BIFU LA ZITTO KABWE NA SAED KUBENEA LAFIKIA PATAMU,KUBENEA AMJIBU ZITTO KWA MAKALA BOMBA SANA,ISOME HAPO
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe |
ZITTO Zuberi
Kabwe, kiongozi mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, ni ndumilakuwili. Ni
kigeugeu. Haaminiki. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).
Anataka kupanda farasi wawili kwa wakati
mmoja; lakini kwa barabara tofauti. Anasukumwa na maslahi binafsi.
Leo anaweza kusema hili, kesho akasema lile. Jana alisema hili;
lakini keshokutwa atasema tofauti na kile alichokieleza juzi, jana na leo.
Pamoja na tabia yake hii kujulikana kwa wengi, bado Zitto
anataka aaminike kwa umma.
Jumapili wiki hii, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema,
“mshindi halali wa uchaguzi wa 25 Oktoba, Tanzania Zanzibar atangazwe.”
Lakini kauli ya Zitto juu ya mgogoro wa kisiasa Visiwani,
aliitoa takribani mwezi mmoja tangu pale wabunge wa upinzani walipomtuhumu Dk.
Ali Mohammed Shein na John Pombe Magufuli, kuvunja Katiba.
Upinzani ulidai bungeni na unaendelea kusisitiza nje ya Bunge,
kwamba Dk. Shein siyo rais halali Visiwani. Naye Magufuli “ameingia Ikulu kwa
mlango wa nyuma.”
Kelele za wapinzani zilimsukuma Spika wa Bunge, Job Ndugai,
kuamuru wabunge wanaotetea Katiba, watolewe nje ya Bunge. Amri ya spika
ikatekelezwa.
Aidha, wiki mbili zilizopita, Zitto huyuhuyu alitoka hadharani
kumtetea Prof. Sospeter Muhongo, aliyeteuliwa kuwa waziri wa nishati na madini
katika serikali ya Magufuli.
Akiandika katika akaunti yake ya face book, Zitto alisema,
“waliosema ufisadi ni mfumo ndio wanasema leo Prof. Muhongo hafai kuwa waziri,
kwa sababu ya tuhuma za wizi wa fedha za umma katika akaunti ya Tegeta Escrow.”
Alihoji: “Sijui lini mahakama ilimhukumu Muhongo! Sijui lini
Muhongo kawa mfumo. Tujifunze kuweka akiba.”
Prof. Muhongo alikuwa waziri wa nishati na madini wakati wa
sakata la Tegeta Escrow.
Zitto anasema kamati ya Bunge ilipendekeza na Bunge likaazimia
kuwa Prof. Muhongo avuliwe madaraka yake ya uwaziri. Prof. Muhongo alijiuzulu.
“Akafanyiwa uchunguzi na Kamishna wa Maadili na kutamka kuwa
hakukutwa na kosa la kimaadili. Unajengaje hoja kuwa hana haki ya kuteuliwa
kuwa waziri?
“Kesha adhibiwa kwa kosa la awali, kwa kujiuzulu. Sheria ipi inasema
hana haki ya kuteuliwa tena?
“Niliongoza Kamati ya PAC. Nina uhakika waziri Muhongo kwenye
sakata lile alishauriwa vibaya na kujikuta anatetea ubadhirifu…
“Mwenye ushahidi dhidi ya Muhongo si aende mahakamani? Tuache
siasa za porojo porojo.” Tuanze kujadili:
Kwanza, undumilakuwili wa Zitto, haukuanza leo, jana wala juzi.
Alianza tabia hii wakati akiwa mwanachama katika Chama cha Demokrasia na
Maendeo (Chadema).
Hata kufukuzwa kwake ndani ya chama hicho, kulichangiwa na tabia
yake hiyo.
Ndani ya Chadema, ambako Zitto alifanikiwa kufikia cheo cha
naibu katibu na naibu kiongozi wa upinzani bungeni, alihubiri asiyoamini na
kuamini asichohubiri.
Kwa mfano, Zitto aliwahi kusema, yeye atakuwa mtu wa mwisho
kuhujumu Chadema. Lakini matendo yake yakawa tofauti na kile alichokuwa
akikinena.
Ndani ya Chadema, Zitto alikuwa akishirikiana na wanaokivuruga
chama. Wanaotuhumiwa kutaka kuangamiza maisha ya viongozi wakuu wa chama na
wanaotajwa kuwa maadui wa chama.
Amekuwa akitajwa kuhusika na njama za kutaka kuondoa viongozi
kinyume cha taratibu. Amekuwa akitajwa kuasisi matumizi ya rushwa kipindi cha
uchaguzi.
Anadaiwa kukubali kupokea fedha kutoka kwa maadui wa chama kwa
lengo la kukidhoofisha, huku akiuhadaa umma kuwa anakipenda chama hicho.
Alikituhumu chama anachodai kukijenga – nje ya vikao – kusheheni
ukabila na udini. Akawa anatolea mfano wa mchakato wa kuwapata wabunge wa Viti
Maalum mwaka 2005, ambapo alisema wengi walitoka mkoa wa Kilimanjaro.
Lakini ni yeye aliyekuwa Katibu wa Kamati ya kutafuta wabunge wa
Viti Maalum. Kama kuna makosa yalifanyika, yeye ndiye alikuwa mhusika mkuu.
Asingeweza kujivua tuhuma hizo.
Kama kuna upendeleo, basi ndiye aliyehusishwa zaidi kwa
kuhakikisha anampitisha dada yake, Mhonga Saidi.
Katika kipindi chake chote cha kuwa naibu katibu mkuu na mbunge,
Zitto hakukisaidia Chadema mkoani Kigoma bali alitumia Chadema kujijenga
binafsi.
Pili, Zitto Zuberi Kabwe, anayedai kuguswa na kilichotokea
katika uchaguzi wa 25 Oktoba, Unguja na Pemba, hakuwa miongoni mwa wabunge
waliopinga uvunjifu wa katiba bungeni.
Hakuwa miongoni mwa waliosimama kupigia kelele wanaovunja
katiba. Alibaki kimya. Alishirikiana na wanaovunja katiba. Akaungana na
wanaomshangilia Dk. Shein. Akamwagiwa sifa na Magufuli.
Alipohojiwa na waandishi wa habari, Zitto alibeza waliotoka nje
ya Bunge. Akawaita wabinafsi.Wanasiasa uchwala.
Akiwa nje ya Bunge na kubaini jinsi upepo wa kisiasa kuhusu
Zanzibar unavyovuma kwa mashinikizo ya mabalozi na jumuiya za kimataifa, Zitto
amegeuka nyuzi 180 kutoka alipokuwa awali. Anazungumza lugha moja na
waliotolewa bungeni.
Tatu, hata utetezi dhidi ya Prof. Muhongo umefuata njia
hiyohiyo. Ni kujikomba. Anategemea huruma ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili
kimsaidie aweze kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya
Umma (PAC).
Zitto anayedai kuwa Prof. Muhongo hana kosa, kamati ambayo yeye
aliiongoza ilimtuhumu Prof. Muhongo kuwa dalali katika wizi wa fedha ndani ya
akaunti ya Tegeta Escrow.
Taarifa ya PAC inaeleza katika ukurasa wa 58, kwamba “Prof.
Muhongo ndiye aliyekuwa Dalali Mkuu aliyewakutanisha Bw. Harbinder Sethi na Bw.
James Rugemalira.”
Sethi ndiye alijiita mmiliki mpya wa kampuni ya Independent
Power Tanzania Limited (IPTL). Rugemalila alikuwa mmiliki wa kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Limited, iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa
katika IPTL.
Katika mkataba kati ya serikali na IPTL, serikali kupitia
Tanesco, ndiyo ilikuwa ikilipia gharama za matengenezo ya mitambo na gharama
nyingine za ufundi ikiwamo ununuzi wa vipuri.
Tanesco ndiyo ilikuwa ikinunua mafuta kwa ajili ya kuendeshea
mitambo ya IPTL na kisha kampuni hiyo kuiuzia Tanesco umeme inaogharamia
kuuzalisha, tena kwa bei kubwa mno.
Ilikubaliwa kuwa mara baada ya mkataba kumalizika, mitambo hiyo
ingekuwa mali ya serikali.
Hata hivyo, wakati mkataba unakaribia kufika mwisho ili mitambo
ikabidhiwe kwa Tanesco, Prof. Muhongo akaruhusu kampuni ya IPTL kuuzwa kwa
mwekezaji mwingine.
Akaagiza Tanesco wajifunge katika mkataba mwingine wa miaka
mitano wa kununua umeme kwa muwekezaji mpya.
Hapa ndipo hasa kwenye ufisadi. Kwamba mitambo ambayo tayari
ilikuwa iwe mali ya Tanesco, haiwezi tena kurudi mikononi mwa umma.
Ni kwa sababu, Prof. Muhongo ameruhusu kuuzwa kwa mkataba,
kinyume na makubaliano ya awali ya mkataba huo. Huyu ndiye anayetetewa na
Zitto.
Hatua ya serikali kukubali kujifunga katika mkataba na kampuni
mpya, ni kielelezo tosha kuwa kuna wizi umefanyika.
Aidha, ndani ya Bunge, Prof. Muhongo alipatikana na hatia ya
kuvunja kifungu cha 29 cha sheria ya fedha ya mwaka 2012.
Kifungu kinamtaka waziri husika, kuthibitisha uuzaji wa hisa,
pale makampuni mawili au matatu yanapoamua kuuza hisa zao.
Prof. Muhongo hakufanya hivyo. Yawezekana alijua kuwa nyaraka
zilizowasilishwa kwa Wakala wa serikali wa Usajili wa Biashara (BRELA),
hazikuwa halali. Zilighushiwa.
Akizungumza kwa sauti ya jeuri, Prof. Muhongo alisema, suala la
uhalali wa umiliki wa hisa katika kampuni hizo linahusu wanahisa wenyewe.
Serikali haiwajibiki kuingilia mahusiano ya kibiashara ya wanahisa katika kampuni
binafsi.
Kitendo cha Prof. Muhongo kushindwa kutimiza wajibu wake, jambo
ambalo lilisababisha nyaraka feki kutumika kuhadaa ulimwengu, ndiyo chanzo cha
wizi huu.
Zitto anajua yote haya. Anajua kuwa Prof. Muhongo hakuwajibika
kisiasa kama anavyodai. Alifukuzwa uwaziri na Bunge kwa kuvunja sheria.
Alituhumiwa kukodisha watu kusambaza uongo bungeni ili
kujitakasa. Akatumia fedha za umma kuchapisha na kusambaza nyaraka za uongo kwa
wabunge ili kulinda kitumbua chake.
Haingii akilini kwa mtu anayejua ukweli huu, kutetea uhalifu,
bila kuwa na ndimi mbili; na bila kutegemea kupata faida au manufaa mengine ya
kisiasa na kiuchumi.
Hata kauli ya Zitto kuwa Kamati ya Maadili ya Ikulu, imemsafisha
Prof. Muhongo, nayo haina mashiko. Inadhalilisha wananchi na ina vimelea vya
hongo. Sababu ni hizi:
Kamati ya maadili ya Ikulu, yenyewe ni mtuhumiwa wa ufisadi wa
wizi katika akaunti ya Escrow. Haiwezi kumsafisha mtuhumiwa na wananchi
wakakubaliana na utakaso huo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Ikulu, wametajwa katika orodha ya
wanufaika; na kuna madai kwamba fedha zilichotwa kwa amri ya rais.
Aliyekuwa rais wa Jamhuri wakati huo, Jakaya Kikwete, alionekana
kuanzia sura yake, maneno yake na kauli zake, kuwa mmoja wa wanufuikaji wa
fedha za wizi.
Mpaka kesho, Kikwete anasumbuliwa na dhambi hii – moyoni,
akilini na hadharani. Anashindwa kuficha ushiriki wake yeye na familia yake
katika kashfa hii kubwa.
Aidha, mpaka Zitto anamsafisha Prof. Muhongo, umma haujaelezwa
majina ya waliokwapua mabilioni ya shilingi kupitia benki ya Stanbic, tawi la
Tanzania.
Kauli kwamba kuna fedha za umma zilizokuwa zimehifadhiwa BoT
zimekwapuliwa Stanbic, ilitolewa kwa mara ya kwanza na Zitto.
Alisema, kuna watu wamegawana mabilioni ya shilingi ya Escrow
kutoka ndani ya benki hiyo, kwa kutumia masanduku na mifuko ya plastiki.
Vilevile, kauli ya Zitto ya kumtetea Prof. Muhongo, sharti
ipingwe na kulaaniwa na kila mmoja, kwa kuwa imesheheni dharau kwa umma na
Bunge.
Hii ni kwa sababu, kauli ya kutaka wananchi wenye ushahidi
kuwasilisha malalamiko yao mahakamani, ni kauli zinazolenga kutetea uhalifu.
Mara kadhaa, wananchi wamezoea kuzisikia kauli hizo kutoka
midomoni mwa wezi na watuhumiwa wa ufisadi nchini.
Nani asiyejua kuwa ili uende mahakamani kushitaki ni lazima uwe
mwathirika wa moja kwa moja wa tendo unalolilalamikia – Locus standi.
Ushahidi wa hili, ni kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco. Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kiligonga mwamba mahakamani pale kilipotaka
kuzuia malipo ya fedha za umma zilizokuwa zikidaiwa na kampuni hiyo.
Zitto hafanyi kwa bahati mbaya. Anakusudia. Ana lengo analotaka
kutimiza. Anataka kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya PAC.
Anategemea kuungwa mkono na wabunge wa CCM. Kamati hii ndilo
duka la wengi waliojizolea mabilioni ya shilingi kwa ulaghai mkubwa.
Katika hili la kutaka kuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge, Zitto
yuko tayari hata kusujudia wachafu. Tusubiri kuona mengine.
Maoni 1
Mimi huwa naliona tatizo moja kwa wanasiasa wa nchi yetu wengi ni wanafiki na wanao ogopa kusema kweli kwa kuchelea upwekwe, wewe SAID KUBENEA huwezi kujifananisha na ZITTO KABWE hata kidogo hususan kwenye masuala ya siasa na uchumi utamzidi tu kwenye fani yako ya uandishi wa habari, KIKUBWA nachokiona kwako ni kuwa unatumia fursa ya uandishi na umiliki wako wa vyombo vya habari kupambana na wanasiasa maarufu ukiwa na malengo tofauti kwanza kujitafutia umaarufu, pili kuongeza mauzo ya gazeti lako kwa kuwa taarifa unazoandika ambazo mwenyewe unaziita za uchunguzi ndizo zinazopendwa na wananchi wengi ambao si weledi wa masuala ya siasa bali ni washabiki tu na tatu unatumiwa na matajiri/mabepari wanaohodhi na kumiliki CHADEMA kama vile ni SACCOS au VICOBA na sio chama cha SIASA, ZITTO na hata DR SLAA wanaijua CHADEMA nnje ndani kama ww unavyomjua mke wako, ila TATIZO la chadema ni uwezo na upeo mdogo wa mbowe kielimu, weledi, na utashi hivyo ile dhana ya akili ndogo kuongoza akili kubwa iko ndani ya CHADEMA, ila kwa kuwa MBOWE ni bepari anamiliki uchumi ndio mana anaweza kupambana na yeyote katika CHADEMA. Kwa mfano baada ya ugomvi wako na DC MAKONDA japo hata mm nakubali yule bwana mdogo MAKONDA ana matatizo ila ulitumia vibaya taaluma yako ya uandishi wa habari na umiliki wa vyombo vya habari kuweka picha ambayo unadai ni ya MAKONDA akimfunga viatu RIDHIWANI lakini baadae ikaonekana picha ile sio ya MAKONDA sasa hizo habari unazuita ni za uchunguzi huwa unafanya uchunguzi kweli au blaa blaa! unatumika sana na unaharibu reputation yako!
Chapisha Maoni