ZITTO KABWE AMPOPOA MAGUFULI NA CCM YAKE,ASEMA WATANZANIA WATAKUJA JUTA,SOMA HAPO KUJUA
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Chama
Cha Mapinduzi (CCM) hata kipate malaika hakiwezi kubadilika, hivyo dawa pekee
ni kukiondoa jumla madarakani.
Akizungumza jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kituo
cha basi Tabata Segerea, Zitto alisema matatizo mengi ya nchi yamesababishwa na
sera mbovu za CCM ambazo baadhi ya wagombea wake ndio waliokuwa wakizitunga,
kuzitetea na kuzitekeleza.
“Kuna ambao wamekuwa watawala tangu tupate uhuru na bado wanataka
waendelee kutawala, ukiwauliza wanasema tupeni tena kipindi kingine.
“Sisi tunataka wote waondoke, tunataka tuweke mwanzo mpya katika nchi
hii ndio maana hata ilani yetu imejikita kutatua changamoto mbalimbali
zinazotukabili,” alisema Kabwe.
Zitto aliyewasili viwanjani hapo saa
10:14 jioni na kuanza kuhutubia saa 11:13 jioni, alisema taifa linakabiliwa na
changamoto kuu nne ambazo ni umaskini, huduma mbovu za jamii, kukosekana kwa
umoja wa kitaifa na ufisadi.
“Leo hii tumekua na uchumi ambao hauzalishi ajira na kusababisha vijana
wengi wanaomaliza masomo yao kuhangaika kutafuta kazi. Ni kwanini uchumi ambao
unakua kwa kasi hauzalishi ajira,?” alihoji Kabwe.
Alisema hivi sasa nchi imekuwa na matabaka kwenye huduma za jamii kama
vile elimu na afya na kusababisha Taifa kuwa la masikini na matajiri.
“Leo hii watoto wa masikini na matajiri hawakutani, wa matajiri wanasoma
shule zao halikadhalika na wa masikini…matajiri wanafundishwa elimu bora wanaandaliwa
kuja kuwatawala masikini.
“Rushwa kubwa ndio inalitafuna taifa hili, mwaka jana zilitengwa Sh
bilioni 546 kwa ajili ya kununulia madawa muhimu lakini ni Sh bilioni 36 tu
ndizo zimetolewa, kuna wajanja wachache wamezifanyia ufisadi zile fedha,” alisema.
Kiongozi huyo wa ACT, alisema wamejipanga vizuri na wamesimamisha
wagombea ubunge 219 nchi nzima hivyo akawataka Watanzania kuwapima kulingana na
uwezo wao kisha kufanya uamuzi.
Awali mgombea ubunge katika Jimbo
la Segerea, Mohamed Mwikongi, alisema akifanikiwa kushinda kiti hicho
ataanzisha mfuko wa maendeleo wa Segerea na kuwahamasisha wananchi wajiunge
katika vikundi ili wapate mikopo.
“Nitaangalia upya mfumo wa wazazi kuchangia gharama za elimu katika
shule za umma na kuzipunguza ili ziendane na hali halisi ya utendaji,” alisema
Mwikongi.
Naye mjumbe wa chama hicho, Terry
Gbemundu, alisema Watanzania wengi wameaminishwa kuwa ni masikini lakini hakuna
umasikini wowote nchini.
“Tunaaminishwa hivyo ili tuibiwe tuzidi
kukandamizwa, akili zimedumazwa lakini sasa uamuzi mnao kwenye sanduku la kura.
“Atakayechagua kijani (akimaanisha CCM)
ambayo imetawala kwa miaka 54 bila mafanikio sijui itabidi tukapimwe akili,”
alisema Gbemundu.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni