WANANCHI KATA YA KIVULE WAPONGEZA KUFUFULIWA KWA SOKO LA KEREZANGE
Na Mussa Augustine.
Diwani wa Kata ya Kivule CPA Rajab Shabani Manyinya amesema kuwa juhudi za kufufua Soko la Kerezange zimeanza kuzaa matunda kufuatia kikao muhimu kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya masoko na minada pamoja na Wananchi wa kata hiyo.
Akizungumza Aprili 22,2026 baada ya kikao hicho CPA Manyinya amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili kwa pamoja na Wananchi na kuweka mikakati ya kufufua Soko hilo sambamba na kuanzisha rasmi mnada sokoni hapo hatua inayotarajiwa kuongeza shughuli za biashara ili kukuza kipato cha Wananchi pamoja na uchumi wa Jiji la Dar es salaam.
“Ushiriki wa Wananchi pamoja na maofisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam umetupa matumaini makubwa na kututia nguvu ya kusonga mbele na mpango huu muhimu kwa maendeleo ya wananchi wetu hivyo naamini tutafanikiwa kufufua soko hili na kuanzisha mnada ambao utakua unafanyika siku ya jumatano kila wiki” amesema CPA Manyinya.
Aidha diwani huyo amebainisha kuwa Wananchi wameonesha mwitikio chanya kwa kuchangia maendeleo ya soko hilo ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi laki moja na nusu hukusanywa kwa wiki kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kuwezesha upatikanaji wa magari ya minada.
Katika hatua nyingine CPA Manyinya amesema kuwa wanatarajia kufanya uchaguzi wa Viongozi wa soko hilo katika nafasi za Mwenyekiti Katibu na Wajumbe ambao watakua na jukumu la kusimamia kwa ufanisi shughuli za soko na mnada ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Hata hivyo amewahakikishia Wananchi wa Kata ya Kivule kuwa mabadiliko chanya yanakuja akiwataka kuendelea kuwa na uvumilivu huku juhudi za maendeleo zikiendelea.
Nae Mwenyekiti wa Minada Mkoa wa Dar es salaam Hamad Nakwambe ambaye pia alikua amemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dar es salaam amesema kuwa Mkoa wa Dar es salaam una magulio 43 ambapo Jiji la Ilala likiwa na magulio 13 na kwamba mnada utakaofumguliwa katika Soko la Kerezange itafikisha idadi ya magulio 14 kwa Jiji la Ilala.
“Tunategemea tukileta mnada hapa Kerezange itasaidia kuwaondoa wafanyabiashara kwenye maeneo yasiyo rasmi kwa kuunga mkono kauli ya Rais Dkt Samia ya kuhakikisha wafanyabiashara wote wanakua kwenye maeneo rasmi” amesema Nakwambe.
Vilevile Mhasibu Mkuu wa Masoko Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Ally Seif amesema kwamba Serikali ya Jiji hilo unataka miradi yote iende vizuri hivyo wao kama watendaji watahakikisha soko hilo linaendelea vizuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wananchi waliohudhuria mkutano huo akiwemo Mwajuma Abdalah amesema kuwa amefurahishwa na hatua ya kufufua soko hilo ambapo litasaidia Wananchi kupata huduma mbalimbali pamoja na kufanya biashara zitakazowakwamua kiuchumi.
“Kwa juhudi za uongozi wa sasa wa kata yetu tunaona wazi kuwa soko linaanza kufufuka na kupata uhai mpya hatua hii inatupa matumaini makubwa ya kuendeleza soko letu tunashukuru sana tutaendeelea kushirikiana na serikali kulinda soko letu.”




No comments
Post a Comment