Zinazobamba

SAKATA LA DC MAKONDA KUTUKANWA NA KUBENEA: MAHAKAMA YASIKILIZA UTETEZI WA MAKONDA


Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (katikati) akiwa na mawakili wake na wafuasi wa Chadema mara baada ya kutoka mahakamani
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (katikati) akiwa na mawakili wake na wafuasi wa Chadema mara baada ya kutoka mahakamani

PAUL Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, amebanwa kwa maswali kutoka kwa Wakili Peter Kibatara anayemtetea mteja wake Saed Kubenea. Anaandika Happyness Lidwino.

Makonda amebanwa kwa maswali na wakili huyo kutokana na ushahidi alioeleza mbele ya mahakama kuhusu kesi yake ya madai aliyoifungua tarehe 15 Desemba mwaka jana dhidi ya Kubenea ambaye ni Mbunge wa Ubungo.

Ikiwa ni siku ya Makonda kujitetea, Wakili Kibatara alimuhoji kwanini aliamua kupeleka kesi hii mahakamani?, Makonda alishindwa kujibu.

Baada ya Makonda kushindwa kujibu, hakimu anayesimamia kesi hiyo Thomas Simba alimweleza Wakili Kibatara aulize swali la pili.

Wakili Kibatara alimuuliza Makonda kwamba alichukua muda gani kwenda katika gari yake baada ya Kubenea kuanza kumtolewa lugha za matusi?

Makonda aliieleza mahakama kwamba, alitumia muda wa dakika 15, Wakili Kibarata alimuhoji kwamba, je katika dakika hizo hakujibu matusi kutoka kwa Kubenea?

Makonda alijibu kwamba, katika muda huo hakumjibu chochote Kubenea. Wakili Kibatara alihoji kwamba inawezekanaje katika dakika zote 15 Makonda asizungumze chochote.
Hata hivyo, hakimu alimtaka Wakili Kibatara kuuliza swali lingine ambapo aliuliza je polisi waliokuwa katika eneo la tukio walichukua hatua gani?

Makonda alisema, polisi walichukua hatua ya kumkamata Kubenea baada ya Kubenea kuendelea kutoalugha ya matusi.
Na hata alipoulizwa aliyetoa amri ya kumkamata Kubenea, Makonda alikana na kudai si yeye isipokuwa polisi ndio walimkamata.

Wakili Kibatara alimuuliza Makonda, “Je, unayajua majukumu ya Mbunge? Je ulijibizana na Kubenea eneo la tukio? Je, unajua ni vigezo gani vilitumika kukuchagua kuwa Mkuu wa Wilaya? Je unafahamu maana ya neno mjinga na mpumbavu?

Maswali hayo ya mtego yalionekana kumpandisha hasira Makonda kutokana na majibu yake kuwa mafupi na kutomridhisha wakili.
Hata hivyo, hakimu aliingilia kati na kumtaka wakili kubadilisha namna ya kuuliza maswali hayo. Hata Wakili Kibatara baada ya kushauriwa na hakimu kubadilisha maswali, aliieleza mahakama kwamba amemaliza.

Makonda alifika mahakamani hapo leo kutoa ushahidi wake huku akifuatiwa na shaidi wake ambaye ni Askali Dc Gabriel mwenye namba F4829 kutoka katika Kituo cha Magomeni.

Makonda alifungua kesi hiyo tarehe 15 Desemba mwaka jana ikiwa ni siku moja baada ya Makonda kuagiza askari wa Jeshi la Polisi kumkamata mbunge huyo kwa madai ya kushindwa kutii agizo lake kama Mkuu wa Wilaya.

Tukio la kukamatwa Kubenea lilitekelezwa Tarehe 14 Desemba mwaka jana jijini Dar es Salaam, baada ya viongozi hao kukutana katika mgogoro wa wafanyakazi wa Kiwanda cha nguo cha Tooku Tanzania.

Kwenye mahakama hiyo, Makonda amefungua madai matatu dhidi ya Kubenea ambayo ni lugha ya matusi, kuitwa mpumbavu, mjinga pamoja na cheo cha kupewa.

Hakuna maoni