MSIBA MZITO TANZANIA LEO,MPAMBANAJI WA WANYONGE AFARIKI DUNIA,SOMA HAPO KUJUA
MWENYEKITI wa
Chama cha National League for Democracy (NLD) ambaye pia ni mgombea ubunge
Jimbo la Masasi mkoani Mtwara, Dk. Emmanuel Makaidi amefariki dunia mchana huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).
Mke wa marehemu, Modesta Makaidi,
amethibitisha kifo cha Dk. Makaidi akisema “kimetokea katika hospitali ya
Nyangao, kiasi cha saa 9 mchana.”
Modesta amesema walimpeleka hospitali haraka Dk. Makaidi baada
ya hali yake kubadilika ghafla nyumbani kwake mjini Masasi wakati akijaandaa
kutekeleza ratiba yake ya shughuli za kampeni ya uchaguzi.
“Ni kweli Makaidi amefariki, kama dakika 45 zilizopita. Mimi ni
mke wake naitwa Modesta Makaidi,” amesema alipopigiwa simu na mwandishi wa
habari hizi kuulizwa juu ya taarifa zilizopatikana awali kuhusu hali ya Dk.
Makaidi.
Modesta amesema “juzi wakati Makaidi akiwa anaenda Kata ya
Mbonde, ghafla alijisikia vibaya. Tukampeleka zahanati ya Best ambako
ikabainika ana presha kubwa. Akapewa dripu. Jioni akaruhusiwa. Leo akaamka
vizuri, lakini hali yake ikabadilika. Ndipo tukampeleka hospitali.”
Aidha, Khamis Hamad, Katibu Mwenezi na msemaji wa NLD, ambaye
awali alipopigiwasimu kuulizwa taarifa hizo alishtuka akisema hakuwa na habari,
alithibitisha kuwa tayari chama kimepokea taarifa na kwamba walitarajia kufanya
kikao jana kujadili namna ya kushiriki katika msiba huo.
“Ni kweli, tumethibitisha kifo cha Mwenyekiti wetu, Dk. Makaidi.
Tunajiandaa kuelekea Ngome kufanya kikao pamoja na vyama washirika wa Ukawa, na
baadaye kwa familia yamarehemu Dk. Makaidi. Na tutatoa taarifa kadri
zitakavyopatikana,” amesema Khamis.
Dk. Makaidi aliteuliwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
kugombea ubunge jimbo la Masasi likiwa moja ya majimbo matatu ambayo chama
hicho kilipata katika mgao wa viti vya ubunge, uliosimamiwa na muungano huo
unaoshirikisha pia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha
Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Majimbo mengine ambayo NLD ilipewa katika mgao wa maridhiano wa
Ukawa ni Ndanda na Lulindi yote yakiwepo mkoani Mtwara.
Hata hivyo, ugombeaji wake ulipata kikwazo baada ya wananchi
jimboni kumgomea.
Wananchi hao walitamka mbele ya mgombea urais anayewakilisha
Ukawa, Edward Lowassa kwamba chaguo lao ni Ismail Makombe (Kundambanda),
aliyeteuliwa na CUF kabla ya mgao wa majimbo kutangazwa.
Lowassa ambaye alipita Masasi wiki tatu zilizopita kuomba ridhaa
ya wananchi, alitoa fursa kwa wagombea wote wawili kuhutubia wananchi kwenye
mkutano huo na akawauliza ni yupi watakaemchagua, wakajibu “tunamtaka
Kundambanda.”
Dk. Makaidi aligoma hata Lowassa alipotoa kauli kuwa angeachia
uamuzi wa wananchi; aliondoka mkutanoni na akashutumu alichoita mpango wa
hujuma unaolenga kunufaisha adui zake Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aliendelea kufanya kampeni na akaapa kuendelea mpaka siku ya
mwisho kwa kuwa anauhakika “nitaiangusha CCM.”
Dk. Makaidi aliungana na viongozi wakuu wa vyama vya UKAWA tangu
wakati wa Bunge Maalum la Katiba akiwa amepinga mkakati wa CCM kuvuruga Rasimu
ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na maoni ya
wananchi.
Wakati fulani Dk. Makaidi alisema wazi kuwa ameamua kuungana na
UKAWA kwa sababu anaamini Tanzania inahitaji mabadiliko sasa.
Akiwa mmoja wa wenyeviti wenza wa umoja huo, alijijengea
umaarufu kwa hatua yake hiyo huku akitajika zaidi kwa kaulimbiu ya chama chake
ya “NLD motomoto moto.”
Siku ambayo Lowassa alitambulishwa rasmi kujiunga na Chadema,
katika salamu zake za pongezi, Dk. Makaidi alimwambia Lowassa, “sasa umekuja
huku kwetu itabidi utufuate sisi kwa haya tunayoyapigania UKAWA, yale ya kule
CCM uyaache kule.”
Kifo cha Dk. Makaidi kitasababisha uchaguzi wa jimbo hilo
kuhairishwa, na kjuwa jimbo la tano la ubunge uchaguzi wake kuhairishwa baada
ya wagombea kufariki. Majimbo hayo ni Lushoto mgombea aliyefariki, Mohamed Mtoi
(Chadema), Handeni Mjini mgombea Dk. Abdallah Kigoda (CCM), Ulanga Mashariki
mgombea ni Celina Kombani (CCM) na Arusha Mjini, Estomih Malla (ACT).
Hakuna maoni
Chapisha Maoni