MRADI WA VITAMBULISHO VYA NIDA NI UTATA,MILIONI 179 ZAYEYUKA,SOMA HAPO KUJUA
Wingu zito limetanda ndani ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuhusu matumizi ya Sh bilioni 179.6 ambako kila kitambulisho cha taifa kimegharimu Sh 89,800 zikiwamo gharama za utawala
Hayo yamebainika siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kushangazwa na watendaji wa mamlaka hiyo ikizingatiwa vitambulisho vilivyokwisha kutengenezwa hadi sasa havifiki milioni mbili na havina saini.
“Utaona ugumu wa kuongoza, nchi inatawaliwa na madudu ya kila aina. Wapo watu wanacheza na fedha wanavyotaka wakati wapo watu masikini sana wengine wanataka bodi zao wakakae Ulaya.
“Hapo ndipo tulipofikia, wengine wanalipwa mshahara wa Sh milioni 35 kwa mwezi…naomba mniombee kabla ya kunihukumu, toeni hukumu kwa haki kwa hawa wanaotaka kuifikisha nchi pabaya, toeni hukumu zao haraka,” alisema.
Rais Dk. Magufuli, licha ya kushangazwa na hali hiyo, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipewa Sh bilioni 70 lakini iliweza kutengeneza vitambulisho 23,253,982 ambavyo vilikuwa na saini ya kila mpiga kura na kila kimoja kimegharimu Sh 3,010.
Kutokana na hali hiyo, tofauti ya gharama kati ya kitambulisho kimoja cha NIDA na cha NEC ni Sh 86,790.
Pamoja na hayo, hivi sasa Watanzania wanasuburi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad, kuhusu matumizi ya fedha hizo za NIDA.
Januari 26 mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu.
Maimu alisimamishwa kazi pamoja na maofisa wengine wanne, kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alisema taarifa zilizomfikia Rais zinaonyesha kuwa NIDA hadi wakati huo ilikuwa imetumia Sh bilioni 179.6, kiasi ambacho ni kikubwa.
Alisema Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi kujua jinsi fedha hizo zilivyotumika, maana amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Licha ya kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, afanye ukaguzi maalumu wa hesabu za NIDA ukiwamo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa, pia aliitaka Takukuru ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.
Credit: Mtanzania
Hakuna maoni
Chapisha Maoni