislamu nchini amesema kuwa, Rais Magufuli ameonesha nia
ya kutaka uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
Amesema, pamoja na hivyo lakini ameshindwa kusimamia
utatuzi wa mgogoro wa kisiasa unaondelea Zanzibar na kwamba, visiwani humo
kumetokea uvunjifu wa katiba uliofanywa na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa
ZEC.
Sheikh Ponda amesema kuwa, kiongozi huyo ameunda
Baraza la Mawaziri bila kuzingatia usawa wa dini na kwamba, kwenye baraza hilo
kuna mawaziri wanane tu ambao ni Waislamu.
Amesema kuwa, Rais Magufuli hatakiwi kusikiliza
ushauri wenye ukada ndani yake kwani wanaCCM wengi hawana uzalendo na nchi.
Sheikh Ponda amemtaja Benard Membe ambaye alikuwa
Waziri Mambo ya Nje katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwa, alimshauri
Rais Magufuli njia sahihi ya kutatua mgogoro wa Zanzibar.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza amesema kuwa, Rais
Magufuli anafukia shimo kwa kuchimba shimo lingine kutokana na kushindwa kupata
ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzaibar.
Amesema kwamba, mgogoro huo hauwezi kutatuliwa kwa
kutumia majeshi wala silaha za moto pia kurudia uchaguzi isipokuwa maafikiano.
“Kuvurukiga kwa uchaguzi wa Zanzibar sio suala geni
na kwamba kwanini chaguzi za nyuma hazijarudiwa,”amehoji Askofu Bagonza huku
akionesha kushangazwa na Rais Magufuli kushindwa kupata ufumbuzi wa mgogoro huo
mpaka sasa.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni