MZIMU WA GAZETI LA MAWIO WAZIDI ITESA SERIKALI YA MAGUFULI,WANAHARAKATI WA THRDC WALILIA,SOMA HAPO KUJUA
Sura ya gazeti la mwisho la Mawio kabla ya kufungiwa |
GAZETI la MAWIO bado linapiganiwa, Onesmo
Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC)
anaeleza kwamba, kuna kila sababu ya kulifungulia ili liendelee na kazi yake
nzuri kwa taifa, anaandika Happyness Lidwino.
Anasema, hatua ya serikali
kulifungia gazeti hilo imekiuka kipengele cha 19 cha Mkataba wa Kimataifa wa
Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) pia kipengele cha 18 cha Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambacho kinatoa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.
Olengurumwa
ametoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es kuhusu hali ya
wanahabari na uhuru wa habari Tanzania.
Serikali
kupitia Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ililifungia
gazeti la MAWIO tarehe 15 Januari mwaka huu kwa madai ya kuandika habari za
uchochezi.
Olengurumwa
ameiomba serikali kuangalia upya uamuzi huo na kwamba adhabu iliyotoa haiendani
sambamba na kile kinachoelezwa kuwa kosa.
Mratibu
huyo amesema kuwa, serikali inaweza kulifungulia gazeti hili na hata kulipa
adhabu nyingine ndogo sambamba na kuhakikisha Sheria ya Vyombo vya Habari na
Sheria ya Haki ya kupata taarifa, inatengenezwa kwa muundo ambao unazingatia
mapendekezo ya wadau ili nchi iweze kuwa sheria inayozingatia viwango vya
Kimataifa.
Ametumia
nafasi hiyo kuviomba vyombo vya habari kushirikiana na mtandao huo ili kutafuta
mbinu zitakazosaidia kuipinga sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo
inakandamiza tasnia ya habari nchini.
Olengurumwa
amesema, wao kama mtandao wamebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu
ikiwemo uhuru wa kupata habari kutokana na sheria ya magazeti ya mwaka 1976
ambayo inakiuka uhuru wa habari na kupata taarifa nchini.
“Kwanza
tunampongeza Rais wetu John Magufuli kwa juhudi za kupambana na rushwa na
kupambana na matumizi holela ya mali za dhuluma, lakini katika siku hizo 100 za
utendaji wake, kama mtandao tumebaini mapungufu mbalimbali ambayo yanakiuka
haki za binadamu,” amesema Olengurumwa na kuongeza;
“Tunaona
mambo kadhaa kama suala la uhuru wa habari kuendelea kukandamizwa, mambo ya
demokrasia na utawala bora likiwemo suala la Zanzibar kuchukua muda mrefu
katika kukamilisha mchakato wake, hivyo basi kama mtandao tunaomba vyombo vya
habari kuungana nasi katika kutafuta namna ya kuipinga sheria ya magazeti inayovunja
na kukiuka Uhuru.”
Amesema,
kwa miaka mingi Sheria ya Magazeti imekuwa ikiorodheshwa kama sheria inayokiuka
uhuru wa kujitosheleza kutokana na kumpa waziri mwenye dhamana nguvu kubwa
kutoa maamuzi.
“Sheria
hii kwanza ilirithiwa kutoka katika uongozi wa Mkoloni na ilitengenezwa kwa
kusudio la kukandamiza sauti ya watawaliwa, tunaiomba serikali kuchukua hatua
za haraka za kurekebisha vifungu vinavyopinga uhuru ama la sheria iangaliwe
upya,” amesema.
Akitolea
mfano wa gazeti la Mwanahalisi, Mwananchi na Mtanzania ambayo yalisitishwa kwa
muda, na sasa gazeti la MAWIO lililofutwa kutokana na taarifa waliyoichapisha
ikilalamikiwa kuwa ni ya kichochezi, Mratibu huyo amesema, suala hilo
limeonesha kuwa sheria hiyo imeendelea kutumika vibaya.
Amesema,
kwa kuzingatia sheria na vigezo vya kimataifa, ufutwaji wa gazeti la MAWIO
umekiuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na katiba ya nchi.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni