Zinazobamba

WAFANYABIASHARA SOKO LA MWANANYAMALA WAIOMBA SERIKALI KULIJENGA KISASA


Mwenyekiti wa Mfavesco Ltd Hassan Madika.

Na Mussa Augustine, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Ushirika wa Soko la Mwananyamala (MFAVESCO LTD), Hassan Madika, ameiomba Serikali kulijenga soko hilo ili liwe la kisasa kama yalivyo masoko mengine.

Akizungumza Aprili 23, 2026 na waandishi wa habari sokoni hapo, mwenyekiti huyo amebainisha kuwa soko hilo halina miundombinu ya kisasa hivyo linahitaji kuboreshwa ili liwe la kisasa.

Aidha, amesema kuwa soko hilo baada ya kuwa ushirika, Serikali imeboresha masoko mengi ya Manispaa ya Kinondoni huku Soko la Mwananyamala likiachwa, hivyo ameiomba Serikali kulijenga liwe la kisasa.

“Tunapatwa na changamoto kubwa ambayo sisi kama ushirika hatuwezi kulijenga hili soko, tunaweza kufanya hivyo endapo tutasaidiwa na Serikali au kupewa mkopo na Serikali,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa wao kama ushirika wameshakaa vikao na kuona kuna mambo mawili lazima yafanyike ili kuboresha soko hilo. Mambo hayo ni kupata mkopo Serikalini ambao wanaweza kuulipa au kujengewa na Serikali kwa makubaliano ya kufanya ushirika uendelee na Serikali kupata sehemu ya mapato yake.

“Changamoto kubwa iliyokuwepo awali ni ubovu wa barabara ya kuingia sokoni ambayo ilikuwa imechimbika na haikuwa na lami, lakini tunashukuru baada ya kuongea na Serikali barabara hii imeboreshwa na kuwekwa lami chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa sasa tunachomuomba ni kutujengea soko la kisasa,” amesema.

Na kuongeza kuwa ushirika unafanya huduma zote za soko ikiwemo kuondoa takataka, ulinzi wa soko, kulipa Manispaa kila mwezi, kulipa TRA kwa mwaka, na wafanyakazi wa soko akiwemo meneja pamoja na watu wa usafi.

Akizungumzia kuhusu kudhibiti majanga ya moto sokoni hapo, mwenyekiti huyo amesema kuwa uongozi wa ushirika wa soko hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamekuwa wakitoa elimu kwa wafanyabiashara jinsi ya kujiepusha na majanga ya moto.

“Tumepewa cheti cha pongezi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuchukua hatua ya kutoa elimu pamoja na kuweka vifaa muhimu vya kuzimia moto ikiwemo fire extinguisher na maji lita elfu 10 ya ziada.”

Hata hivyo, amewasihi wafanyabiashara wa soko hilo kuendelea kutoa huduma kwa upendo kwa wateja wao, kuzingatia ubora wa bidhaa pamoja na kupanga bei nafuu ili kuwavutia wateja kutoka maeneo mbalimbali mkoani Dar es Salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo akiwemo Frank Zabroni, Mudi Mtaremwa, Victoria James Kyando pamoja na Abdunuri Shomari wamesema kuwa soko hilo lina miundombinu iliyochakaa hivyo kulingana na ukubwa wa soko hilo inahitajika kujengwa soko la kisasa ili waweze kufanya vizuri biashara zao.



No comments