ACT WAZALEONDO YAONYWA SOMA HAPO KUJUA
Karatu. Baadhi
ya wakazi Jimbo la Karatu, mkoani Arusha wameonyesha kukerwa na kitendo cha
mgombea mwenza wa Chama cha ACT-Wazalendo, Hamad Yusuf cha kumponda mgombea
urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Wamekitaka chama hicho kunadi sera zake badala ya
kumzungumzia mtu kinapoendelea na kampeni zake jimboni humo, la sivyo watasusia
mikutano yao ya kampeni.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika juzi
katika Viwanja vya Mazingira Bora, mgombea huyo wa ACT - Wazalendo, alidai kuwa
Lowassa amekwenda Chadema siyo kwa kutaka urais, bali kutafuta kusafishwa
kutokana na kashfa ya ufisadi.
Alipomaliza kutoa kauli hiyo, baadhi ya watu
waliokuwa wakimsikiliza walianza kuondoka uwanjani hapo wakidai kuwa amewakera
kwa kauli yake hiyo.
Mkazi wa Karatu Stendi, Simon Jackson alisema mgombea
huyo asiwavuruge, hawakuja kusikiliza tuhuma na matusi katika mkutano huo bali
sera.
“ACT-Wazalendo isituvuruge, hatuwezi kumkataa
Lowassa kwa sababu eti alikuwa fisadi, mbona hawajamshtaki mpaka sasa, atuambie
chama chake kitatufanyia nini,” alisema Jackson.
Alisema mgombea mwenza huyo anapaswa kujenga hoja za
kuwashawishi wananchi.
Naye Mariam Olesaiki, alisema Karatu wanahitaji
kiongozi atakayewaletea mabadiliko ya kuwa na serikali ya majimbo aliyodai
itawapatia fursa ya kufaidika na rasilimali zao moja kwa moja.
“Nchi yetu ina vyanzo vingi vya mapato, tunachotaka
kusikia katika mikutano ya kampeni ni fedha za Ngorongoro zinachangia kiasi
gani kwenye bajeti ya Taifa siyo fulani kafanya nini,” alisema Philemon Urio.
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea urais wa ACT
- Wazalendo, Anna Mghwira alisema wakati umefika wa kuiondoa CCM madarakani.
Alisema kazi hiyo itashindikana kama wananchi
hawatataka kubadilika na kuendelea kuipa kura CCM.
“Liwake jua inyeshe mvua, lazima tuiondoe CCM
madarakani,” alisema na kuongeza:
“Huu ni mwaka wa mabadiliko na ni wa wanawake,
tunahitaji rais mwanamke au sio baba zangu na mama zangu,” aliuliza mgombea
huyo na kujibiwa “ndiyo”.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni