JOYCE NGATOPA AMUANGUKIA RAIS DKT. SAMIA

Joyce Ngatopa akiwa na mtoto wake mwenye ulemavu Alhaj Seif Lulile
*Amuomba msaada wa kumjengea nyumba ya kuishi na mwanae mwenye ulemavu.
Na Mussa Augustine, Dar es Salaam
Joyce Yohane Ngatopa (49), mkazi wa Mtaa wa Kigogo Kati, Manispaa ya Kinondoni, amemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wadau mbalimbali kumsaidia kujengewa nyumba ya kuishi yeye na mtoto wake mwenye ulemavu wa viungo uliomfanya ashindwe kutembea tangu alipozaliwa mwaka 2013.
Ombi hilo amelitoa Aprili 23, 2026 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea nyumbani kwake alikopanga, na kujionea hali ngumu ya maisha anayopitia.
Mama huyo ana watoto watatu ambao ni Agness Chovecho, Abubakar Seif Lulile na Alhaj Seif Lulile ambaye ana ulemavu.
Amesema tangu mwaka 2013 mtoto wake alianza kupata changamoto ya kushindwa kutembea.
Alimpeleka katika hospitali za CCBRT na Muhimbili kwa matibabu, ambapo ilibainika kuwa hawezi kutembea kutokana na kovu kwenye ubongo lililotokana na kushindwa kulia wakati wa kuzaliwa

Joyce Ngatopa akiwa na mtoto wake mwenye ulemavu Alhaj Seif Lulile,huku akionesha poti anayotumia mtoto huyo kujisaidia.
Ameeleza kuwa alishauriwa mtoto huyo afanyiwe mazoezi ya viungo na apewe dawa za kumkinga dhidi ya degedege, hivyo anatumia vidonge 90 kwa mwezi.
“Huyu mtoto nambeba kumpeleka shule ya Lutinda na kumrudisha nyumbani tangu akiwa na miaka minne hadi sasa ana miaka 13. Sina msaidizi,maisha yangu ni ya shida,mtoto amekua mkubwa kumbeba mgongoni,na mazingira ninayoishi si rafiki,tumepanga chumba kimoja tunacholala wote,” amesema Joyce huku akilia.
Ameongeza: “Naomba msaada wa bajaji au bodaboda ya kumpeleka mtoto shule na kumrudisha.Mazingira ya ninapoishi hata bodaboda au bajaji haiwezi kufika. Mtoto hawezi kuchuchumaa, anajisaidia kwenye poti.”
Joyce Ngatopa akionesha hati ya kiwanja alichonacho Mlandizi Mkoani Pwani.
Aidha, amesema anamiliki kiwanja Mlandizi, Mkoani Pwani, lakini hana uwezo wa kujenga nyumba yenye mazingira rafiki kwa mtoto wake na familia kwa ujumla.
“Naomba Serikali, wabunge, mawaziri, wasanii na Watanzania kwa ujumla wanisaidie. Napata shida sana, hata baba wa watoto hawa hawezi kufanya kazi kutokana na matatizo ya kiafya, na tunaishi chumba kimoja,” amesema.
Ameeleza kuwa changamoto hizo zimemuathiri kisaikolojia na wakati mwingine hukosa chakula au hupata mlo mmoja kwa siku kutokana na hali duni ya maisha.
“Nashindwa kufanya biashara kwa sababu muda mwingi nipo shuleni kumhudumia mtoto. Anapotaka kujisaidia nampeleka chooni, kisha narudi naye nyumbani wanapoachiwa saa 9 alasiri,” amesema.
Kassim Omary RamadhanKwa upande wake, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kigogo Kati, Kassim Omary Ramadhan, amesema mama huyo alishafika ofisini kueleza changamoto zake na hatua zimeanza kuchukuliwa.
“Ni kweli mama huyu amepanga na mazingira ya nyumba za kupanga ni changamoto kwa mtoto wake,tumezungumza na wadau ili apate angalau chumba na sebule,tayari ana kiwanja,na tumewaomba wadau mbalimbali akiwemo Salehe Medy, Ahmed Matofali na Sheikh Harib kusaidia vifaa vya ujenzi,tunachosubiri ni utekelezaji wa ahadi zao,”amesema Ramadhan.
Diwani kata ya Kigogo Nassibu LimiraNaye Diwani wa Kata ya Kigogo, Nassibu Limira, amesema kata hiyo imekuwa ikimsaidia kwa misaada midogo kupitia wadau mbalimbali, lakini mahitaji yake ni makubwa.
“Mume wake alipata matatizo ya kiafya baada ya kufanya kazi za nguvu, hivyo mama ndiye anayehangaika kwa sasa kwa kufanya biashara ndogo ya bagia inayomuingizia shilingi elfu tano au sita kwa siku,huku akitakiwa kugharamia usafiri wa mtoto kwenda na kurudi shule,” amesema Mh.Limira
Ameongeza kuwa anatoa wito kwa makampuni, mashirika na watu binafsi kujitokeza kumsaidia mama huyo, ikiwemo kumpatia bajaji ili aweze kujifunza kuendesha, kumpeleka mtoto shule na kutafuta kipato.



No comments
Post a Comment