UCHAGUZI MKUU 2015 UNAPASWA KUWA SHIRIKISHI- WANAHARAKATI
Sehemu ya wanahabari wakifuatailia taarifa hiyo ya wana FEMACT. |
Wakati joto la uchaguzi
kuelekea Oktoba 25 likizidi kupanda, kuna kila dalili kuwa msingi mkuu wa
Demokrasia ya uchaguzi ambao ni ushiriki wa kila raia katika mchakato huo
unalegalega. Pamoja na maandalizi yanayoendelea kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka
huu, yapo mambo kadhaa ambayo yanahitaji kuwekwa sawa. FemAct imeamua kuchangia
katika kuleta suluhu ya baadhi ya mambo hayo kwa kuchambua changamoto zilizopo
na kupendekeza suluhu.
Taarifa hii ni sehemu ya mchango huo wa
Mtandao wa FemAct. Uchaguzi ni suala la kikatiba. Kwa mujibu wa ibara ya 21(1)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kila raia anayo haki ya kushiriki
katika shughuli za utawala wa nchi. Aidha, ibara ya 8 inabainisha kuwa Wananchi
ndio msingi wa mamlaka yote ya nchi na kwamba serikali itapata madaraka na
mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.
Kiutendaji, njia kuu
kwa wananchi kukasimisha mamlaka na madaraka yao ni kwa kuchagua viongozi wao
kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa miaka yote ya uhai wa taifa letu tangu
uhuru na kwa uwazi zaidi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Uchaguzi ndiyo njia kuu
kwa wananchi kutoa ridhaa yao kwa serikali kutekeleza mipango ya maendeleo
katika kipindi cha uongozi kinachowekwa kikatiba na kisheria. Tanzania inaingia
katika uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi kwa mara ya nne mwaka huu
uchaguzi wa kwanza ukiwa ule wa mwaka 1995. Pamoja na miaka 20 ya demokrasia ya
Vyama vingi, ukuaji wa usawa wa Kijinsia bado unasuasua.
Zipo dalili kuwa wanawake, vijana na Watu
wenye Ulemavu wanakwamishwa kushiriki na kushindana kutokana na vikwazo
mbalimbali. Kwa mfano, vyama vya siasa, ambavyo ndiyo njia pekee ya kuwania
uongozi wa kuchaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 39 (1) (c) na ibara ya 69 (1) (b)
ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, vimetawaliwa na mifumo
kandamizi ikiwemo mfumo dume ndani ya taasisi hizo ukiwa kikwazo kikuu kwa
ushiriki wa makundi hayo kama wagombea wa uchaguzi.
Kati ya vyama takribani 24 vyenye usajili
halali, ni chama kimoja tu cha ACT kina mwanamke kama Mwenyekiti wa Chama, huku
vingine viwili vikiwa na makatibu wakuu wanawake vikiwemo ADC na DP.
Kwa vyama vingine, safu
nzima ya uongozi ndani ya chama kuanzia mwenyekiti hadi wajumbe wa vikao muhimu
vya chama zimeshikiliwa na wanaume.
Hii inapelekea ukakasi na kuminya sauti za
wanawake katika maamuzi mengi ikiwemo uteuzi wa wagombea katika nafasi
mbalimbali wakati wa uchaguzi. Pamoja na juhudi hizi kwa baadhi ya vyama FemAct
inatoa angalizo kuwa uteuzi wa wanawake usiwe kwa kuzingatia idadi tu bali pia
kuwe na fursa ya kushiriki kikamilifu katika kutoa mamuzi kwenye ngazi zote.
Mtandao kupitia
mashirika wanachama imekua ikifanya mafunzo kwa watangaza nia na viongozi wa
kisiasa kuhusu masuala ya uongozi na demokrasia. Mafunzo hayo yaliwalenga
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Katika tamthmini ya awali, hasa baada
ya mchakato wa ndani ya vyama kuanza, makundi hayo yamekua yakikabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na lugha za matusi na za kudhalilisha,
dharau na kejeli, ukatili wa kijinsia na wakati mwingine rushwa ya ngono,
matumizi makubwa ya fedha n.k.
Hali hiyo inaashiria
kutokuwepo kwa mazingira rafiki kwa makundi hayo jambo linaloweza kusababisha
kukata tamaa kwa makundi hayo.
Kwa hali inavyoonekana
mwaka huu, ni dhahiri kuwa idadi ya wanawake watakaoteuliwa kupeperusha bendera
za vyama vyao katika nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani itakuwa
ndogo sana kwa sababu ya visingizio kadhaa. Ndiyo maana, uamuzi wa Chama cha
Mapinduzi kumsimamisha mwanamke katika nafasi ya mgombea mwenza wa urais
kitendo ambacho kinatoa hali inayofanya kuwepo uwezekano wa kuwa na Makamu wa
Rais Mwanamke Tanzania ni jambo la kupongezwa, tulitarajia na vyama vingine vya
siasa kuzingatia usawa wa kijinsia katika uteuzi wao. Bila kujali kama mwenza
huyo na mgombea wa chama chao watashinda au la, historia iliyowekwa itabaki
vizazi na vizazi ikionesha jinsi Tanzania ilivyofikia utayari wa kuwa na Makamu
wa Rais mwanamke. FemAct inaendelea kudai kama ilivyokua tangu mchakato
umeanza, kuwa chama chochote kitakachoingia madarakani kihakikishe kuwa moja
kati ya nafasi kuu tatu yaani nafasi ya uraisi, makamu wa raisi na waziri mkuu
ishikiliwe na mwanamke. Kwa upande wa Wanawake ambao ni asilimia 50 na Vijana
ambao ni zaidi ya asilimia 60 kama wapiga wakuu katika uchaguzi, hamasa ya
wanawake kujitokeza imeonekana kuzidi kupanda. Katika zoezi la uandikishaji
wapiga kura linalokamilishwa hivi sasa, wanawake wengi walionekana katika
misururu mirefu kuanzia alfajiri huku wengi wakiwa wamebeba watoto. Hata katika
uchaguzi uliopita mwaka 2010 ambapo ni asilimia 42% tu ilijitokeza kupiga kura
kumchagua Rais wa Tanzania, takwimu zinaonesha kuwa wengi katika hao walikuwa
ni wanawake, vijana na wasichana. Hamasa kubwa iliyoonekana wakati wa
uandikishaji inaashiria kuwa mwitikio wa jumla katika uchaguzi wa mwaka 2015
unaweza ukawa mara mbili ya mwaka 2010. Hili ni jambo la afya kwa uchaguzi na
ukuaji wa Demokrasia nchini. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa maandalizi
yaliyobaki kuelekea siku ya upigaji kura yanahakikisha kuwa kunakuwa na hali ya
amani, utulivu na wezeshi kwa mazingira rafiki kuwezesha wananchi kupiga kura.
Kwa hatua zilizokamilika mfano uteuzi ndani ya vyama umeonesha dalili za
uvunjifu wa amani hivyo tunatoa angalizo kwa serikali, vyama vya siasa na
wapiga kura kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika kwa amani na utulivu kwani
makundi yanayoathirika zaidi katika uvunjifu wa Amani ni wanawake,watoto na
watu wenye ulemavu. Kuhusu uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali za
uongozi, Mtandao unaona changamoto kubwa mbili. Kwanza, matumizi mabaya ya
fursa ya viti maalum vya wanawake katika nafasi ya ubunge na udiwani, ubunge na
uwakilishi; pamoja na matumizi makubwa mno ya fedha katika uchaguzi kiasi cha
kuwanyima fursa wanawake, vijana na wasichana kumudu kugharamia michakato ya
kugombea katika uchaguzi. Taarifa kwamba baadhi ya vyama vimekuwa vikiwazuia
wanawake kugombea nafasi za viti vya majimbo na udiwani kwa kisingizio kuwa wao
wasubiri viti maalum ni za kusikitisha sana. Dhana ya viti maalum ni kuwezesha
kunyanyua idadi ya wanawake wanaoshiriki katika siasa. Aidha, viti maalum
vinapaswa kuwa ni nafasi za kujengea uwezo wanawake na wasichana na sio
kuvifanya kuwa vya kudumu. Viti maalum bila juhudi nyingine za kupanua fursa za
wanawake kushitriki Siasa ni sawa na kazi bure. Pia, mifumo ya kuwezesha
wagombea kufadhili shughuli za uchaguzi inapaswa kuwa jukumu la vyama na siyo
mgombea mmoja mmoja. Hii itapunguza uwezekano wa wagombea kuumiza vichwa
kufikiria wapi wapate fedha za kufanyia maandalizi ya uchaguzi ikiwemo
kuendesha kampeni. Mfumo wa sasa ambapo rasilimali za uchaguzi ni jukumu
binafsi la mgombea unashawishi na kulea wizi wa mali za umma, rushwa na
ufisadi. 3 Jambo jingine la kuliangaliza taifa wakati huu ni kuhusu siasa
nyepesi za kuhamahama vyama, sambamba na kukosekana kwa mfumo mbadala wa
wagombea huru. Hili nalo limekuwa kikwazo kwa wanasiasa makini ambao wangependa
kugombea bila kudhaminiwa na vyama vya siasa. Kuwepo kwa wanasiasa wanaohama
vyama baada ya majina yao kuenguliwa katika vyama vyao kupitia kura za maoni,
licha ya kuwa ni haki yao kufanya hivyo, ni bora vyama vya siasa vikahakikisha
kuwa vinakuwa na utaratibu wa kuchuja watu wanaokimbilia katika vyama vyao
katika misingi ya kiuwajibikaji na uongozi bora nas si kwa maslahi binafsi.
Kutokana na hili, kunahitajika elimu ya uraia inayoweka bayana misingi mikuu ya
demokrasia ya uchaguzi ambapo anayegomea anapaswa kujua kuwa kunakushinda au
kushindwa na kuwa tayari kukubali matokeo. Vinginevyo, dhana nzima ya
demokrasia inakuwa haina maana kwa kuwa wanaoshindwa wanakuwa chanzo cha
migogoro na fujo kiasi cha uwezekano wa kutoweka kwa amani.
Imetolewa, Lilian Liundi Abdullah Othman
Mkurugenzi Mtendaji, TGNP Mtandao Mwenyekiti – FEMACT Mratibu, FEMACT Kwa Niaba
ya; 1. Life Skills Association (LISA) 2. Tanzania Education Network (TENMET) 3.
Tanzania Citizens’ Information Bureau (TCIB) 4. Journalists Environmental
Association of Tanzania (JET) 5. Binti Leo 6. African Youth 7. African Life
Foundation 8. Pwani - DPA
Hakuna maoni
Chapisha Maoni