JK ALIKOROGA TENA NA UKAWA,ATANGAZA VITA NA WAPIGA KURA,NI WALE WATAKAOBAKI KITUONI,SOMA HAPO KUJUA
Rais Jakaya Kikwete (katikati) akiwasili katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma katika maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge na Kumbukumbu za kifo cha Mwalimu Julius Nyerere |
RAIS Jakaya Kikwete ametangaza vita na wapigakura watakaobakia maeneo
ya vituo vya uchaguzi baada ya kupigakura zao, akisema watakuwa wanavunja
sheria za nchi. Anaandika Charles William … (endelea).
Akiwa ni Amiri Jeshi Mkuuu wa majeshi ya
ulinzi na usalama, Rais Kikwete ameonya kwamba watakaokaa vituoni
‘watashughulikiwa’ na serikali.
Ametoa tamko hilo
mchana leo alipokuwa akihutubia kilele cha mbio za mwenge wa uhuru kwenye
Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa
Habari, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara pamoja na Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Chiku Galawa.
Rais ambaye dhahiri
ametoa majibu ya kilichojitokeza kuwa ni malumbano yanayoendelea kati ya Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jeshi la Polisi na Serikali kwa upande mmoja na kwa
upande wa wili viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA).
Wakati Tume na
serikali wamekuwa wakisisitiza kuwa wananchi hawatakiwi kukaa maeneo ya karibu
na vituo vya uchaguzi baada ya kupiga kura, viongozi wa UKAWA – Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD – wanahimiza watu kubakia vituoni masafa ya mita 100 nje ya
vituo kwa ajili ya kujiandaa kulinda kura za wagombea wao.
Oktoba mosi mbele
ya umati mkubwa wa wananchi kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, “mkishapiga kura, wanawake
nendeni nyumbani, wanaume mtakaa umbali wa mita 200 unaotakiwa kisheria na
mtakaa hapo mkilinda kura zenu mpaka matokeo yatakapopatikana.”
Viongozi wa UKAWA
wanasema kwamba hakuna haki kwa wananchi kuambiwa waende kusubiri matokeo ya
uchaguzi majumbani kwao wakati kuna dalili nyingi za kutokuwepo uhakika kuwa
Tume itamudu kuzilinda kura dhidi ya kuchakachuliwa.
Tume ya Uchaguzi
imekuwa ikijitahidi kuonesha uwazi katika mifumo ya ushughulikiaji kura ingawa
imekataa katakata kuonesha mifumo ya ujumlishaji wa kura wakati daftari lenyewe
imelitoa jana kwa ajili ya kuhakikiwa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi.
Katika hali hiyo
ya malumbano, Rais Kikwete anajitokeza kusema kuwa serikali haitamvumilia mtu
yeyote anayekusudia kuvunja sheria kipindi cha uchaguzi kwa kuwa hayuko tayari
kuona demokrasia “inatekwa nyara.”
Rais analalamika kwa
kuhoji, “Mnakaa nje ya vituo vya kupigia kura kufanya nini? Wewe upo nje ya kituo,
utalindaje kura? Mtu wa kulinda kura ni wakala wa chama chako, labda kama ni
mzembe.”
“Mipango ya
kuvuruga amani inafahamika na itadhibitiwa watu wao wapige kura mapema na
wanawake waende nyumbani, wanaume wabaki kulinda kura, wanadhani wengine hawawezi
kuwahi… msiilazimishe serikali kufanya mambo yasiyopendeza, wanaotaka kufanya
fujo hawatavumiliwa waatadhibitiwa,” amesema.
“Mkishapiga kura
nendeni nyumbani Tume ya Uchaguzi imeshafafanua vizuri suala hili… tofauti na
hapo ni vurugu, na sisi kama serikali hatutawavumilia watakaokiuka sheria.
Tutawadhibiti kwa nguvu ileile watakayoitumia,” amesema katika hotuba
iliyotangazwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.
Rais Kikwete
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa amedai suala la kulinda kura ni mkakati wa
viongozi wa vyama vya siasa kuwazuia baadhi ya wananchi kupigakura baada ya
wanachama wa vyama vyao kupiga kura.
Huko nyuma,
viongozi wa UKAWA walishatangaza kuwa watayatangaza matokeo ya kura za urais
hata kabla ya Tume, kwa kuwa sheria inaruhusu kutangaza kura zinazokamilika
kuhesabiwa na kuidhinishwa na wagombea na mawalaka wao almuradi sio matokeo ya
majimbo yote.
Habari hii kwa hisani ya Mwanahalisi oline
Maoni 1
labda tukumbushane tuu kinachoendelea, kwamba ni mtihani mkubwa wa chama dola ccm,walioitawala tanzania kwa miaka 55 wanapokaribia kuangushwa katika uongozi-nchi na watanzania walio wengi jumapili tarehe 25 octoba 2015 kwenye uchaguzi mkuu.hakuna mwana-mabadiriko mwenye akili timamu anayewazia fujo ni ndoto,hata chembe.tunamwomba mwenyezi mungu siku hiyo iwe siku ya shwari kweli-kweli amani itawale ili watanzania tujitokeze kwa wingi sana sana kukata kiu yetu.penye fujo utapigaje kura? tunafanyiwa njama,mtego,tuwe makini sana. sisi na lowassa,lowassa na sisi. tujipe moyo mkuu tutavuka salama munngu yupo upande wetu,inshallah heri.
Chapisha Maoni